Dar es Salaam. Wadau wa mazingira na usimamizi wa majanga wametaja sababu za madhara wakati wa mvua ni ujenzi holela katika maeneo ya mikondo ya maji, udhaifu wa usimamizi wa mipango miji na miundombinu isiyo himilivu.
Mbali na hayo, wamependekeza mbinu za kukabiliana na hali hiyo, ikiwamo Serikali kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa kusaidia wananchi majanga yanapotokea.
Wamesema hayo leo Jumatano Aprili 30, 2025 wakichangia mjadala wa Mwananchi X Space uliojadili mada isemayo: ‘Nini kifanyike kupata suluhu ya kudumu ya madhara yatokanayo na mvua’. Mjadala huo umeandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).

Maji yakiwa yametanda eneo la Kariakoo Mjini Unguja kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kisiwani Zanzibar
Miongoni mwa madhara ni uharibifu wa miundombinu, ikiwamo barabara na madaraja, lakini inakuwa neema kwa baadhi ya waendesha pikipiki na bajaji wanaotoza mara mbili ya kiwango cha nauli tofauti na ile iliyokuwa ikitozwa awali.
Mdau wa mazingira, David Levi amesema chanzo cha mafuriko ni wananchi kujenga kwenye mikondo ya maji.
“Mfano maeneo ya Tegeta, Dar es Salaam hadi kuja Boko zamani kulikuwa na mitaro iliyoruhusu maji ya mvua kutembea kwenye njia zake, leo maeneo mengi yamejengwa, ujenzi wenyewe wanaanza kunyanyua ardhi kutafuta usawa na mwisho wa siku maji yanakosa pa kwenda,” amesema.
Mbali ya hayo, amesema mamlaka zinapaswa kutupiwa lawama kwa kutokusimamiwa mipango miji.
“Serikali walitakiwa kusimamia maeneo ya kujenga, tunapata hasara kubwa mvua zikinyesha huharibu miundombinu ya barabara,” amesema.

Amedai vitendo vya rushwa huchangia ujenzi holela wa makazi, hivyo miundombinu kuharibika wakati wa mvua ikiwamo ya barabara na madaraja.
Katika hatua nyingine, baadhi ya makandarasi na watendaji wanatajwa kuchangia uwepo wa mafuriko wakati wa mvua, wakishauriwa kuwa waaminifu na waadilifu wanapotekeleza miradi.
Mdau wa mazingira, Sanday Masubo amesema: “Kila msimu wa mvua tunapata mafuriko, ukiangalia barabara zetu nyingi mitaro ya kupitisha maji ni midogo ikilinganisha na kasi ya maji hata kama ujenzi wa makazi ni holela,” amesema.
Mbali ya hayo, amesema mitaro hiyo haisafishwi hivyo mvua ikinyesha kidogo athari huonekana kwa takataka kutuama.
“Watu wanaojenga holela viongozi wanawajua, wataalamu waliochora ramani wanaangalia na hawakushauri chochote,” amesema.

Amesema wananchi huuziwa viwanja wakati wa kiangazi lakini mvua zikianza kunyesha hakuna anayefanya biashara hiyo.
Nini kifanyike
Mtaalamu wa Udhibiti wa Majanga, Profesa Herbert Qambalo ameshauri kubainisha maeneo hatarishi na kuweka miundombinu himilivu ili kupata suluhisho la kudumu la madhara yatokanayo na mvua.
“Kunatakiwa kufanyika ushirikishwaji mzuri kwa wadau wa maendeleo, Serikali na wananchi na kuweka sera nzuri ya usimamizi, ufuatiliaji na kufanya tathimini ya kina ya maafa. Pia kufanya matumizi bora ya ardhi,” amesema.
Profesa Qambalo amesema sera ya tathimini ya maafa ipo lakini changamoto yake ni utekelezaji, hakuna bajeti ya kuwezesha hilo kufanyika.

“Kinachokosekana ni bajeti ya ufuatiliaji na kufanya ardhi ipimwe, mfano kuna sera ya majanga ya mwaka 2004 na ipo kwenye maboresho ya kuja na sera mpya ya mwaka 2024/2025 lakini sera hizi lazima ziungane na zingine za matumizi ya ardhi kama mipango miji, kilimo na zilenge kuboresha maisha ya watu,” amesema.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Usimamizi wa Maafa, Suleiman Kova amesema hakuna namna ya moja kwa moja ya kudhibiti madhara yatokanayo na mvua, bali njia pekee ni kuyapunguza.
“Hapa Dar es Salaam, kuna sehemu kunaitwa Bonde la Mpunga ambalo ni mapitio ya maji, sasa mvua ikinyesha maji yana sehemu zake za asili na binadamu wa kawaida hawezi kuzuia. Sasa njia hizo asili za maji zinakutana na maendeleo ya miji ikiwamo watu kujenga, ila mvua ikija inapita moja kwa moja.
“Ndiyo maana madhara ya uharibifu wa barabara yanatokea, njia pekee ni Serikali na wananchi kupunguza athari ikiwamo kuzuia vifo visitokee. Hata Serikali ijue wazi kwamba haiwezi kudhibiti kwa asilimia 100 athari za mafuriko,” amesema.
Kova ameshauri kuangaliwa kwa mfumo wa nchi, mabara na dunia ili isisababishe joto ambalo linasababisha mabadiliko ya tabianchi hasa katika karne ya 21 ambayo kuna athari kubwa zimejitokeza kutokana na shughuli za kibinadamu na viwanda.
“Taasisi kama za kwetu, zipo si kupunguza tu bali kutoa elimu kwa wananchi namna ya kujikinga ili wasipate madhara zaidi ikiwamo kupoteza maisha,” amesema Kova aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam.

Mhitimu wa Chuo Kikuu katika fani ya usimamizi wa bima na majanga, Yusuph Mohamed ameshauri Serikali itenge bajeti ya kutosha ya kununua vifaa vitakavyosaidia kupambana na majanga ya mvua pindi yanapojitokeza.
“Kufanya hivi itasaidia kwa sababu kinachoonekana Serikali haijaweka kipaumbele kwa kiwango kinachotakiwa kusaidia wananchi wakikumbana na majanga.
“Dharura ikitokea wanakuja kwenye matukio wakionekana kabisa hajawa kamili na wanaanza kuogopa ile hatari wanayokwenda kukumbana nayo,” amesema.