
Unguja. Wakati Zanzibar ikithibitisha kuanza rasmi kutumika kwa Mfumo wa Taarifa wa Kukabiliana na Maafa (ZDMIS), wadau mbalimbali wamependekeza utumike kama suluhisho la kuwasaidia wananchi kwa kutoa njia bora za kujikinga na maafa kabla hayajatokea.
Pia kuhakikisha waathirika wanawekewa mazingira bora ya kuishi.
Mapendekezo hayo yametolewa leo Alhamisi Mei Mosi, 2025 katika kikao cha kuthibitisha mfumo huo kilichofanyika Mwembe Madema, Mjini Unguja.
Wadau kutoka sekta mbalimbali zikiwamo za Serikali, wamesema ili mifumo hiyo iwe na ufanisi, inapaswa kuunganishwa kusudi zisome taarifa kutoka vyanzo mbalimbali kwa usahihi na kwa wakati.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), Judith Bihondwa amesema ni muhimu mfumo huo kutambua maeneo hatarishi zaidi yanayoathirika wakati wa mvua na majitaka, ili kuwawezesha wananchi wa maeneo hayo kuandaliwa kwa wakati.
“Kwa wananchi ambao maeneo yao yatabainika kuwa hatarini, ni lazima kuwe na maandalizi ya mazingira mbadala. Huwezi kumwambia mtu ahame bila kumpangia anakokwenda. Ni lazima kuwe na utaratibu rasmi wa kuwahamisha,” amesema Judith.
Aidha, amewataka watendaji kufanya uchunguzi wa kina kubaini misaada inayotolewa (pindi yanapotokea majanga kama mafuriko) inaishia wapi, kwa sababu baadhi yake haifikiki kwa walengwa.
Kwa upande wake, Mashauri Shehe Khamis amesema baadhi ya maafa yanayosababisha madhara kisiwani Zanzibar yanatokana na vitendo vya wananchi wenyewe, kama vile uchimbaji wa mchanga holela katika makazi yao bila kujali athari zake.
Amesema mfumo huo unatarajiwa kusaidia kutoa mwongozo wa namna ya kudhibiti shughuli hizo hatarishi ili kuwanusuru wananchi wa maeneo husika.
Naye Suwed Hussein Suwed alipendekeza elimu kuhusu mfumo huo ifundishwe shuleni ili kuwajengea vijana uelewa mapema, kwa kuwa wao ndio watakaokuwa watumiaji wakuu wa mfumo huo katika siku zijazo.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Dk Islam Seif Salum amesema mfumo huo umetengenezwa kwa lengo la kutoa taarifa ya uwapo maafa kabla hayajatokea ili kurahisisha hatua za kukabiliana nayo.
Amesisitiza kuwa sekta mbalimbali zinapaswa kubadilika na kutafuta suluhisho la kudumu kuhusu mafuriko yanayotokea Zanzibar, hasa katika vipindi vya mvua za masika na vuli.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Maafa, Makame Khatib Makame amesema utekelezaji wa mfumo huo umetokana na tathmini ya mifumo iliyopo, ambapo ilibainika kuwa mingi haijawa na uwezo kusomana k kwa ufanisi, hivyo kutotoa taarifa kwa usahihi.