
Morogoro. Uwepo wa mpango wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, usafiri wa treni ya kisasa SGR pamoja na ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere vimetajwa kuwa ni moja ya mipango ya kusaidia kupunguza ongezeko la gesi joto ambapo malengo ni nchi ni kupunguza kwa asilimia 30 mpaka 35 ifikapo mwaka 2030.
Hayo yamebainishwa na Ofisa mazingira mwandamizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Issa Nyashilu kwenye kongamano linalohusu mchango wa Taifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi lililoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, mazingira kwa kushirikiana na Shirika na maendeleo la umoja wa mataifa UNDP.
Ambapo chini ya mkataba wa makubaliano wa Paris wa mwaka 2015 kila nchi inapaswa kuandaa mkataba unaoitwa mchango wa Taifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Dk Nyashilu amesema kupitia mpango wa matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia nchi itaweza kuokoa misitu inayoteketea kwa ajili ya kuchoma mkaa na matumizi ya Kuni na hivyo misitu itabaki salama na hivyo kupunguza gesi joto.
“Kupitia usafiri wa treni ya kisasa ya SGR Kwa kiasi kikubwa imepunguza uchaguzi wa hewa, abiria wanaosafiri kwa safari moja tu ya treni kama wangetumia usafiri wa mabasi ungeweza kuona foleni ya mabasi mangapi ambayo yangebeba abiria hao na pia ni kwa kiasi gani yangechafua mazingira kutokana na moshi na matumizi ya mafuta,” amehoji Nyashilu.
Ameongeza, “hali kadhalika na mradi wa ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere nalo limeweza kupunguza gesi joto hasa kutokana na uwepo wa umeme wa uhakika ambao unaweza kutumika kama nishati safi ya kupikia,”
Naye mkurugenzi msaidizi masuala ya mabadiliko ya Tabia ya nchi ofisi ya Makamu wa Rais Dk Kanizio Mwanyika amesema kutokana na uuzaji wa gesi joto tayari baadhi ya halmashauri zenye misitu ya vijiji zimeanza kunufaika ambapo hadi sasa zaidi ya Sh38 bilioni zimepatikana.
“Ajenga ya Rais Samia Suluhu Hassan ya matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia inakwenda sambamba na biashara ya cabon,” amesema Dk Mwanyika.
Akizungumzia kongamano hilo linafanywa kwa ajili ya kujadili masuala yatakayowekwa kwenye mchango wa Taifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na vipaumbele vitakavyotumika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Kwa upande wake Ofisa na mratibu wa utafiti kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) Dk Hulda Gidion amesema mabadiliko ya tabianchi yanagusa kila sekta na yana muathiri kila mmoja, hivyo kama tume wamekuwa wakihusika kwenye tafiti, bunifu na teknolojia mbalimbali zitakazosaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.