
Dar es Salaam. Chadema kugeukia heandshake? ndilo swali linaloumiza vichwa vya baadhi ya wadau wa siasa, baada ya viongozi wa chama hicho kukutana na waziri mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga anayetambulika kwa historia yake ya siasa za maridhiano.
Jana Jumamosi Machi 22, 2025 Odinga alikutana na viongozi wakuu wa Chadema wakiongozwa na Tundu Lissu.
Katika taarifa yake aliyoichapisha kwenye ukurasa wake wa X, Odinga amesema pamoja na mambo mengine amekishauri chama hicho kuzungumza na Serikali kumaliza tofauti zao.
“Nimefanya mazungumzo na viongozi wa upinzani wa Tanzania walionitembelea. Tumebadilishana mawazo kuhusu uimarishaji wa demokrasia katika bara hili, ikiwa ni pamoja na mchango madhubuti katika maendeleo ya Taifa na vyama ndani na nje ya Serikali.
“Nimewahimiza kutanguliza mazungumzo na ushirikiano wenye kujenga na Serikali yao kwa masilahi ya Taifa na uhifadhi wa demokrasia ya Tanzania,” aliandika Odinga.
Mbali na Lissu, wengine alioambatana nao ni Makamu wake Bara, John Heche na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godless Lema ambao nao walitumia akaunti zao za X kueleza ziara hiyo iliyolenga kubadilishana mawazo katika kampeni yao ya ‘No Reforms, No Election’.
Hatua hiyo, inaibua maswali kwa baadhi ya makada wa chama hicho na wadau wa siasa, wakihoji Chadema itabadili msimamo wake na kurejea kwenye meza ya mazungumzo?
Swali hilo linakuja katika kipindi ambacho tayari kulishakuwa na mazungumzo kati ya Chadema na Serikali na yalikwama kutokana na kushindwa kukubaliana baadhi ya mambo.
Kama hiyo haitoshi, hatua hiyo inakuja kipindi ambacho Chadema ilishatangaza msimamo wake wa kuzuia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, iwapo mageuzi ya kisheria hayatafanyika wakiwa na kampeni ya ‘No Reforms, No Election’.
Kinachosubiriwa ni iwapo kikao cha Odinga na Chadema kitabadili upepo wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Odinga ni mwanasiasa mkongwe nchini Kenya anasifika kwa siasa za maridhiano na ameshafanya hivyo kwa marais wanne tofauti.
Mara ya mwisho ni hivi karibuni baada ya kuingia makubaliano ya nne ya ‘handshake’ na Rais wa Kenya, William Ruto.
Tukio la kihistoria lililozua mjadala, limefanana na mikataba aliyosaini na marais wastaafu; Daniel Moi (2001), Rais wa tatu Mwai Kibaki, , Uhuru Kenyatta (2018) na sasa Mkataba wa Makubaliano (MOU) na Rais Ruto.
Ziara hiyo ya Lissu na wenzake kwenda kwa Odinga zimekoleza mijadala hasa ikizingatiwa mtangulizi wake wa Uenyekiti, Freeman Mbowe alikuwa akikiongoza chama hicho na maridhiano na Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Katika kampeni za uchaguzi wa Chadema uliofanyika Januari 21,2025, Mbowe alituhumiwa kukirudisha chama nyuma kwamba amepewa chochote na Serikali. Mbowe alipinga.
Lissu alisema kwa mazingira ya wakati huu kunahitajika sura mpya na yeye (Lissu) alisema ni mtu sahihi na katika maelezo yake amekuwa akisema hatahitaji mazungumzo ‘ya mapendano’, zaidi watatumia umma wa wananchi kuamua mambo.
Hata hivyo, wanazuoni na wachambuzi wa siasa waliozungumza na Mwananchi leo Jumapili Machi 23, 2025 wamekuwa na maoni mseto, baadhi wakisema sio jambo kuonana na Odinga, lakini ni vema Chadema wakatumia muda huu kujiandaa na chaguzi wa Oktoba.
Lakini mchambuzi mwingine amehoji hatua ya wao kwenda kwa Odinga ambaye aliungwa mkono na Rais Samia Suluhu Hassan katika mchakato uenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Nchi za Afrika (AU).
“Ni bora wangeenda kwa Uhuru (Kenyatta – Rais wa zamani wa Kenya), sijui wamelenga nini? Kama mtakumbuka Raila alipigiwa debe na Rais Samia kwenye kuwania uenyekiti wa kamisheni ya AU lakini hakufanikiwa.”
“Kwa vyovyote Raila hawezi kuigeuka Serikali ya Tanzania, sielewi walifuata nini labda kupata mbinu za kupambana na Serikali. Lakini kingine kuaminika kwao kutaporomoka kwa wanachama waliowachagua kwa kigezo cha misimamo,” amesema Dk Faraja Kristomus ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Dk Kristomus amesema itafika mahali zile kashfa walizompa Freeman Mbowe (mwenyekiti wa zamani wa Chadema) zitawageukia sawa na kuyala matapishi yao wenyewe.
“Sasa watarudi tena kutaka kuzungumza na yuleyule ambaye walisema amemlambisha Mbowe asali au watazungumza na waliyedai hana utu wala hajali upinzani kwa sababu anawakandamiza,” amesema Dk Kristomus.
Dk Kristomus amehoji, “endapo Chadema wakirudi katika meza ya mazungumzo watatumia mbinu ipi ileile iliyotumia na Mbowe waliodai imekwama? Au watatumia moduli ipi ya mazungumzo.”
Mchambuzi huyo amesema anachokiona kwa viongozi wa Chadema kukutana na Odinga walidhani anaweza akawapa mbinu nzuri za kuondokana na mkwamo wao uliopo hivi sasa.
“Kwa maana nyingine Chadema wanatamani kushiriki uchaguzi, wakati huohuo wanaogopa mazingira ya sasa kwamba watapoteza. Huenda walifika kule ili awape mbinu ya namna ya kushiriki uchaguzi, lakini imekuwa tofauti.
“Sidhani kama wamefurahia ushauri wa Odinga, nadhani nia yao wameenda Kenya kuonana na Raila kama mpinzani mkongwe atakayewasaidia, lakini ushauri walioupata huenda yasiwe matarajio yao,” amesema Dk Kristomus.
Mchambuzi mwingine, Ramadhan Manyeko amesema chachu ya mabadiliko ya Kenya yalitokana na Odinga, hivyo Chadema wanamuona kiongozi huyo wa upinzani wa taifa hilo, ni mwenye ushawishi atakayewasaidia kuondokana na mkwamo waliona nao.
“Wameenda kwa Raila kama mtu mwenye ushawishi katika ukanda wa Afrika Mashariki, ili atumie ushawishi wake kuishawishi Serikali ya Tanzania kuhusu mabadiliko wanayoyahitaji.
“Raila ni mkongwe kwenye siasa za mageuzi na amekuwa akikikanza na Serikali ya Kenya, lakini ndiyo chachu ya katiba mpya ya Kenya,” amesema Manyeko.
Hata hivyo, Manyeko amesema wanachokipigania Chadema hivi sasa hakitafanikiwa kwa sababu muda si rafiki badala yake waanzishe vuguvugu hilo baada ya uchaguzi wa Oktoba ili kupata ahueni kwenye chaguzi zijazo.
“Agosti kampeni zinaanza na jambo wanalolitaka Chadema ni kitaifa linahusisha wadau wengi wa vyama vya siasa. Shida iliyopo Chadema wamewaweka njia panda makada kuhusu uchaguzi na wengine hawafanyi maandalizi.”
“Rai yangu pamoja na kuwepo na ajenda ya bila mabadiliko, hakuna uchaguzi, Chadema wawaambie wanachama wao washiriki uchaguzi, huwezi kuuzuia wakati hushiriki, wafanye maandalizi maana uchaguzi ni maandalizi,” amesema Manyeko.
‘Wajiandae na uchaguzi’
Maelezo ya Manyeko yalishabihiana na Said Msonga ambaye ni mchambuzi wa siasa za kimataifa, aliyeishauri Chadema kutumia muda huu kujiandaa na uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Msonga amesema Chadema wana hoja kuhusu ajenda yao ya ‘No Reforms, No Election’, lakini imekuja kwa kuchelewa hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu uliobakisha miezi saba kufanyika.
Amefafanua ili kuwepo kwa mabadiliko ya sheria yoyote katika Taifa lazima ipitie vyombo mbalimbali likiwamo Bunge ambalo lina mamlaka ya kutunga sheria kwa kufuata michakato yote muhimu.
“Sasa hivi tunazungumza tupo Machi kuelekea Aprili, tumebakisha miezi michache kuanza mchakato wa uchaguzi hasa namna ya kupata wagombea. Sasa ili kupata mabadiliko lazima Bunge likae lijadili mabadiliko hayo, jambo ambalo kwa sasa haliwezekani,” amesema Msonga.
Msonga amesisitiza Chadema wana hoja nzuri, lakini wamechelewa, hata hivyo wakati wakiendelea kunadi ‘No Reforsm, No Election’, vyama vingine vinaendelea na maandalizi ya kuwataka makada wake kutia nia kuanzia udiwani hadi urais.
“Sasa hivi ni ngumu kwa makada wa Chadema kutangaza anagombea udiwani au ubunge atahoji anataka kwa mazingira yapi? Inawezekana Chadema ikajirudi kwa kushiriki uchaguzi, lakini muda hautakuwa rafiki kwao.
“Chadema wana hoja nzuri, lakini huenda ikawagharimu baadaye kwa sababu muda huu wa kuonana na Odinga kisiasa sio jambo baya, wanatimiza wajibu wao, lakini je, wajibu utakuwa na matokeo gani katika kile wanachokilenga?
Msonga amesema Odinga amewashauri waketi na Serikali, kitakachotokea Serikali itakubali lakini itawaambia muda sio rafiki hadi Bunge na uchaguzi umalizike.
” Moja ya mambo ya msingi ambayo Chadema wanapaswa kuyafanya kwa sasa ni kuwaandaa wanachama wao kushiriki kwa sababu wao ndio chama kikuu cha upinzani ili kufuta makosa yaliyojitokeza mwaka 2020,” amesema Msonga.
Walichokisema makada wa Chadema
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema:” Viongozi walioshiriki walipaswa kuja na ujumbe mmoja wa walichojadiliana kisha wafuasi wangejua kilichojadiliwa.”
Mrema anasema:”Tusubiri kauli ya msemaji wa chama ambayo itaunganisha ujumbe uliopelekwa na ushauri wa Odinga, kisha msimamo wa chama ni upi.
“Lakini yote kwa yote unaenda kuomba ushauri kwa bingwa wa maridhiano na ‘handshake’ Afrika wakati msimamo wako hauhusiani na maridhiano, handshake na nusu mkate? Unaweza kwenda kama unataka kupata mbinu za maridhiano, nusu mkate na handshake,” amesema Mrema.
Naye, kada mwingine wa Chadema, Edward Kinabo anasema: “Kimsingi, ushauri wa Odinga unaakisi ushauri au wito unaoweza kutolewa na wadau wengine wa demokrasia hususan ambao kwa ujumla wao wanaitwa jumuiya ya kimataifa.”
“Nilishaandika huko nyuma, kwamba wadau wengi wa demokrasia (kama si wote), wataishia kutoa wito tu wa kujaribu kuihimiza Chadema iketi na upande wa Serikali na CCM kwenye meza ya mazungumzo (mapendano).
“Hilo ni takwa na kanuni ya kawaida ya kidiplomasia. Kwa hiyo, sioni wakitusaidia kuishawishi au kuibana serikali bali naona wakiishia kutupooza tu na kutuhimiza sisi (Chadema) tuzungumze na Serikali,” amesema.
Kinabo aliyekuwa mgombea ubunge 2020 Kibaha Vijijini anasema: “Iwe tunaingia ndani ya uchaguzi au tunadai ‘reforms’ nje ya uchaguzi, hatima ya demokrasia ya nchi yetu bado itabaki mikononi mwa Watanzania wenyewe. Tuna kazi kubwa ya kufanya.”
Ameongeza kuwa, “Sasa kwa bahati mbaya sana, wenzetu wengine hawataki tuseme kwa sababu eti tunaonekana tuna vidonda vibichi na vinavyonuka vya uchaguzi.