Dodoma. Changamoto ya mifumo ya usafirishaji wa zao la parachichi ambayo inasababisha usafirishaji kuchukua siku 50, imetajwa kuathiri viwango vya ubora vinavyokubalika katika nchi zinazonunua zao hilo.
Kabla ya changamoto hiyo, usafirishaji wa zao hilo ulikuwa ukitumia, siku 25 hadi 30 kufika kwenye soko husika la nje ya Tanzania.
Hoja hiyo imeibuliwa katika mkutano wa kwanza wa wadau wa zao hilo jijini Dodoma, leo Alhamisi Aprili 4,2025.
Ofisa Mtendaji wa Taasisi inayoshughulika na kilimo cha mbogamboga na matunda ya Tanzania Horticulture Association (TAHA), Dk Jacqueline Mkindi amesema asilimia 40 ya parachichi inayozalishwa nchini inakwenda kwenye soko la Ulaya na Uingereza huku India ikienda asilimia 30.
Amesema asilimia 19 ya parachichi inauzwa katika nchi za Mashariki ya Kati na asilimia 11 inayobakia inakwenda nchi za China, Kenya na Afrika Kusini, hivyo kutokana na mauzo hayo jitihada na nguvu kubwa zinatakiwa kuwekezwa katika kulishika soko hilo.
“Eneo ambalo tunatakiwa kuliwekea mkazo ni mifumo ya usafirishaji kwa sababu hivi sasa kwenye mchakato wa kupeleka mazao duniani kuna changamoto kubwa ya kwenye bahari nyekundu (red sea crisis),”amesema.

Baadhi ya mkutano wa wadau wa parachichi nchini.
“Hiyo imefanya badala ya kutumia siku 25 hadi 30 sasa hivi tunatumia hadi siku 50, kwa hiyo ubora unaathirika na gharama za usafirishaji zimekuwa ngumu sana, hivyo miongoni mwa vitu tunavyoongelea hapa ni namna gani ya kuboresha mifumo ya usafirishaji ili kulinda ubora, upotevu wa mazao lakini kupunguza gharama,”amesema.
Amesema pia wameongea jinsi Tanzania ilivyojipanga katika kukidhi viwango vya ubora vya kitaifa, kikanda na kimataifa kwa sababu bila kukidhi viwango hivyo, parachichi ya Tanzania haiwezi kuuzika.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko, (COPRA), Irene Mlola amesema uzalishaji wa zao hilo uko katika tani 195,000 kwa mwaka kutoka tani 50,000 zilizokuwa zikizalishwa miaka mitano iliyopita.
Amesema zao hilo linahitaji uhifadhi kwa hiyo kwa kushirikiana na sekta binafsi watahakikisha wanaweka mazingira wezeshi ya miundombinu ya uhifadhi ya ubaridi.
Pia wanajikita katika ongezeko la thamani na kuwa hadi sasa wana viwanda vinne vya kuongeza thamani kwa zao hilo ambavyo vimeanza kuzalisha bidhaa mbalimbali.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Profesa Joseph Ndunguru amesema Serikali imetoa Sh2 bilioni kwa ajili ya kudhibiti viuatilifu na magonjwa katika zao hilo.

“Tunaandaa nyaraka za kufungulia masoko mapya ambazo zinaeleza zao hilo linalimwa wapi ili kama mnunuzi anapenda kufuatilia aweze kufanya hivyo,”amesema.
Amesema wameongeza mitambo ya kuchakata sampuli za wakulima ikiwemo mitambo mikubwa ambayo sampuli inawezesha kuchakata sampuli 2,000 kwa wiki na hivyo kuondoa usumbufu kwa wakulima na wafanyabiashara kupeleka nje ya nchi.