Wadau wa Kiswahili wamlilia Profesa Qorro, kuzikwa Mei 5

Dar es Salaam. Wadau wa Kiswahili wamesema kifo cha Profesa Martha Qorro ni pengo kubwa kwa kuwa licha ya eneo lake la ubobezi kuwa lugha ya Kiingereza alikuwa mstari wa mbele kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika nyanja mbalimbali.

Profesa Qorro aliyefariki dunia alfajiri ya Aprili 30, anatarajiwa kuzikwa Mei 5 katika Kijiji cha Upper Kitete kilichopo wilayani Karatu.

Msemaji wa familia, James Bwana amesema Profesa Qorro alifariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu ya ugonjwa wa saratani na ndiyo uliogharimu maisha yake.

“Maombolezo yanaendelea nyumbani familia na waombolezaji tunaendelea kukusanyika ila shughuli za mazishi zinatarajiwa kufanyika siku ya Jumatatu kijijini Upper Kitete,”amesema Bwana.

Akimzungumzia Profesa Qorro, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), Consolata Mushi amesema mwanazuoni huyo alikuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa lugha ya Kiswahili licha ya kuwa alibobea katika lugha ya Kiingereza.

“Martha alikuwa profesa wa lugha ya Kiingereza lakini siku zote alikuwa mstari wa mbele kuonesha ni kwanini anapigania watoto wajifunze kwa lugha ya Kiswahili, alifanya hivyo akiwa na uthibitisho maana alipitia madaftari ya wanafunzi akaona ni kwa namna gani lugha inawasumbua kwenye kujifunza,” amesema.

“Alikuwa mkereketwa wa lugha ya Kiswahili kwa maslahi mapana ya jamii, katika kipindi cha uenyekiti wake Bakita ndiyo tuliandaa Kamusi Kuu ya Kiswahili. Kwa kifupi mama huyu alikuwa na mawazo yenye tija kwa ukuaji wa lugha hii adhimu,” amesema Mushi.

Kwa upande wake mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St Johns, Shadidu Ndossa amemtaja kama mwanataaluma mzalendo na profesa wa Kiingereza  aliyesimama kidete kuitetea lugha ya Kiswahili.

Amesema profesa huyo alifanya tafiti nyingi katika eneo la lugha ambazo ziliibua maarifa kuhusu uhusiano kati ya lugha na elimu na katika machapisho yake alionesha Kiswahili ndiyo lugha inayoweza kutumika kwenye kufundishia na kujifunzia kwa ndiyo wanayoielewa watoto wengi.

“Ni miongoni mwa watalaamu wachache wa Tanzania ambao walikuwa na uzalendo wa hali ya juu, alikuwa profesa wa Kiingereza lakini alikuwa kinara wa kupambania lugha ya Kiswahili. Alifanya tafiti nyingi kwenye upande wa lugha na elimu na kuwa miongoni mwa watu wachache waliobobea kwenye eneo hilo.

“Alipendekeza Kiingereza ifundishwe kama lugha ya pili, hii haikuwa kitu cha kawaida kumkuta profesa wa Kiingereza akatetea lugha ya Kiswahili, aliongozwa na weledi wake na mapenzi ya umajumuhi wa Kiafrika kuwa lugha ya Kiswahili ni lugha ya Kiafrika inaweza kutoa maarifa na inaweza kuwasiadia wanafunzi wa Kitanzania kuelewa vizuri kile wanachofundishwa,”amesema Ndossa.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza), Dk Mwanahija Ali Juma amesema mwanazuoni huyo alitoa msukumo mkubwa katika lugha ya Kiswahili inatumika kwa ufasaha na ufanisi.

“Nitamkumbuka kama jemedari wa lugha, mama huyu alikuwa mfuasi wa isimu alihamasisha mambo mengi yafanyike ili kuhakikisha Kiswahili kinatumika kwa ufasaha. Kwa kifupi ana mchango mkubwa katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili, tumuenzi kwa kuyaendeleza aliyoyapigania,” amesema Dk Mwanahija.

Naye Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili Dk Caroline Asimwe amesema jumuiya ya Afrika Mashariki imempoteza mdau mashuhuri katika kipindi cha kuandaa sera ya lugha ya Kiswahili.

 “Profesa Martha alikuwa mtetezi wa lugha ya Kiswahili. Alijikita zaidi katika masuala ya upangaji lugha na sera ya lugha Lugha katika elimu hasa kwa upande wa lugha ya kufundishia katika elimu nchini Tanzania. Kwangu binafsi, alikuwa mlezi na mshauri. Alikuwa mwenyekiti wa kamati ya mtihani wangu wa kutetea tasnifu ya uzamivu pale Tataki (Taasisi ya Taaluma za Kiswahili), UDSM (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,”amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *