Wadau Geita waingilia kati upungufu wa vyoo shuleni

Geita. Wanafunzi 1,156 wa Shule ya Msingi Ikulwa iliyopo katika Manispaa ya Geita wanatumia matundu manane ya vyoo, sawa na tundu moja kutumiwa na wanafunzi 163, jambo ambalo ni kinyume na mwongozo wa Sera ya Elimu unaoelekeza tundu moja kutumiwa na wasichana 20 au wavulana 25.

Uhaba wa matundu ya vyoo husababisha foleni ndefu za wanafunzi wanaosubiri huduma ya choo, hivyo kutumia muda mwingi nje ya darasa, badala ya kujifunza, pia, wanachangia mazingira yasiyo salama kiafya.

Kutokana na upungufu huo, Shirika lisilo la Kiserikali la Plan International, kupitia mradi wake wa Wawezeshe Wasichana Kuendelea na Masomo (Kagis), unaofadhiliwa na Serikali ya Canada, limejenga choo chenye matundu 18 ili kupunguza changamoto hiyo.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Daniel Jonathan akizungumza jana Februari 20, 2025 wakati wa makabidhiano ya choo hicho, amesema shule hiyo ilikuwa na upungufu wa matundu 53 ambapo sasa itakuwa na upungufu wa matundu 27 baada ya kukamilika ujenzi huo.

“Wamejenga matundu 18 ya vyoo, 10 ni ya wasichana na matundu manane ni ya wavulana, ujenzi wa matundu haya utapunguza uwiano wa tundu moja kwa wanafunzi 163 kwa wasichana hadi kufikia uwiano wa 1: 46; na wavulana kutoka tundu 1: 125 hadi 1: 42.

“Hii itapunguza changamoto ya wanafunzi kutumia muda mwingi wakati wa kwenda kujisaidia,” amesema Jonathan.

Mbali na ujenzi wa vyoo, pia Kagis huwajengea uwezo wanafunzi na walimu katika stadi za maisha na klabu za masomo pamoja na ufundishaji unaozingatia usawa wa kijinsia.

Msimamizi wa mradi wa Kagis, Nicodemas Gachu amesema kupitia mradi huo, miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa vyoo na madarasa hutekelezwa, lengo likiwa ni kumwezesha mtoto wa kike kuendelea na masomo.

Amesema kupitia mradi huo, mahudhurio shuleni yameongezeka baada ya mradi kugawa baiskeli kwa wasichana ambapo amesema mahudhurio yamepanda kutoka asilimia 82 mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 94 mwaka 2023.

Mkurugenzi mkazi wa Plan International nchini Tanzania, Jane Isambuche amesema katika Mkoa wa Geita, miundombinu ya vyoo imejengwa kwenye shule tisa za mkoa huo ambapo mbali na miundombinu hiyo, Plan hutekeleza miradi ya elimu, afya, kilimo pamoja na ulinzi na usalama wa mtoto.

Amesema katika sekta ya elimu, watoto wa kike wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uhaba wa miundombinu unaozingatia usawa wa kijinsia, utoro na upungufu wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia.

Ametaja shule nyingine zilizonufaika na mradi wa vyoo na maji kuwa ni pamoja na shule ya Iponya, Makarai, Nyakato, Lutozo Mchongamani, Katoro, Kilimani na Igwata pamoja na Isongamile.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema mradi wa Kagis utapunguza upungufu wa matundu ya vyoo kutoka uwiano wa 1:113 hadi kufikia 1:75 kwa shule ya Lutozo, Mchongani kutoka 1: 250 hadi 1:120 na Kilimani kutoka 1:124 hadi kufikia 1:54.

Amesema ujenzi huo utaongeza mahudhurio hasa kwa wasichana baada ya vyoo vilivyojengwa kuwa na chumba maalumu kwa ajili ya wasichana kujihifadhi.

Choo cha matundu 10 kilichojengwa kwa ajili ya wasichana katika shule ya Msingi Ikulwa Manispaa ya Geita.

Akisoma taarifa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala Msaidizi, Herman Matemu amewataka maofisa elimu na viongozi wengine katika ngazi za wilaya na shule kuhakikisha kunakuwa na mfumo wa maji ili vyoo, hivyo vya kisasa viweze kutumika ipasavyo.

Takwimu za kitaifa

Ripoti ya Tanzania Water and Sanitation Network (Tawasanet) inaonyesha kuwa asilimia 32 ya shule nchini hazina maji safi na asilimia 13 hazina vyoo kabisa.

Kwa mujibu wa taarifa ya elimu msingi ya mwaka 2020, kuna upungufu wa matundu ya vyoo 181,000 sawa na asilimia 62 ya mahitaji, hivyo kusababisha uwiano wa tundu moja kutumiwa na wanafunzi 62 kinyume na mwongozo unaopendekeza uwiano wa 1:25 kwa wavulana na 1: 20 kwa wasichana.