Wadakwa wakiwa na meno ya tembo, bangi

Mbeya. Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa mbalimbali akiwemo, Marko Kweya (51), Mkazi wa Kijiji cha Miyombweni, Wilaya ya Mbarali mkoani humo kwa tuhuma za kukutwa na mano manne ya tembo.

Pia, jeshi hilo linamshikilia Hassan Hassan (50), Mkazi wa Mkoa wa Tanga baada ya kumkamata akiwa na dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilogramu 25.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya (RPC), Benjamin Kuzaga akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi, Mei 17, 2025 amesema Kweya alikamatwa Mei 15, 2025 katika kitongoji cha Azimio, Kata ya Miyombweni, Tarafa ya Rujewa, akiwa na  meno manne ya tembo yenye uzito wa kilogramu 18.

Kuzaga amesema mtuhumiwa alibainika akiwa ameyaficha kwenye mifuko miwili ya sandarusi. Amesema hatua hiyo imetoana na ushirikiano walioufanya baina yao na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) na Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (Tawa).

Katika tukio jingine, Kamanda Kuzaga amesema Mei 8, 2025 walimkamata Hassan katika kizuizi cha Polisi eneo la mpakani Wilaya ya Mbarali barabara Kuu ya Tanzania na nchi jirani ya Zambia (Tanzam).

Amesema mtuhumiwa alikamatwa akisafirisha dawa hizo aina ya bangi kwenye basi la kampuni ya Abood lililokuwa likitoka Mbeya kwenda jijini Dar es Salaam huku akiwa ameficha kwenye sanduku.

Kamanda Kuzaga ameonya watu wanaojihusisha na uharifu na kwamba Jeshi la Polisi halijalala litawashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kamanda huyo amesema wanawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kuhujumu miundombinu ya maji ya kimkakati yenye thamani ya zaidi ya Sh28 milioni.

Watuhumiwa hao walikamatwa kati ya Aprili 22 na Mei 15, 2025 katika oparesheni maalumu ya Polisi ya kukabiliana na uharifu.

Mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya Larsen & To u bro Limited ulikuwa ukitekelezwa katika Mji wa Lujewa Wilaya ya Mbarali ambao ungetoa huduma ya maji katika Mkoa wa Mbeya na Njombe.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni , Edwin  Liweuli (26) Chesco Muheze (44) mlinzi wa mradi wa huo kutoka kampuni ya Jimson Security Ltd ya Mkoa wa Iringa, Hamza Madete (29), wote wakazi wa Igawa Wilaya ya Mbarali na mwingine Victor Timbulo (25), mkazi wa Ifakara Mkoa wa Morogoro.

“Watuhumiwa walikamatwa kati ya Aprili 22 mpaka Mei 15, 2025 katika misako mbalimbali ya Jeshi la Polisi ambao baada ya kuiba vifaa na mabomba 50 walianza kusafirisha kwa kutumia pikipiki aina ya boxer ambayo haina namba za usajili,” amesema.

Kamanda Kuzaga amesema vifaa walivyo kamatwanavyo vilikuwa vinatumika kutekeleza mradi wa kimkakati ambao ungeondoa adha ya maji kwa wananchi wa Mkoa wa Mbeya na Njombe.

“Huo ni mradi wa kimkakati ambao Serikali imewekeza zaidi ya Sh28 milioni, watuhumiwa baada ya kukamatwa na kupekuliwa walibainika wakiwa na vifaa na mabomba 50,” amesema.

Aidha amesema watuhumiwa baada ya kuhojiwa walikiri kutenda kosa hilo na kwamba watafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi zaidi wa tukio hilo.

Mkazi wa Igawa, Rehema John ameomba Polisi kufanya kaguzi za mara kwenye mabasi ya masafa marefu ili kudhibiti usafirishaji wa dawa za kulevya.

“Doria pia zifanywe kwenye vyombo vya usafiri wa bodaboda kwani wapo ambao vinara wa kusafirisha bangi na milungi,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *