Wadakwa wakidaiwa kusafirisha gramu 3,263 za dhahabu kwa njia ya magendo

Geita. Jeshi la Polisi mkoani Geita linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kukutwa wakisafirisha kwa njia ya magendo, gramu 3,263.72 za dhahabu yenye thamani ya zaidi ya Sh749 milioni.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Adam Maro amesema watuhumiwa hao walikamatwa Machi 24, 2025 saa tano usiku katika Mtaa wa Kapera wilayani Bukombe.

Amewataja waliokamatwa kuwa ni Yohana Idama (34) mkazi wa Nyamhongolo Wilaya ya Ilemela Mwanza, Moshi Manzili (26) mkazi wa Bariadi Mkoa wa Simiyu na Hamidu Salum (25) mkazi wa Nyasubi wilayani Kahama.

Akielezea kukamatwa kwa watu hao, Maro amesema Jeshi la Polisi lilipata taarifa za siri kutoka kwa wasamaria wema na kuweka mtego uliofanikisha kukamatwa kwao.

Amesema baada ya upekuzi kwenye gari walilokuwa wanatumia, walikutwa na dhahabu hiyo imefichwa ndani.

Maro amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kufanywa na polisi kwa kushirikiana na mamlaka nyingine ili kubaini na kuwakamata watakaobainika kujihusisha na uhalifu huo, kisha kuwafikisha mahakamani.

Wakati huohuo, mtoto mmoja amefariki dunia na wengine watatu wote wa familia moja, wamejeruhiwa na radi katika Kijiji cha Kakoyoyo wilayani Bukombe kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha.

Tukio hilo lililotokea Machi 23, 2025 saa 12 jioni lilipelekea kifo cha Ibrahim Masumbuko (9), mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya Msingi Kakoyoyo.

Kaimu kamanda amesema siku ya tukio mvua kubwa iliyoambatana na upepo na radi ilinyesha na watoto hao walikuwa kwenye shamba la mpunga wakiwinda ndege, walipoona mvua walikimbia kurudi nyumbani na wakiwa njiani ndipo walipigwa na radi ikaua mmoja na kujeruhi wengine.

Amesema baada ya uchunguzi, mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa familia huku watoto wengine wakipatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Bulega na hali zao zinaendelea vizuri.

Hili ni tukio la tatu kutokea la watu kupigwa na radi wilayani Bukombe tangu mwaka 2025 kuanze, baada ya Januari 27, 2025 wanafunzi saba wa shule ya Sekondari Businda kupoteza maisha huku wengine 82 wakijeruhiwa wakiwa darasani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *