Wachumi wafunguka faida, hasara ongezeko laini za simu

Dar es salaam. Wachumi wameeleza manufaa na changamoto ya ongezeko la laini za simu nchini.

Kauli za wachumi hao zinakuja kukiwa na ongezeko la usajili wa laini za simu kulingana na  ripoti iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Desemba  mwaka 2024, inaonyesha ongezeko la laini za simu  kutoka 51,292,702 mwaka 2020  hadi kufikia 86,847,460  mwaka 2024 ikiwa ni  ukuaji wa asilimia 69.3.

Profesa Dickson Pastory, mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Biashara, amesema ongezeko la laini za simu  ni ishara ya kuimarika kwa mapato ya Serikali kupitia kodi.

“Mtu akiwa na laini ya simu ni dhahiri kuwa ataitumia na kwa matumizi hayo, anachangia kodi katika mfuko wa Serikali,” amesema Profesa Pastory.

Hata hivyo, Profesa Pastory amebainisha changamoto inayotokana na baadhi ya laini kusajiliwa lakini kutotumika kwa muda mrefu, akisema hali hiyo  husababisha ongezeko la idadi ya laini zilizosajiliwa, lakini nyingi kati ya hizo si hai.

“Changamoto kubwa ni kwamba baadhi ya laini zinakuwa hazitumiki kwa muda mrefu licha ya kuwa zimesajiliwa, hivyo kuonesha ongezeko la usajili lakini sio matumizi halisi,” amefafanua Profesa Pastory.

Mchumi mwingine, Profesa Anna Sikira amebainisha faida ya kila mwananchi kumiliki laini ya simu, akisisitiza ni nguzo kuu ya mawasiliano katika karne ya sasa.

“Simu ni msingi wa mawasiliano katika karne hii, na taarifa ni nguvu. Hivyo ni dhahiri kadiri laini za simu zinavyoongezeka, ndivyo watu wanavyowasiliana zaidi na kupitia mawasiliano hayo maendeleo yanapatikana,” amesema  Profesa Sikira.

Hata hivyo, Profesa Anna ametahadharisha kuhusu changamoto zinazowakumba watumiaji wa laini hizo, hususan vijana kutokana na athari za mitandao ya kijamii.

“Licha ya mawasiliano kuwa muhimu, tunaona namna mitandao ya kijamii inavyoharibu tabia za vijana, wakijaribu kuiga maisha yasiyo ya kweli yanayoonyeshwa mitandaoni,” amesema.

Aidha, Thobias Swai mchambuzi wa masuala ya kiuchumi naye ameeleza sababu za ongezeko la laini za simu akitaja kuongezeka kwa idadi ya watu na upatikanaji wa huduma za mtandao katika maeneo ambayo awali hazikuwepo.

“Kila mwaka, zaidi ya watu milioni mbili huanza kutumia laini za simu na maeneo mapya yanaendelea kufikiwa na huduma za mtandao,” amesema Swai.

Pia, amebainisha umuhimu wa matumizi ya laini za simu katika uchumi, hususan katika sekta ya biashara.

“Umiliki wa laini za simu umekuwa msaada mkubwa kwa watu katika kukuza biashara zao. Dunia ya sasa inategemea sana mtandao, hivyo ongezeko la laini za simu linachochea ukuaji wa biashara kwa kiasi kikubwa” amefafanua.

Balozi Morwa, mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki jijini Mbeya amesema  pamoja na ongezeko la laini za simu bado kuna athari za kodi na tozo kwenye maendeleo ya mtu mmoja mmoja.

“Iwapo kodi na tozo za matumizi ya laini hizi za simu zitapunguzwa na kudhibitiwa, tofauti na ilivyo sasa, hatua hiyo itavutia watumiaji wengi zaidi na kusaidia kukuza maendeleo ya wananchi,” amesema Balozi Morwa.

Amesema ongezeko la laini za simu ni zaidi ya takwimu,  linaakisi maendeleo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii.