Wachumi: Fanyeni haya kukabili hasara ya mashirika ya umma

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwasilisha ripoti ya ukaguzi kwa Rais Samia Suluhu Hassan ikibainisha hasara kwenye mashirika ya umma, wachumi wamependekeza Serikali iingia ubia na sekta binafsi ili mashirika yake yaendeshwe kibiashara.

Jana, Machi 27, 2025 CAG, Charles Kichere na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Crispin Chalamila waliwasilisha ripoti zao za mwaka 2023/24 kwa Rais Samia, wakionyesha mafanikio na changamoto walizobaini.

Katika taarifa yake, CAG Kichere alibainisha hasara ya mabilioni ya shilingi ambayo mashirika ya umma yanapata kwa sababu mbalimbali. Hasara hizo zimekuwa zikijirudia mwaka hadi mwaka, jambo ambalo limeelezwa linahitaji suluhisho la haraka na la kudumu.

Mashirika yaliyotajwa kupata hasa ni Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Shirika la Reli Tanzania (TRC), Shirika la Posta Tanzania (TPC) na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Kichere alibainisha mwaka wa fedha 2023/24, ATCL imepata hasara ya Sh91.8 bilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 62 kutoka hasara ya Sh56.6 bilioni mwaka uliopita.

Kwa upande wa TTCL, alisema lilipata hasara ya Sh27.7 bilioni mwaka wa fedha wa 2023/2024 ikiwa ni ongezeko kutoka Sh4.32 bilioni ya hasara kwa mwaka uliopita.

CAG Kichere alisema mwaka wa fedha 2023/2024, TRC ilipata hasara ya Sh224 bilioni, ikilinganishwa na Sh102 bilioni za mwaka uliopita.

Ongezeko la hasara hizo, limewaibua wadau wa sekta ya uchumi na biashara wakishauri hatua mbalimbali za kuchukua.

Ubia na sekta binafsi

Katika ushauri wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umaskini nchini (Repoa), Dk Donald Mmari amesema CAG alieleza baadhi ya mashirika yamebainika kuwa na usimamizi mbovu, hivyo ni muhimu menejimenti za mashirika hayo ziangaliwe upya kwa kuleta utamaduni mpya wa usimamizi wa mashirika, hasa ya kibiashara kutoka sekta binafsi.

“Lazima uunganishe masilahi ya menejimenti na wafanyakazi pamoja na wamiliki wa kampuni, sasa kama wamiliki hawasukumwi na faida, kwa maana ya Serikali. Asili ya Serikali ni kutoa huduma, asili ya sekta binafsi ni kupata faida, sasa unafanyaje kuunganisha vitu hivi?

“Hili ni jambo muhimu kuliangalia, ama kuangalia usimamizi wa haya mashirika au kuingia ubia na sekta binafsi,” ameeleza Dk Mmari alipozungumza na Mwananchi kuhusu ripoti ya CAG itakayowasilishwa bungeni ndani ya siku saba za kazi.

Akizungumzia ATCL ambako CAG amebainisha hasara kuongezeka, amesema mashirika ya ndege ni magumu kuyaendesha na kuwa miaka minne iliyopita alisoma ripoti moja ambayo ilionyesha shirika la ndege pekee lililokuwa likipata faida Afrika ni Ethiopian Airline.

“Usafirishaji wa anga ni biashara ambayo ni complex (ngumu), kwa kweli inahitaji kuendeshwa kibiashara, kusimamiwa vizuri na hilo linaweza kufanywa na sekta binafsi,” amesema.

Amesema sekta binafsi inaweza hilo kama menejimenti itachaguliwa kwa makini kulingana na sifa na kupewa uhuru wa kujiendesha.

Dk Mmari amesema ukiendesha shirika kibiashara, lazima uzingatie kuongeza mapato na kupunguza matumizi, hapo ndipo unaweza kupata faida.

“Kama mifumo ya umma inafanya haya mashirika yasiweze kuzalisha faida, basi tuangalie namna ya kuyabinafsisha ama kuingia ubia na sekta binafsi ambayo inaweza kuleta ufanisi kwenye uendeshaji wake au tuangalie uongozi wake uwe thabiti na usioingiliwa katika kufanya uamuzi wa kibiashara,” amesema.

Mtazamo huo hauko mbali na wa Dk Onesmo Kyauke, mchambuzi wa masuala ya uwekezaji ambaye amesema mashirika mengi ya umma duniani hayafanyi vizuri, yanaendeshwa kwa hasara kwa sababu wafanyakazi wake hawaweki jitihada kwa kuwa wana uhakika wa kulipwa mishahara na Serikali.

Amesema namna rahisi ni kubinafsisha mashirika hayo lakini Serikali ibaki na asilimia chache katika umiliki, ili kuiwezesha kupata faida.

“Benki kama NBC au NMB, sasa zinaendeshwa kwa faida nzuri, lakini zilivyokuwa serikalini zilikuwa zikijiendesha kwa hasara. Imefika mahali mashirika haya ya umma yabinafsishwe. Hata Air Tanzania, Serikali ibaki labda na asilimia 30 zingine asilimia 70 ichukue sekta binafsi, utaona namna watakavyofanya vizuri,” amesema.

Amesema: “Kama ni shirika tu la uzalishaji, haliathiri usalama wa Taifa, kupambana na haya matatizo yote ya hasara ni kubinafsisha na siyo kubinafsisha lote, Serikali inaweza kubaki na asilimia 40 na sekta binafsi ikachukua zinazobaki.”

Amesema ubinafsishaji au ubia huo unaweza kufanyika pia kwa ATCL kwa kushirikiana na kampuni kubwa kama Emirates, hiyo itasaidia kuleta mapinduzi na Serikali itapata faida.

Hasara ziangaliwe vizuri

Mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude amesema hasara zilizobainishwa na CAG zinatakiwa kuangaliwa kwa utulivu kwa sababu kuna vitu viwili vinaangaliwa ambavyo ni gharama za uendeshaji na gharama za kihesabu.

Ametoa mfano wa ATCL akisema inaweza kuonekana inatengeneza hasara kwa maana ya gharama za kihesabu ambazo wanaangalia matumizi dhidi ya mapato yaliyokusanywa.

Hata hivyo, amesema mashirika ya umma yana majukumu mengine tofauti na kampuni za kibiashara.

Amesema ATCL ni shirika la umma ambalo pamoja na majukumu mengine, linafanya kazi ya kufungua soko la usafiri wa anga Tanzania.

“ATCL inapokuwa inatekeleza wajibu huo, inaweza ikawa haitengenezi faida ile ya kwenye vitabu, ambayo ndiyo inatazamwa na CAG, lakini inaweza kuwa imetengeneza faida kwa maana ya impact (matokeo).

“Kwa mfano, Air Tanzania inaweza kuanzisha njia kutoka Dar es Salaam kwenda Nachingwea au Mpanda, wanapoanza kutengeneza hiyo ruti, patakuwa na gharama kwa sababu wateja wanaokwenda njia hiyo wanaweza wasiwe wengi kwa zile siku za mwanzo… hizi ni gharama ambazo kwa kampuni ya kibiashara haiwezi kwenda, lakini ATCL kwa jukumu lake la kufungua soko, lazima itakwenda,” amesema.

Amesema matokeo ya kazi hiyo yanaanza kuonekana kwa kampuni nyingine za kibiashara kuanza kupeleka ndege zao huko anakokwenda ACTL, maana yake asingekwenda wengine pia wasingekwenda.

“Kwa hiyo, upande wa impact kwa bahati mbaya ripoti huwa hazionyeshi, kwamba mandate (mamlaka) za haya mashirika siyo tu kutengeneza faida, bali kuna wajibu mwingine kama huo nilioutaja,” amesema.

Amesisitiza ni muhimu kufanya tathmini ya kina ya wajibu wa mashirika ya umma kama yametimiza wajibu wake mpana, badala ya kuangalia kigezo kimoja cha kutengeneza faida.

“Wao wanaweza wasitengeneze faida, kama ambavyo kampuni hiyohiyo angepewa mtu ambaye ni mtaalamu wa biashara. Ndiyo maana baadhi ya watu wanapendekeza ile miradi inayopaswa kuendeshwa kibiashara, basi wapewe wafanyabiashara,” amesema.

Mhadhiri wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi amesema mashirika mengi yanaonekana kupata hasara kwa sababu hali imebadilika, lakini yenyewe yameshindwa kubadilika kuendana na wakati ili kupunguza au kuepusha hasara zinazojitokeza.

“Kwa mfano, Shirika la Posta Tanzania, yale majukumu iliyokuwa inafanya yamebadilika, mambo yanafanyika kwa simu za mkononi, mambo ya barua yamepungua sana. Kwa hiyo nao wajipange kuhakikisha wanaongeza ufanisi. Wajifunge kubadilika kuendana na wakati,” amesema.

Profesa Moshi amesema mikataba mingi inayosainiwa haina uwazi wa kutosha, wananchi wanapata taarifa juujuu.

“Ule mchakato uwe na uwazi ili tuepukane na rushwa kwenye mikataba hiyo,” amesema.

Amesisitiza pia usimamizi wa mashirika ya umma kupitia bodi zao uimarishwe na wafuatilie maelekezo wanayotoa ili kuhakikisha kwamba mashirika yanaendeshwa kwa ufanisi na kuleta tija.

“Bodi zinafanye kazi zao kama inavyostahili na pia wakaguzi wa ndani na nje watimize wajibu wao kikamilifu ili kuondoa hasara hizi,” amesema.

Pia alizungumzia kuhusu kuongezeka kwa hati safi akisema ni jambo zuri kwa sababu linaonyesha mashirika yanazingatia mambo yanayotakiwa kufanyika.

Deni la Taifa

Kuhusu deni la Taifa, CAG Kichere alisema deni la Serikali limeongezeka kufikia Sh97.35 trilioni Juni 30, 2024 kutoka Sh82.25 trilioni kwa mwaka 2022/23.

Kwa mujibu wa CAG, deni hilo bado ni himilivu kutokana na viashiria vikuu alivyovitaja ikiwemo thamani halisi ya deni na pato la Taifa.

Akizungumzia deni hilo, Dk Kyauke amesema nchi nyingi zina madeni na Tanzania kuwa na deni si tatizo kama fedha zimekwenda kwenye miradi ya maendeleo kama vile reli ya kisasa (SGR) na Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) ambayo italeta matokeo makubwa.

“Miradi hii italeta mapinduzi makubwa ya kiuchumi na hilo deni litalipika, kwa hiyo sioni kama deni ni shida, hata nchi kama Marekani zina madeni makubwa, nchi nyingi zina madeni lakini kwa kuwa miradi iliyoanzishwa inaonekana, mkopo siyo tatizo,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *