Arusha. Katika hatua ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, wachoma nyama mkoani Arusha wameahidiwa kupewa majiko yanayotumia nishati safi kwa ajili ya kazi yao.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa Machi 7, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda wakati akikagua maandalizi ya nyama choma kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambayo kitaifa yatafanyika jijini hapa kesho Machi 8.
Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Makonda amesema miongoni mwa sababu ya athari ya mabadiliko ya tabianchi ni ukataji holela wa miti kwa ajili ya shughuli za kibinadamu ikiwamo uchomaji mkaa, hivyo ofisi yake itagawa majiko ya nishati safi ili kukabiliana na hilo.
“Tunawashukuru wenzetu wa Wizara ya Nishati kwa kutupatia majiko na nishati safi katika shughuli yetu hii kama mnavyoona hata moshi wake hauumizi.
“Nilikuwa nawauliza wachoma nyama wetu kama kuna utofauti wowote, wamenihakikishia kuwa hii imesaidia sana, na ofisi ya mkuu wa mkoa tutahakikisha baada ya tukio hili tunagawa majiko yanayotumia nishati safi kwa wachoma nyama wote Arusha,” amesema Makonda.
Akizungumzia suala hilo, miongoni mwa wachoma nyama hao, Robert David amesema wakipewa majiko hayo yatakuwa nafuu kwao na kwa afya zao.
“Wakitupatia kweli majiko hayo itakuwa poa sana, maana shughuli kama ya leo isingekuwa mkaa huu na majiko haya, tungetumia muda nrefu,”amesema David.
Magdalena Mushi ambaye naye ni mchoma nyama Arusha amesema, majiko ya nishati safi yatasaidia kuongeza mauzo kwa sababu yanatumia muda mfupi kuivisha.
“Tukipewa majiko hayo, tutakuwa tunachoma nyama nyingi kwa muda mfupi, itaongeza hata mapato yetu,” amesema Magdalena.
Wakati wachoma nyama wakizungumzia athari kiafya, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha watu 33,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia.
Kuhusu nishati safi, Rais Samia Suluhu Hassan katika kikao cha Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki (EAC) kilichofanyika Arusha Novemba 29, 2025 alisema miongoni mwa mikakati ya Tanzania ni kuhakikisha vijiji vyote vinakuwa na umeme.

Mchoma nyama mkoani Arusha, akitumia jiko la nishati safi. Picha na Ally Mlanzi
Pia, Rais Samia alisema miongoni mwa kikwazo cha kupatikana kwa nishati safi ni gharama kubwa, huku akisema Tanzania inatumia karibia asilimia nne ya Pato lake (GDP) katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Malengo ya nishati safi
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akizungumza katika Mkutano wa Jukwaa la Majadiliano kuhusu Masuala ya Nishati kwa Bara la Afrika kwa ngazi ya Mawaziri Oktoba 17, 2024 alisema hadi mwaka 2030 watu milioni 300 Afrika watakuwa wanatumia nishati safi, huku Tanzania ikiwa ni kinara katika kuhamasisha Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia.