
Dar es Salaam. Shirikisho la Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (Femata), limeiomba Serikali mashine za kuchimba ambazo kwa sasa ziko 10.
Akitoa maombi hayo leo Jumanne, Novemba 19, 2024, kwenye mkutano wa sita wa kimataifa wa Madini na Uwekezaji Tanzania mwaka 2024, Makamu wa Rais wa Femata, Victor Tesha, amesema wanaomba mashine hizo ziwepo kila wilaya nchini humo.
“Kwa sasa zipo 10 na zinakuja tano hadi Desemba zitakuwa 15, ombi letu ziwe nyingi ili kuchochea uchimbaji wa madini kusaidia kuchimba na kupata taarifa za kutosha kwa wachimbaji wetu,” amesema.
Pia, ameomba leseni maalumu za wachimbaji wadogo,”tunatambua Serikali kupitia Wizara ya Madini ifute leseni 2000 kwa sababu hiyo tunaomba leseni hizo zipewe wachimbaji wadogo hapa Tanzania.”
Amesema wachimbaji wadogo wanachangia asilimia 40 ya pato la Taifa licha ya teknolojia hafifu walizonazo huku lengo lao likiwa kufika asilimia 60 hadi 70.
“Tanzania sehemu iliyofanyiwa utafiti ni asilimia 16 pekee na wachimbaji wadogo tunachangia asilimia 40; je ikifika utafiti asilimia 50 naamini tutachangia asilimia zaidi ya hizo,” amesema Tesha.
Ombi lingine wameomba ruzuku moja kwa moja kwa vyama vya wachimbaji wadogo ili kuongeza tija ya uchimbaji wa madini.
“Tija itaongezeka ya uchimbaji madini. Pia, tunaunga mkono uzalishaji thamani wa madini,” amesema.
Aidha amepongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuwa na wachimbaji wadogo bega kwa bega katika changamoto ikiwamo ya kuvamiwa.
Akijibu maombi hayo Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema mashine za kuchimba Serikali itaendelea kutenga bajeti ili kuwa nazo za kutosha kama walivyotaka.
Waziri Mkuu amesema Serikali itaanza na ngazi ya kikanda kisha itanunua za kutosha kufikia lengo la kuwa nazo kila wilaya.
“Serikali imefanya mapitio ya ardhi yenye madini; na katika suala la leseni kubwa za uchimbaji madini zilizokaa muda mrefu bila kufanya kazi. Tumezichukua ardhi hizo na tunazo, malengo ni kutoa leseni mpya ndogo ndogo kwa wachimbaji wetu wadogo waweze kumiliki na kuwekeza,” amebainisha.
Majaliwa amewaahidi wachimbaji wadogo kukaa tayari kupata maeneo ya uchimbaji waweze kumiliki na washirikiane na Serikali.
Mkutano huo wa siku tatu ulioanza leo Novemba 19, umewaleta pamoja washiriki mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Endelea kufuatilia Mwananchi