
Geita. Zaidi ya watu 10,000 wa Kata ya Buswola wilayani Nyang’wale Mkoa wa Geita wameathirika kiuchumi baada ya shughuli za uchimbaji mdogo wa madini katika Mgodi wa Ifugandi kusimamishwa kwa miezi saba kutokana na mazingira hatarishi.
Hata hivyo, wachimbaji wadogo wa eneo hilo wamedai kuwa, mgodi huo umesimamishwa sio kwa sababu ya mazingira hatarishi, bali mgogoro wa leseni uliopo kati yao na Kampuni ya Sailats Investment Co. ltd.
Wananchi walioathirika ni pamoja na wanachama 175 wa Chama cha Ushirika wa Wachimbaji Wadogo Ifugandi, wafanyakazi na vibarua zaidi ya 2,000 mgodini hapo, wafanyabiashara na mama lishe.
Imeelezwa kuwa, mgodi huo ulisimamishwa Machi mwaka huu baada ya ofisi ya madini mkoa wa kimadini Mbogwe kufanya ukaguzi na kubaini mazingira hayako salama na baada ya maboresho, Oktoba 22 mwaka huu ukaruhusiwa kuanza kazi lakini Oktoba 30 kibali hicho kikaondolewa na shughuli kusimama.
Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Mbogwe, Jeremiah Hango amethibitisha kufanya ukaguzi katika mgodi huo na kubaini mazingira hatarishi.
Anasema walimtaka mwenye leseni kukubaliana na wachimbaji ili waandae mpango kazi wa kufanya shughuli zao kwa usalama.
Hango anasema pendekezo hilo lilitekelezwa na ofisi yake ikatoa kibali cha kuanza kazi lakini pande hizo mbili zikashindwa kukubaliana, ndipo mmiliki huyo alikwenda wizarani na sasa wameitwa jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Novemba 18, mwaka huu ili kusuluhishwa.
Mwakilishi wa Kampuni ya Sailats Investment Co. Limited yenye leseni ya mgodi huo, Edward Kitambala anasema Serikali ndiyo ilisimamisha uchimbaji baada ya kukagua na kubaini mzingira ni hatarishi.
Kitambala ambaye ni Meneja wa Mgodi wa Ifugandi anasema kazi yake ni kusimamia hali ya usalama na uzalishaji.
Anasema hawezi kuruhusu shughuli ziendelee kwenye mazingira ambayo siyo salama kwani shida ikitokea anayebeba lawama ni mmiliki wa leseni.
“Kwenye maduara kuna sehemu ambazo timba zimekufa na ni asilimia 20 tu kati ya 100 ya sehemu ambazo zimefungwa timba, kwingine kote kuko wazi. Kinachohofiwa ni kwamba, pale kuna milipuko inafanyika kwa hiyo inaweza ikajitokeza shida ardhi ikafukia watu,” anasema meneja huyo.
Katibu wa Chama cha Ushirika wa Wachimbaji Wadogo Ifugandi, Emmanuel Ronjamila anasema walianza uchimbaji mdogo eneo hilo mwaka 2012 hadi 2019 bila leseni, ndipo wakaunda vikundi vidogo kuanzisha chama cha ushirika ili kupata leseni.
Anasema kikundi kiliundwa mwaka 2021 na kufuatilia leseni lakini hawakuipata.
Ronjamila anasema wakati wanaendelea kufanya kazi, eneo hilo lilikuwa na leseni ya utafiti inayomilikiwa na Kampuni ya Sailats Investment Limited kwa ajili ya utafiti tangu mwaka 1994 ndipo mgogoro ukaibuka.
Anasema Mei 17 mwaka huu walikutanishwa jijini Dodoma ili kusuluhishwa na ikaamuliwa leseni ipewe kampuni kwa kuwa ndiyo iliyotangulia.
“Machi mosi mwaka huu, tulipokea barua ya kufanya ukaguzi kwenye leseni ambazo tumeingia nazo mikataba, ofisi ya madini ilileta ripoti ya ukaguzi na ikaonekana leseni moja ina hitilafu lakini sisi tunaamini taarifa hiyo haikuwa na uhalisia wa eneo hili,” anasema Ronjamila.
Katibu huyo anasema ili kuruhusiwa kuendelea na kazi zao katika eneo hilo, walitakiwa kuandaa mpango kazi wa uchimbaji salama na kuweka zaidi ya Sh800 milioni kwenye akaunti yao ya benki, licha ya kutimiza masharti hayo hakuna kilichoendelea jambo linalowapa hofu huenda baadhi ya viongozi wanahusika kukwamisha.
Mwenyekiti wa chama hicho, Zabron Mesanga anasema moja ya makubaliano na mmiliki wa leseni kwenye kikao cha usuluhishi cha Mei 17 mwaka huu jijini Dodoma ni kuonyesha mipaka ya maeneo ya leseni zake tatu ili eneo la wazi linalobaki limilikiwe na wachimbaji hao wadogo.
Anasema baada ya kutimiza masharti ya mpango kazi wa kufanya uchimbaji salama katika eneo hilo waliweka Sh812 milioni kwenye akaunti ya ushirika, ndipo danadana za kibali kuruhusiwa kufanya kazi zilipoanza.
“Baada ya kuruhusiwa tuliandaa vitendea kazi na kuvipandisha mlimani lakini kabla hatujaanza kazi tukaletewa barua ya kutuzuia na wakatuma barua kututaka twende Dodoma Novemba 17, mwaka huu katika kikao kingine cha usuluhishi,” anasema Mesanga.
“Tulipoingia mkataba wa kisheria kuturuhusu kufanya kazi hapa kama miongoni mwa wawekezaji tulitengeneza barabara ya mlimani na uwekezeji mwingine kwenye huu mlima wa zaidi ya Sh500 milioni,” anasema Mesanga.
Wadaiwa mamilioni
Kabla ya kupewa zuio hilo, chama hicho kilikuwa kimekodisha mitambo mitatu zikiwamo katapila 320 na dozer kutoka Kampuni ya G5 Logist kwa Sh150 milioni lakini mitambo hiyo baada ya kufikishwa eneo la tukio, imeshindwa kufanya kazi siku zaidi ya nane sasa.
Anasema kampuni hiyo huwatoza Sh1.2 milioni hadi Sh1.5 milioni kwa kila mtambo kila siku.
Mkurugenzi wa Kampuni ya G5 Logist, Moses Msabila anasema kabla ya kuingia makubaliano hayo na kuleta mitambo mlimani hapo walikagua eneo, kuzungumza na msanifu wa mradi huo na kuonyeshwa kibali cha kuendelea na kazi, lakini anashangazwa mambo kubadilika baada ya vifaa vyake kufika hapo.
“Hawa wachimbaji walipokuja kuniomba mitambo hii walinikuta nafanya kazi na nikawaambia siwezi kuegesha mitambo bila kulipwa, ninavyoongea hapa wananilipa kila siku kwa mashine tatu.
“Niliwataka waniambie nitoe mitambo lakini nikishaitoa lazima niwatoze gharama ambazo mitambo yangu imesimama hapa. Mashine moja iko hapa lakini mbili ziko njiani nilikuwa nimeshazipakia kutoka Mwanza kuja hapa,” anasema Msabila.
Mjumbe wa ushirika huo, Mwoleka Desdery anasema wachimbaji wamechanga fedha nyingi kwa kukopa na wengine kuuza nyumba ili kukidhi masharti ya kibali cha kuchimba eneo hilo, hivyo wanaiomba Serikali iwasaidie waanze kazi na kulipa madeni hayo.
“Sisi tunahitaji tupate hatima ya mgogoro huu, mwenye leseni aamrishwe na mamlaka zinazohusika, turuhusiwe na mitambo iliyoletwa hapa mlimani ianze kazi. Tunaamini Rais ambaye anasikiliza watu wake atusaidie wananchi tuliopo mahali hapa tunaumia,” anasema Desdery.
Mfanyabiashara wa chakula, Mariam Charles anasema biashara zimedorora kwa kuwa walitegemea kuuza chakula kwa wafanyakazi na vibarua wa mgodi huo.
“Hali ya uchumi na mitaji tuliyowekeza imeshuka baada ya kusimamishwa huu mlima (mgodi) mambo yote yamesimama. Kwa niaba ya kina mama Rais Samia Suluhu Hassan atusikie tunahangaika, tunaomba mlima uachiwe ili tupate kipato tusomeshe watoto na maisha yaendelee,” anasema Mariam.
Novesta Solomon, mamalishe anasema mwanzo alikuwa anapika wastani wa kilo nane mpaka 20 za wali kwa siku lakini tangu mlima huo ufungwe anauza kilo mbili na wakati mwingine zinabaki.
“Tunashindwa tufanye nini, hali imekuwa ngumu hatuingizi kipato kama ilivyokuwa mwanzo, tunatakiwa kulipa kodi ya jengo, tuna madeni kwenye maduka, tunapokwenda kuchukua nafaka, hii inatufanya tunashindwa kuendesha biashara zetu, niko kwenye mtihani,” anasema Novesta.