Wachezaji waibebe au waiangushe Simba Afrika

Wawakilishi wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, Simba imejua mpinzani wake katika hatua ya robo fainali ya mashindano hayo ambayo ni Al Masry ya Misri.

Simba itaanzia hatua hiyo ya mtoano kwa kucheza ugenini huko Misri kati ya Aprili Mosi hadi 2 na timu zitarudiana wiki moja baadaye hapa nchini katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Hii itakuwa ni mara ya pili kwa Simba na Al Masry kukutana katika Kombe la Shirikisho Afrika ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni 2018 katika raundi ya kwanza ya mashindano hayo ambapo Simba ilitolewa kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya mechi mbili baina yake na Al Masry kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Ni muda wa miaka sita umepita sasa tangu Simba ilipotolewa na Al Masry ambayo ni mingi sana na kuna mabadiliko makubwa ambayo timu zote mbili zimepitia na ziko tofauti kulinganisha na zilipokutana mwaka 2018.

Kwa mfano Simba ina mabadiliko makubwa katika kikosi chake kulinganisha na kile cha mwaka 2018 lakini ina mabadiliko katika benchi la ufundi, uongozi, bajeti na hata uzoefu wa klabu kiujumla na mashindano ya kimataifa.

Kikosi cha sasa cha Simba kina wachezaji watano tu ambao walikuwemo kwenye kikosi chao kilichotolewa na Al Masry miaka sita iliyopita ambao ni makipa Ally Salim na Aishi Manula, mabeki  Mohamed Hussein na Shomari Kapombe pamoja na kiungo Mzamiru Yassin.

Na kati ya hao sita, ni wawili tu ambao wana uhakika na nafasi ya kuanza katika kikosi cha Simba ambao ni Hussein na Kapombe lakini wengine wanne wameshindwa kufua dafu mbele ya nyota ambao wameingia kikosini katika miaka ya hivi karibuni.

Wakati ule Simba ilikuwa inashiriki ikiwa imetoka kupita kipindi cha miaka karibia mitano bila kushiriki mashindano ya kimataifa hivyo haikuwa na uzoefu wa mechi hizo kama klabu katika masuala ya kiufundi na kiutawala.

Lakini leo hii tunaizungumzia Simba ambayo katika kipindi cha awamu sita tofauti zilizopita za mashondano ya klabu Afrika, imetinga hatua ya robo fainali mara tano, mafanikio ambayo yameifanya sasa hivi kuwa katika nafasi ya sita katika chati ya ubora wa klabu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Katika kipindi hicho imekutana na timu nyingi bora na ngumu zinazofanana na Al Masry na nyingine zina daraja la juu na vikosi vizuri zaidi kulinganisha na timu hiyo ya Misri.

Msimu huu bajeti ya Simba ni zaidi ya Shilingi 10 bilioni lakini mwaka 2018 ilikuwa ni chini ya Sh2 bilioni hivyo haikuwa inamudu baadhi ya gharama za ushiriki wa mashindano hayo kulinganisha na hivi sasa.

Kwa maana hiyo dhidi ya Al Masry hivi sasa, Simba haiingii kinyonge kama ilivyokuwa kipindi kile na yenyewe ndio kwenye makaratasi inapewa nafasi kubwa ya kutinga nusu fainali huku Al Masry nafasi ikiwa ndogo kwa upande wao.

Hata hivyo ili matarajio ya wengi yatimie kwa Simba kusonga mbele, kazi kubwa inapaswa kufanywa na wawakilishi hao wa Tanzania kuhakikisha kwamba inaitupa nje ya mashindano timu hiyo ambayo kwa sasa katika Ligi Kuu ya Misri inashika nafasi ya tano.

Viongozi wanapaswa kuhakikisha wanaandaa mapema utaratibu wa timu kusafiri kwenda Misri, huduma ya malazi pindi timu itakapokuwepo ugenini pamoja na huduma nyingine stahiki zinazohitajika pindi timu inapokuwa na mchezo.

Benchi la ufundi hapana shaka limeshaanza kuifuatilia Al Masry na kisha kufanyia kazi ubora na udhaifu wao ili litengeneze mpango bora wa kukabiliana nao katika mechi hizo mbili zilizo mbele yao.

Lakini juhudi za viongozi na benchi la ufundi hazitokuwa na maana wala faida yoyote ikiwa wachezaji watashindwa kucheza kwa bidii kubwa katika michezo dhidi ya Al Masry.

Wachezaji wa Simba wanapaswa kuhakikisha wanajilinda na kushambulia kww pamoja kama timu na kuepuka kufanya makosa ambayo mwisho wa siku yanaweza kuwapa faida wapinzani wao.

Licha ya kuongoza kundi lake katika hatua iliyopita huku ikiwa na namba nzuri za mabao ya kufunga, Simba ilionyesha udhaifu katika safu yake ya ulinzi ambapo katika mechi sita za hatua ya makundi iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne.

Idadi kubwa ya mabao hayo ilitokana na makosa binafsi ya wachezaji wa Simba lakini bahati nzuri yalifunikwa na maba ambayo ilifunga yaliyochangia itinge robo fainali.

Hatua iliyo mbele na hata za juu zaidi ya hapo zinahitaji umakini na utulivu wa hali ya juu na wanaotakiwa kutekeleza ni wachezaji na sio watu wengine.