
SIMBA inahesabu saa kabla ya kushuka uwanjani kesho Jumapili kukabiliana na Stellenbosch ya Sauzi katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku mfadhili wa zamani, Azim Dewji, akiwaongezea mzuka mastaa kwa kutangaza dau kwa kila bao na asisti.
Simba itaikabili Stellenbosch kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar kuanzia saa 10:00 jioni mechi ikiamuliwa na mwamuzi Jean Jacque Ndala wa DR Congo kabla ya wiki ijayo kwenda ugenini kwa mchezo wa marudiano na mshindi wa jumla atafuzu moja kwa moja kufuzu kucheza fainali ya michuano hiyo.
Azim alitoa ahadi hiyo jana akisema kwamba lengo ni kutaka kuona ndoto ya Simba kwenda fainali inatimia kwa kuongeza dau la fedha kwa kila bao na asisti kutoka Sh2.5 milioni iliyokuwapo katika mechi za robo fainali dhidi ya Al Masry ya Misri na sasa atatoa Sh6 milioni kwa mechi hizo za nusu. Katika mchezo dhidi ya Al Masry Dewji aliwalipa fedha Ellie Mpanzu na Steven Mukwala waliofunga mabao mawili yaliyofanya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2 na kuwapa pia kiasi kama hicho mabeki Shomari Kapombe na nahodha Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ walioasisti, kila mmoja akiondoka na kitita cha Sh2.5. Simba ilivuka kwenda nusu kwa penalti 4-1 baada ya kipa Moussa Camara kuokoa mbili na Kapombe kufunga mkwaju wa mwisho kuizima Al Masry iliyoshinda nyumbani 2-0.
Kwa mchezo wa kesho, Azim amewaongezea dau mastaa wa timu hiyo akiwaambia kila asisti itaondoka na Sh6 milioni kama ambazo atapewa pia mfungaji wa bao husika ikiwa na maana kila bao litakuwa na thamani ya Sh12 milioni kutegemea na jinsi litakavyofungwa tofauti na Sh5 milioni za mechi ya robo.
“Wachezaji walifurahia kile ambacho tulifanya katika mchezo uliopita wanaona ilitengeneza umoja ndani ya timu na nimeongea nao wameniambia wanataka niongeze na watafunga mabao mengi. Nimewaambia mchezo huu nitanunua kila bao kwa Sh12 milioni,” alisema Azim.
“Katika hizo Sh12 milioni, mgawanyo ni uleule atakayetoa pasi atapata milioni sita na atakayefunga pia atapata milioni sita. Lengo hapa tunataka kuona wote wanashiriki kutengeneza ushindi. Tunataka mabao zaidi ili mchezo wa marudiano uwe rahisi kwetu tukacheze fainali.”
“Wachezaji wanasema wanataka kutengeneza ushindi mkubwa. Kwenye mechi hii sisi viongozi nafasi yetu ni kuwapa motisha ya namna hii lakini pia mashabiki wenzangu wengine kazi yetu twende tukaufurishe Uwanja wa Amaan ili tukawape nguvu vijana wetu kukamilisha malengo yao.
“Nina imani na timu kuanzia benchi la ufundi linalofanya kazi nzuri chini ya Fadlu Davids… Simba inashinda kwa ubora uwanjani na inasonga mbele. Haya ndio mambo yanayonifanya niupongeze uongozi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji ‘MO’ na bodi yake nzima.”
Ahadi hiyo ya Azim aliyeiongoza Simba 1993 na kuifikisha fainali ya Kombe la CAF na kupoteza nyumbani katika mechi ya marudiano kwa mabao 2-0 mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast, inaifanya kila bao sasa litatengeneza jumla ya Sh22 milioni endapo ahadi ya bao la Mama inayotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan haitaongezeka kutoka Sh10 milioni.