Licha ya kubadilishwa kwa mfumo wa usajili wa wachezaji kwa ajili ya Ligi tofauti zilizopo Tanzania, lakini bado kuna madudu yamekuwa yakijitokeza na kuzua sintofahamu kwa wadau.
Kumekuwa na kesi karibu kila msimu kupitia madirisha ya usajili ya Ligi Kuu Bara na hata Ligi nyingine iwe kwa lile dirisha kubwa au dogo na kusababisha usumbufu mkubwa kwa mamlaka ya soka.
Hata hivyo, upo mkakati madhubuti umepangwa kufanyika msimu ujao unaoweza kuwa dawa ya uhuni unaoendelea katika sajili kwa klabu mbalimbali nchini.
Mmoja wa vigogo wa Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), amefichua kuwa katika kuhakikisha sajili zinafanyika bila kuwepo kwa uhuni na udanganyifu wanakuja na kitu ambacho kinaweza kuwabana wachezaji na viongozi janjajanja.
Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji wa (TFF), Said Soud ndiye aliyefunguka hayo na kuanika uhuni unaofanywa na baadhi ya wachezaji na viongozi wa klabu za soka nchini kipindi cha usajili ambapo baadae huleta usumbufu kwa mamlaka kutatua kesi hizo hususani usajili ya kidigitali.
Soud amefichua hayo alipofanya mahojiano maalumu na Mwananchi na kufunguka njia nzuri y kukomesha madudu yote yanayojitokeza katika usajili wa wachezaji wa Ligi Kuu na klabu nyingine, lakini akisimulia uzoefu ana changamoto alizokutana nazo katika kamati anayoisimamia ikiwamo kupitia kesi zaidi ya 40 kwa siku kipindi cha kupitia sajili za klabu mbalimbali nchini. Endelea naye….!

KIGEZO USAJILI PASIPOTI
Imekuwa ikifahamika kuwa usajili wa wachezaji wa kigeni kigezo chao ni kanuni ya ubora pamoja na kuwa sehemu ya kikosi cha timu yake ya taifa sasa mambo yanaenda kubadilika hasa kwa wachezaji wa ndani kama anavyothibitisha Soud.
“Tupo kwenye mpango mkakati wa kuhakikisha mchezaji yeyote awe wa ndani au wa kigeni kusajiliwa kwa kuwa na hati ya usafiri (Passport),” anasema Soud na kuongeza;
“Miaka ya hivi karibuni wachezaji wote wawe wa ndani na nje wanatakiwa kuwa na hati ya kusafiria ili aweze kusajiliwa nafikiri kwa nyota wa kigeni itakuwa rahisi kwao kwani hawawezi kuja nchini bila pasipoti.
Anasema kwa upande wa wachezaji wa kigeni wao pia watatakiwa kupata vibali zaidi ya hati ya kusafiria, watatakiea kuwa na kibari cha makazi na hati ya kufanya kazi ili wawese kukidhi mahitaji ya kusajiliwa.

USAJILI KIDIGITALI WANUKIA
Suala la usajili linachukuliwa rahisi kutokana na timu kutangaza wamefanikiwa kumalizana na mchezaji fulani kumbe kwenye ishu za kuingiza kwenye mfumo kuna changamoto kubwa kama anavyosisitiza Mwenyekiti wa Sheria na hadhi za wachezaji TFF.
“Maisha sasa yanaendeshwa na utandawazi sana hasa mitandaoni tuna mpango wa kutunga kanuni ambayo itatuondolea changamoto hizo kwa kuhakikisha usajili unafanyika kwa mifumo ya onlne mchezaji, klabu na kamati kushuhudia usajili unapofanyika,” anasema na kuongeza;
“Uamuzi huo ni kutokana na changamoto zilizopo sasa kwani timu zinaweza kuingiza kalatasi ambalo halina ujumbe wowote kwa lengo la kuwahi dirisha kufungwa na sisi tukiangalia tunakutana na karatasi halina kitu chochote na makalatasi yaliyo mezaji yamekamilika kwa kila kitu.”
Anasema mfumo wao unasoma karatasi bila kujia lina maandishi au la hivyo timu zimekuwa zikifanya ujanja kwa lengo la kuwahi dedline na kuingiza karatasi ambalo halijakamisha usajili.
Soud anasema kutokana na changamoto hizo wanaunda mkakati maakum na tayari wameshaanza kujadili kwenye vikao vyao ili kuhakilisha wanaunda mkakati maalumu wa kupitisha kanuni ya kufanya usajili kidigitali.
KUIDHINISHA USAJILI
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji (TFF) imekuwa ikishughulika na madai ya wachezaji zaidi kama inavyofahamika lakini Soud amefunguka kazi nyingine ambazo wamekuwa wakifanya.
“Kuna kitu wengi hawafahamu mbali na kuhagaika na changamoto za usajili wa wachezaji sisi pia ndio tunaidhinisha sajili za wachezaji wa kigeni endapo wameshindwa kukidhi mahitaji tunazuia,” anasema na kuongeza;
“Sisi ndio tunaidhinisha wachezaji hasa wa kigeni kwa kutizama wamefuata kanuni, wamefuata idadi inayotakiwa lakini wakizidi kwa mujibu wa kanuni tunawazuia.”
Soud anasema usajili wa wachezaji wa kigeni idadi ni wachezaji 12 kama kuna timu imemtoa mchezaji kwa mkopo na wanasajili mwingine basi alietolewa kwa mkopo anatakiwa kutolewa kwenye mfumo na wao hawamtambui kama mchezaji wao.
“Mfano Yanga walikiwa na mchezaji wao Lazarous Kambole walikuwa wanataka kuachana naye ili wamsajili Tuisila Kisinda tulizuia kwamba wamtoe kwa mkopo ili aingie huyo hadi hapo walipotoa taarifa ya kumuuza Uganda ndio tuliporuhusu usajili mpya.”

UTAPELI WA MIKATABA
Kumekuwa na kesi nyingi kwa baadhi ya wachezaji wakilia na usajili kwa kuweka wazi kuwa wamekuwa wakiongezewa miaka tofauti na makubaliano na hata mikataba waliyosaini hilo kweli lipo kama anavyothibitisha Suddy.
“Ni kweli changamoto hiyo ipo lakini inasababishwa na wachezaji wenyewe kwasababu wamekuwa wakiona fedha wanasahau vitu vya msingi kama kubeba copy ya mkataba,” anasema na kuongeza;
“Pia kuma wachezaji wanaruhusu waajili wao wawasajilie mikaba ili kuwahi dirisha kabla ya kufungwa na wao wanatumiwa hiyo mikataba lakini inakuwa haina siani tofauti na mkataba ulio ingizwa kwenye mfumo wa usajili.”
Anasema mchezaji anaposaini hachukui mkataba lakini kwenye mkataba ulio kwenye mfumo unaweza ukawa tofauti hivyo mchezaji kama akiulizwa mkataba halali uko wapi asipokuwa nao basi shida itakuwa juu yake kwani usahihi ni mkataba uliopo.
Soud anasema kumalizana kwenye karatasi na kuingizea kwenye mfumo ni vitu viwili tofauti hivyo wachezaji wanatakiwa kuwa makini hasa kuchukua copy za mikataba yao ili kuweza kuwasaidia shida kama hizo zinapotokea.

KESI ZA MADAI CHANGAMOTO
Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji imekuwa ikiteseka na kesi mbalimbali lakini Mwenyekiti wake amedai keshi za madai ndio zimekuwa zikiwapa changamoto kwenye ufuatiliaki kama anavyofunguka.
“Unajua wachezaji wanasajiliwa kwenye timu na wanapotaka kuondoka kwenye hizo timu wanataka kuondoka rahisi bila kuangalia ni namna gani timu iliyompa mkataba inatakiwa kunufaika,”
“Mfano suala la Feisal Salum ‘Fei Toto’ sakata lake halikuea la halali kutaka kuvunja mkataba akiwa na tayari ya kuwa na uelekeo wa kwenda timu nyingine haikupaswa kuwa hivyo atakama mkataba unamruhusu kuondoka anatakiwa kujali klabu iliyomkuza ili nayo inufaike kwa lolote,” anasema na kuongeza;
“Wachezaji wanatakiwa kuelewa utofauti wa kuvunja mkataba ambayo ni suala ambalo linampa uhuru mchezaji lakini anatakiwa kujua kuwa anaruhusiwa kufanya hivyo kama atataka kusimama kwa muda ata wa miaka mitatu au zaidi bila kucheza mpira na sio kutaka kuhamia timu nyingine.”
Soud anasema mchezaji akitaka kuondoka timu moja kwenda nyingine ni lazima timu iliyomuinua inufaike kama ambavyo mataifa mengine yanafanya.
“Lakini mazingira ambayo yanaweza kumuondoa mchezaji bila kulipa chochote ni kuto kulipwa mishahara kwa miezi kuanzia miwili ambayo pia itapewa kipaumbele kama mchezaji husika atakuwa alikuwa anatengeneza mazingira kuanzia mwezi wa kwanza ajaingiziwa fedha, akionyesha mazingira ya unyanyaswaji akiwa na ushahidi sio kwa kuzungumza kama Fei Toto kwamba anakula ugari na sukari hakuna mtu anaweza akaamini.”

SAKATA LA LAWI
“Mkataba wake ndio unakipengele cha kuwataka kukaa pamoja shida yoyote inapotokea ndio maana kila wakikaa wanawataka wakae mezani wazungumze,” anasema na kuongeza;
“Simba walikiuka makubaliano ya kimkataba na ndio maana walishindwa kumpata Lawi lakini bado timu inamuhitaji wanaingia na kutoka hasa wanaposikia mchezaji huyo akihusishwa na timu nyingine.”
Anasema mkataba ulieleza kuwa mchezaji anatakiwa kupewa fedha yote bila mabaki lakini muda sahihi ulipofika Simba hawakufanya hivyo waliweka kiasi kidogo ambacho ata nusu haikufuka, pia mkataba ulisema endapo atapata timu yoyote nje ya Tanzania atapewa 20% za fedha zote.
Soud anasema klabu zina malalamiko mengi, lakini Lawi yupo sahihi na ndio maana hadi sasa anacheza Coastal Union timu ambayo ni sahihi yeye kucheza kutokana na mkataba wake.

KUVUNJA MKATABA
Suala la uvunjwaji wa mikataba baina na timu na mchezaji limekuwa likifanyika ki holela sana na kusababisha migogolo kama anavyofunguka Suddy kuwa timu nyingi zinakosea na kujikuta zinaingia kwenye changamoto.
“Unapomvunjia mkataba mchezaji unatakiwa kukaa naye kwaajili ya mazungumzo mfano umebakiza mwaka mmoja au miwili kwa hali yetu ilivyo hatutaweza kumudu kwa miaka hiyo miwili ambayo imebaki sisi
“Wewe unapovunja kabla ya siku moja sio kwamba unahaki ata mchezaji pia anahaki hivyo anaweza akaja kudai hivyo sisi tunatizama mazingira yalivyokuwa na sheria kufuata mkondo kwa mchezaji kulipwa,” anasema Soud.
Soud anasema wachezaji wengi wanavunjiwa mikaba bila ya makubaliano na ndio maana kesi za namna hiyo zimekuwa nyingi na vilabu vimekuwa vikifungiwa kusajili kutokana na kukutana na rungu la kutakiwa kuwalipa wachezaji ambao wamewavunjia mikataba bila ya kuwalipa.

KESI 40 KWA SIKU
Kamati ya Sheria na hadhi za wachezaji zimekuwa zikikutana mara kwa mara hasa kipindi cha kufungwa kwa dirisha la usajili ili kupitia mashtaka mbalimbali kama anavyofunguka Suddy kuwa wamekuwa wakipitia keshi nyingi zinazowaka pamoja kwa muda mrefu.
“Sina kumbukumbu kwa mwaka tunaweza kupokea ngapi kwa mwaka lakini kwa siku tunaweza kusikiliza hadi 40 ambazo kati ya hizo kuna baadhi wanaomba kesi ihairishwe kutokana na kukosa muda,” anasema na kuongeza;
“Tunakaa kuanzia asubuhi hadi jioni tunachoka lakini ndio kazi yetu licha ya baadhi ya washitaki wanaweza wakapata au wakaamua kuachana na kazi kutokana na kufuatilia kwa muda na kuamua kukata tamaa.”
NYOTA SIMBA ADAI BONASI
Wakati wachezaji wengi wamekuwa wakikimbilia kushtaki madai yao kwenye kamati ya sheria na hadhi za wachezaji wakiamini hakuna kitakachoshindikana imebainika kuwa nyaraka za ushahidi ni muhimu zaidi kama anavyofunguka Soud.
“Kuna mchezaji simkumbuki ni wa muda kidogo amewahi kucheza Simba na Yanga alikuja kudai madai yake ambayo alitakiwa kulipwa akiwa Simba na ilikuwa ni suala la bonasi nakiri kuwa kuna kesi unaona kabisa mchezaji anahaki na anatakiwa kulipwa lakini hakuna maandishi,” anasema na kuongeza;
“Hilo sakata Simba walilikubali lakini walisema halipo katika maandishi yalikuwa ni makubaliano ya mdomo tu sio haki kwamba lazima apate hivyo na sisi hatuwezi kuwa na nguvu ya kumpigania.”
Anasema huyo mchezaji alitakiwa kupata Sh. 5 milion alikuwa na haki lakini hakuna maandishi ambayo yanaweza kumpa haki ya kupata na wahusika ambao ni Simba walisema hawana mapatano naye.
KAMATI HAIINGILIWI
Wakati Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPLB) ikiingiliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa upande wa Kamati ya sheria na hadhi za wachezaji ni tofauti kama anavyothibitisha Soud.
“Watu hawaamini lakini sio rahisi kwetu sisi kuingiliwa lakini viongozi wamekuwa na kawaida ya kuuliza kufahamu kesi fulali imefikia wapi sio kutuamulia nini cha kufanya,” anasema na kuongeza;
“Wajumbe wanatoka sehemu tofauti tofauti na kuna muda tunabishana kila mmoja anaona anauelewa zaidi ya mwingine lakini suala la kuingiliwa sio kweli na halipo.”
SAJILI TIMU MBILI TOFAUTI
Imekuwa ikitokea mara kadhaa kwa baadhi ya wachezaji kuibuka kwenye sajili ya timu mbili togauti Soud katolea ufafanuzi juu ya suala hilo.
“Sakata la wachezaji kusajiliwa timu mbuli tofauti ni namna ambayo ujanja unatumika kwani mfumo tunaoutumia unafanya shida hizo zitokee kwani inawezekana kwa wachezaji kuchezesha majina yao,” anasema na kuongeza;
“Mfano mimi ni Said Soud naweza nikatumia kwa usahihi jina la kwanza na la pili naondoa herufi moja au mbili jina linaingia kwenye mfumo hii ndio changamoto inayotokea pale suala la mchezaji mmoja kusaini timu mbili tofauti.”
ELIMU KWA WACHEZAJI
Ni wachezaji wachache ambao wanacheza ligi kuu wana elimu za kutosha wakisomea mambo mbalimbali lakini kuna wengine walichagua kucheza mpira na kukacha shule suala ambalo Suddy amelitaja kama changamoto kwenye soka la Tanzania.
“Ni muhimu kwa wachezaji kupewa elimu ili waweze kuelewa haki zao, wachezaji wengi wa kitanzania elimu zao ni ndogo hata kwenye kiwango cha mpira kuna utofauti, mfano ukimchukua mchezaji wa darasa la saba na kidato cha nne kuna utofauti mkubwa,” anasema na kuongeza;
“Kutoa elimu kwa wachezaji wao sio kujiangusha hao ni wachezaji wao wasiwanyime haki ya kujua haki zao, suala la wachezaji kukosa elimu linaturudisha nyuma sana lakini wachezaji wakipata elimu ya kutambua haki zao changamoto nyongi zitapungua.”