Kilwa. Basi la timu ya Dodoma Jiji limepata ajali huku ikidaiwa wachezaji na watumishi wa timu hiyo ambao wanakadiriwa kufika 37 kujeruhiwa baada ya basi lao kutumbukia mtoni.
Ajali hiyo imetokea leo Februari 10, 2025 katika eneo la kati ya Nangurunkuru na Somanga ambapo gari hilo lilidumbukia mtoni.
Katibu Mkuu wa timu hiyo, Fortunatus Johnson amethibitisha tukio hilo akieleza kuwa wachezaji wote wamejeruhiwa kwa kukatwa na vioo vya gari.

Amesema baada ya mchezo wa jana dhidi ya Namungo walianza safari leo alfajiri kuwahi maandalizi ya mechi ijayo dhidi ya Simba, Februari 15 na kwamba tayari majeruhi wote wamepelekwa hospitali kwa uchunguzi wa awali na haraka.
“Jumla walikuwamo 37, wachezaji 25, ‘staff’ 15 na dereva mmoja, tayari wamepelekwa hospitali ya Nangurunkuru kwa uchunguzi wa awali, hatujajua ni nani kaumia lakini ajali ni kubwa kwa kuwa walitumbukia mtoni na lile eneo ni polini”

“Tatizo ni mawasiliano kwa sababu simu zao wote zimezama. Naendelea kuwasiliana na mmoja wapo lakini kuna msaidizi wangu amekuja nyuma yao kwa kuwa mimi nilitangulia hapa Dar es Salaam,” amesema Kiongozi huyo.
Amesema baada ya ajali hiyo waliwasiliana na serikali ya mkoa wa Lindi ambapo walitoa msaada wa ambulance tatu na kuwachukua majeruhi hao.