Wachezaji African Sports walala kwenye gari

WAKATI African Sports (Wana Kimanumanu) ya jijini Tanga ikipambana kubaki katika Ligi ya Championship, ukata unazidi kuiandama timu hiyo kiasi cha wachezaji wake kulazimika kulala ndani ya gari badala ya hotelini au kwenye nyumba za wageni.

Timu hiyo kongwe nchini katika mechi 25 za Championship ambazo imecheza imekusanya pointi 14  ambazo zimetokana na ushindi wa mechi nne, sare mbili na kuchapika michezo 18 ikifunga mabao 21 na kufungwa 46.

Matokeo hayo yanaiweka katika nafasi ya 14 ambayo kikanuni ni ya kucheza hatua ya mtoano (playoff) ili kukwepa kushuka daraja wakati huu ambapo utofauti wa pointi zake na timu iliyopo nafasi ya 15, Transit Camp ni alama tatu.

Transit Camp ambayo kama ligi ikimalizika leo inaungana na Biashara United iliyopo nafasi ya 16 kushuka daraja moja kwa moja hadi First League, ina pointi 11 baada ya kucheza mechi 24 ikiwa na faida ya mchezo mmoja mkononi.

Kocha wa African Sports, Kessy Abdallah ameliambia Mwanaspoti kwamba sababu ya kuendelea kufanya vibaya katika Ligi ya Championship ni uchovu ambao wamekuwa wakikumbana nao hasa wanaposafiri kwenda kucheza mechi za mikoani kutokana na wachezaji wake kulala ndani ya gari kwa kukosa fedha za kuwalipia hoteli au hata nyumba za kulala wageni.

“Uwezo wa kiuchumi sio mzuri. Kwa mantiki hiyo hatuwezi kufikia sehemu nzuri ya kukaa na wachezaji wakawa vyema, hivyo tunakaa kwenye gari na inatufanya kuwa na uchovu muda wote,” alisema Kessy.

“Watu wa Tanga sapoti ni ndogo sana na mpira ujue ni gharama kubwa. Mtu anakupa milioni mbili halafu ukimfuata tena anaanza kuzungumza maneno mengi.”

Kocha huyo aliwaomba wadau wa soka mkoani humo kuhakikisha wanaiunga mkono timu hiyo katika mechi tano za ligi zilizosalia ili ifanye vizuri na kujitengenezea mazingira mazuri ya kubaki kwenye nafasi ya kucheza mechi za mtoano.

“Kwa uchache kila mchezaji kwa siku inatakiwa atumie Sh10,000 mpaka 15000 zidisha mara 24 pamoja na viongozi sita ambao tupo, hivyo watu wa Tanga wanatakiwa watoe pesa kuisaidia hii timu,” alisisitiza.

Akizungumzia kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Mbuni FC ambacho walikipata katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Kessy alisema kilitokana na uchovu na  pia wachezaji wake watano kubaki Tanga kutokana na changamoto za kifamilia.

Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa African Sports, Ramadhan Sadick alisema ni kweli wanakabiliwa na ukata, ingawa wanaendelea kupambana kuhakikisha wanaondokana na jambo hilo.

“Suala la kulala njiani ni kweli kwa sababu tunasafiri usiku na tunafika siku husika ya mech. Hii ilitutokea mchezo wetu na Biashara United kule Mara, lakini tuna kikao Jumatano ya Aprili 2 hii na wanachana wetu ili kujadiliana namna ya kuondokana na changamoto iliyopo,” alisema.

Ramadhan alisema moja ya kipaumbele chao cha kwanza kwa sasa ni kuweka mikakati mizuri ya kuhakikisha timu hiyo inasalia tena katika Ligi ya Championship kwa msimu ujao, huku akiwaomba wadau na mashabiki kuendelea kuwapa sapoti kwa ajili ya michezo mitano iliyosalia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *