Wacheza kamari walivyopiga mamilioni uchaguzi wa Papa

Dar es Salaam. Uchaguzi wa Papa Leo XIV (Robert Francis Prevost) haukuwa tu tukio la kidini lililofuatiliwa kwa makini na mamilioni ya waumini wa Kanisa Katoliki duniani, bali pia ulibadilika kuwa fursa ya kiuchumi kwa wacheza kamari waliobashiri matokeo yake.

Kabla ya Leo XIV, kutangazwa kurithi mikoba ya Papa Francis aliyefariki Aprili 21, 2025, katika makazi yake ya Mtakatifu Marta, Vatican, majina 12 ya makardinali waliokuwa wanapigiwa chapuo kuchaguliwa katika wadhifa huo ni Pietro Parolin (Italia), Luis Tagle (Ufilipino), Fridolin Ambongo Besungu (DRC), Matteo Zuppi (Italia) na Péter Erdő (Hungary).

Wengine ni, Anders Arborelius (Sweden), Pierbattista Pizzaballa (Italia), Juan José Omella (Hispania), Reinhard Marx (Ujerumani), Robert Sarah (Guinea) na Marc Ouellet wa Canada

Katika hali ya kushangaza, Kardinali Prevost, ambaye hakutajwa sana katika mizunguko ya midahalo ya wachambuzi wa Vatican, ndiye aliyeibuka mshindi katika uchaguzi huo uliogubikwa na usiri mkubwa, na inaelezwa kuwa kuna wacheza kamari waliotumia tukio hilo la kihistoria kama fursa ya kupiga pesa.

Tovuti ya Jarida la Forbes imeripoti kuwa wacheza kamari mtandaoni walitumia zaidi ya Dola za Marekani milioni 40 (zaidi ya Sh107.9 bilioni) kubashiri juu ya atakayekuwa Papa mpya na mshindi mmoja alipata dola 52,000 (Sh140 milioni) kwa ubashiri wa hatari kuwa Prevost (Leo) atakuwa papa.

Watu wengi walijaribu kubashiri ni nani angechaguliwa kuwa Papa mpya na hata kuweka pesa zao katika ubashiri huo. Wachache walitegemea kuwa angekuwa Mmarekani huyo kutoka Chicago, nchini Marekani.

Wacheza kamari waliwekeza kiasi hicho cha zaidi ya Sh107 bilioni katika mkutano wa hivi karibuni wa uchaguzi wa Papa, kupitia majukwaa mawili tu ya masoko ya utabiri: zaidi ya dola milioni 30 (zaidi ya Sh80 bilioni), kwenye Jukwaa la Polymarket, kulingana na tovuti yao, na zaidi ya dola milioni 10.6 (zaidi ya Sh28 bilioni) kwenye Kalshi, kwa mujibu wa msemaji wa kampuni hiyo.

Kabla ya mkutano huo, Papa mpya Leo XIV ambaye hapo awali alikuwa Kardinali Robert Prevost alikuwa na uwezekano wa chini ya asilimia 1 ya kuchaguliwa, kulingana na tovuti ya Kalshi.

Msemaji wa Jukwaa la Kamari la Kalshi, aliieleza Forbes kuwa kati ya biashara (mikeka) zaidi ya 33,000 iliyowekwa kwenye jukwaa la kamari la Kalshi kuhusu mkutano huo, ni biashara 416 tu zenye jumla ya karibu dola 450,000 (zaidi ya Sh121 milioni) ndizo zilizowekwa kwa Prevost.

Forbes pia imeripoti kuwa mkeka uliowekwa na kushinda kiwango cha juu zaidi kwenye jukwaa hilo ulikuwa na thamani ya dola 52,641 (zaidi ya Sh140 milioni) kutokana na kuweka dau la dola 526 (Sh1.1 milioni), ameongeza msemaji. Hata hivyo, jukwaa hilo halikuanika jina la mchezaji kamari huyo aliyeshinda kitita hicho.

Mkutano huo wa uchaguzi wa Papa ulikuwa “kichocheo kikubwa, sawa na tukio kubwa la michezo,” amesema msemaji wa Kalshi.

Hata hivyo, dola milioni 10.6 (zaidi ya Sh26 bilioni) zilizowekezwa kwenye jukwaa hilo ni kidogo ukilinganisha na kiasi kilichotumika katika uchaguzi wa hivi karibuni wa rais wa Marekani: dola milioni 132 (zaidi ya Sh356 bilioni), kwa mujibu wa kampuni hiyo ilivyohojiwa na jukwaa la MarketWatch Novemba, 2024.

Masoko ya utabiri hufanya kazi kama masoko ya hatima (futures), ambapo watumiaji hununua na kuuza kandarasi zinazolipa kulingana na matokeo ya tukio la baadaye.

Masoko haya yaliibua mijadala na uchunguzi wakati wa uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka jana, kutokana na hofu kuwa yanaweza kutumika kwa ajili ya upotoshaji au ushawishi usiofaa, pamoja na masuala ya udhibiti wa kisheria.

Wachezaji wakubwa wa masoko hayo wanaweza kuyatumia kushawishi ushiriki wa wapigakura siku ya uchaguzi, alisema Cantrell Dumas, ambaye ni Mkurugenzi wa Sera za Derivatives katika Shirika la Utetezi la Better Markets, alipoongea na CNBC Oktoba 15.

Kwa sasa, watumiaji wa Kalshi wanaweza kubashiri matukio mbalimbali, kuanzia ni lini mchezo wa video wa Grand Theft Auto VI utatolewa hadi ni lini msemaji wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt, atasema katika mkutano wake ujao na waandishi wa habari.

Watumiaji wa Polymarket wanaweza pia kubashiri matokeo kama hayo, ingawa watumiaji wa Marekani kwa sasa wamezuiwa kutumia jukwaa hilo kutokana na kanuni za Tume ya Biashara ya Baadaye ya Bidhaa (Commodities Futures Trading Commission).

Kama ilivyo kwa aina nyingine zote za kamari, kubashiri kupitia masoko ya utabiri kunaweza kuwa njia ya hatari.

Wataalamu wa fedha kwa kawaida hupendekeza kuwa uweke dau tu kwa kiasi unachoweza kumudu kupoteza, na kuepuka kuweka dau zaidi mara kwa mara baada ya kupoteza.

Papa anavyopatikana

Mchakato wa kumchagua Papa hufanyika mara chache sana na unahusisha vikao vya faragha vya makardinali wote wa Kanisa Katoliki walio na umri usiozidi miaka 80.

Katika Kanisa la Sistine, kura hupigwa kwa siri hadi jina moja lipate theluthi mbili ya kura zote.

Tangu enzi za karne ya 13, utaratibu huu umezingatia hadhi na heshima kubwa, huku ishara ya moshi mweupe juu ya paa la Sistine ikiashiria kumpatikana kwa Papa mpya.

Hata hivyo, ujio wa teknolojia na masoko ya kifedha ya kidijitali umechochea ongezeko la kamari katika matukio ya kidini na kisiasa.

Kwa baadhi, ni udhalilishaji wa imani; kwa wengine, ni njia halali ya kutengeneza pesa. Hili limeibua mjadala mpana kuhusu maadili ya kamari inayohusisha matukio ya kiroho.

Wakati waumini wakiendelea kumkaribisha Papa mpya, upande mwingine wa dunia unaangalia jinsi tukio hilo takatifu limegeuka kuwa mchezo wa pesa.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira, nyongeza na Kalunde Jamal.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *