Wabunge wataka usawa gharama za kuunganisha umeme, mikopo elimu ya juu

Dodoma. Wabunge wamependekeza mageuzi kadhaa katika sekta ya umeme na elimu kwa kuitaka Serikali kuondoa gharama za kuunganisha umeme na kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa usawa, bila ubaguzi kwa wanafunzi waliomaliza shule za binafsi.

Hoja hizo zimetolewa leo Jumanne, Novemba 5, 2024 wakati wa mjadala wa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa kueleza changamoto wanazoziona katika maeneo wanayowakilisha na mapendekezo ya maboresho kwa manufaa ya wananchi wote.

Mbunge wa Ukerewe (CCM), Joseph Mkundi, amependekeza gharama za kuunganisha umeme vijijini na mijini ziwe sawa, ili kuweka usawa wa huduma kwa wananchi wote.

Mkundi amefafanua katika maeneo ya mijini, wananchi hutozwa Sh300,000 kuunganishiwa umeme, huku maeneo ya vijijini yakiwa Sh27,000 na kwamba gharama zinapaswa kuwa sawa kwa wote.

“Ikiwezekana wananchi wapewe umeme bure na gharama hizo zikatozwe polepole kupitia bili wanazolipa kila mwezi,” amesema Mkundi na kuongeza;

“Hii itasaidia kuongeza uzalishaji na ubunifu katika jamii, watu wetu wataweza kutumia nishati ya umeme kujiinua kiuchumi na kuchangia kwa ujumla kwenye pato la Taifa.”

Kauli hiyo imeungwa mkono na mbunge wa Bunda Mjini, Chacha Maboto, anayesema kuondoa gharama za kuunganisha umeme kutasaidia wananchi wa vijijini, hususan wakulima na wafugaji ambao wengi wao hawana uwezo mkubwa wa kifedha.

Maboto ametoa mapendekezo kwamba Serikali iwaunganishie umeme bure na kuwatoza kidogokidogo kupitia bili zao za kila mwezi.

“Serikali ina mpango wa kupeleka umeme kwenye vitongoji ambako kuna wakulima na wafugaji ambao si wafanyabiashara. Ni bora kuwaunganisha kwanza na kisha kulipia polepole kupitia ununuzi wa umeme,” amesema Maboto na kueleza kuwa hatua hiyo itasaidia wananchi kujikimu kimaendeleo.

Mbunge wa Geita Mjini, Costantino Kanyasu ameeleza changamoto zinazowakabili wanafunzi wa elimu ya juu wanaotafuta mikopo, hasa wale waliomaliza shule za “English Medium” au za binafsi.

Amesema mfumo wa sasa wa mikopo una upendeleo dhidi ya wanafunzi hao, licha ya kwamba baadhi yao wanahitaji msaada wa mikopo, kwani wazazi wao walishafariki dunia.

“Mfumo unapaswa kuangalia mahitaji ya wanafunzi mmoja mmoja na sio kigezo cha shule walizosoma. Kuna watoto ambao wazazi wao wote wamefariki na wanahitaji msaada,” amesema Kanyasu na kuongeza kuwa, “ni muhimu kwamba haki ya kupata mkopo iwe sawa kwa wote, hasa kama mfumo hauwezi kugundua hali halisi ya mahitaji ya mwanafunzi.”

Kanyasu pia amesisitiza umuhimu wa kujenga vyuo vikuu vya tiba kwenye hospitali za kanda, ili kuongeza nafasi za wanafunzi waliomaliza masomo ya sayansi.

Ameeleza idadi ya wanafunzi wenye sifa za kusomea masomo ya tiba inazidi uwezo wa vyuo vikuu vilivyopo, ikiwamo Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), hivyo kujengwa vyuo vingine vya sayansi ni muhimu kwa ustawi wa Taifa.

Kwa upande wake, mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda amezungumzia umuhimu wa kuimarisha mfumo wa elimu kwa kuwa na mitalaa thabiti na isiyobadilika mara kwa mara.

Mwakagenda amesema mabadiliko ya mara kwa mara katika mitalaa huathiri ubora wa elimu, na kuwa watoto wanahitaji mfumo wa elimu unaowaweka kwenye mstari mmoja wa maendeleo.

“Tunaiomba Wizara ya Elimu kuhakikisha mitalaa haichezewi wala kubadilishwa kila wakati. Mfumo thabiti unasaidia watoto wetu kujikita kwenye elimu inayowajengea msingi mzuri wa maisha yao ya baadaye,” amesema Mwakagenda.

Kwa upande wake, mbunge wa Kilombero, Abubakari Asenga ameeleza masikitiko yake juu ya hali ya watoto wanaoishi mitaani katika miji kama Mwanza.

Amesema idadi ya watoto wa mitaani inaongezeka, jambo linaloathiri maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Ameonyesha wasiwasi wake kuhusu ongezeko la idadi ya watu nchini na changamoto za malezi, akitaja mfano wa video ya kijana wa bodaboda kutoka Mbeya aliyehimiza vijana wenzake kuwajibika katika malezi ya watoto wao badala ya kuwakimbia.

 “Tulipokwenda Mwanza, tuliona watoto wanalala kwenye korido za maduka. Watoto wengi hawajui wazazi wao na wanalazimika kujilea wenyewe. Hii ni changamoto kubwa inayohitaji kushughulikiwa,” amesema Asenga.

Mbunge wa Momba, Condester Michael Sichalwe amehitimisha hoja zake kwa kuitaka kampuni ya Vodacom kupunguza gharama za vifurushi vya intaneti, ili kuwawezesha wananchi kumudu huduma za mtandao kwa urahisi zaidi.

Amesema intaneti imekuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku, hivyo ni muhimu kuwa na gharama nafuu zinazomwezesha kila mtu kufaidika na fursa za kidijitali.