
Dodoma. Wabunge wameibua hoja ya umuhimu wa kuwa na sera na sheria mahususi zitakazosimamia matumizi ya akili mnemba (Artificial Intelligence – AI), wakisema teknolojia hiyo mpya ina faida nyingi, lakini pia inakuja na changamoto na madhara yanayohitaji kudhibitiwa mapema.
Wito huo umetolewa leo Jumamosi, Mei 10, 2025 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatuma Toufiq, wakati akifungua mafunzo maalum kwa wabunge kuhusu akili mnemba yaliyofanyika jijini Dodoma.
Toufiq ambaye aliyemwakilisha Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema pamoja na kwamba Tanzania imeshaanza matumizi ya akili mnemba lakini bado hakuna sera wala sheria inayozungumzia suala hilo.
“Hakuna sera wala sheria ya kuonyesha utumiaji wa akili mnemba, uendeshwe vipi lakini usimamiwe vipi ili kusudi kujua kwa matumizi hasi yanakabiliwa vipi. Lengo ni kuweza kuwalinda wale watu wanaoweza kuathirika,”amesema.
Amesema wameona katika matumizi ya akili mnemba waathirika wakubwa wa matumizi hasi wamekuwa ni wanawake.
Mafunzo hayo yaliandaliwa kwa ushirikiano wa shirika la kidijitali la Omuka, Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), na Taasisi ya Viongozi Wanawake Duniani (WPL).
Wabunge kutoka Kamati mbalimbali za Kudumu za Bunge, zikiwemo za Miundombinu, Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Elimu, Masuala ya Ukimwi, pamoja na Utawala, Katiba na Sheria, walihudhuria mafunzo hayo.
Naye Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Shirika la Omuka, Neema Lugangira amesema akili mnemba inaweza kuwasaidia wabunge kwa kwenye kuwatengenezea mpango mkakati katika shughuli zao za kisiasa, kibunge na uchaguzi.
Amesema uwezo huo unatokana na teknolojia hiyo kutumia muda mfupi kutafuta kila kilicho katika mitandao na kutoa picha ya mtu anayoitaka.
“Akili mnemba ni kitu ambacho kina tija. Lakini tija hiyo ili tuipate ni lazima itumike kwa ufasaha. Hivyo moja ya vitu tutakavyokwenda kuangazia kama wabunge ni lazima tuwe na Sera ya akili mnemba,”amesema.
Amesema kwa kuwa na sera kutawafanya kunufaika na faida zake lakini kujikinga pamoja na kudhibiti madhara yanayoweza kutokana na matumizi ya akili mnemba.
Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu amewaondoa hofu Watanzania kuwa mafunzo hayo, hayajaja kwa ajili ya kupoteza ajira za Watanzania kuboresha ajira.
“Mimi nikienda katika kampeni, nitawaambia kwa ukiona kuwa mtu amenitengenezea picha ya ajabu msishangae hiyo ni akili bandia na hiyo picha ni bandia. Mbunge wenu orginal (halisi) nipo hayo mambo siwezi kuyafanya,”amesema Msambatavangu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari (UTPC), Kenneth Simbaya ameshauri waandishi wa habari wanapotumia akili mnemba kujihakikishia usahihi wa takwimu kutoka vyanzo ilivyotoa taarifa hizo.
“Kitu kikubwa ni kucross check (kuhakiki) kwa sababu pia akili mnemba inaweza kukosea. Kwa waandishi wa habari tunapaswa kuendelea kujisomea ili kuwa na taarifa sahihi…Akili mnemba ina akili lakini anakaa nyuma ya hiyo akili mnemba ndio anaakili zaidi,”amesema.