
Dodoma. Tatizo la ajira limeibuka bungeni kwa Mbunge wa Sumve (CCM), Kasalali Mageni kukosoa mfumo wa ajira akisema hauko wazi.
Mageni amekosoa hilo leo Alhamisi Aprili 10, 2025 wakati akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2025/26 ya Ofisi ya Waziri Mkuu aliyoiwasilisha jana Jumatano.
Mbunge huyo amesema katika maeneo mengi watu wanapata ajira kwa kujuana ndiyo maana zikitangazwa nafasi watu wanaanza kutuma jumbe fupi (sms) kwa wabunge wao.
“Serikali ikitangaza nafasi za ajira simu za wabunge zinaanza kujaa sms watu wakiomba kusaidiwa kupana nafasi, huu utaratibu wa utoaji wa ajira unatakiwa kuangaliwa upya,” amesema Mageni.
Mbunge huyo ameomba ofisi ya Waziri Mkuu itazame kwenye eneo hilo na kuweka utaratibu mzuri ili kuondoa kilio cha watu nchini na kuifuta dhana ya ajira za kupeana.
Kwa upande wake, mbunge wa Vwawa (CCM), Joseph Hasunga amesema utaratibu wa utoaji wa ajira unatakiwa kuwashirikisha sekta binafsi, kwani Serikali peke yake haiwezi kumaliza tatizo la kuwapatia ajira watu wote.
Hasunga amekiri Serikali imekuwa ikitoa ajira za kutosha lakini wahitaji ni wengi kwa hiyo ni wakati Serikali kujenga mazingira ya ushirikishwaji kwenye jambo hilo.
Mbunge huyo amepongeza pia mpango wa Serikali wa kuwapa mafunzo maalumu wahitimu wa vyuo vikuu ili wapate ujuzi kupitia vyuo vya ufundi stadi (Veta), akisema mpango huo unakwenda kuwasaidia vijana wengi wasiokuwa na ajira.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Nusrat Hanje amezungumzia suala la ajira akisema bado halijawa sawa kwani kuna wimbi kubwa la raia wa kigeni wanaochukua nafasi za wazawa.
Hanje amesema kuna raia wa kigeni wanaouza heleni hadi za Sh3,000 kitu ambacho si sahihi kulingana na sera ya nchi kwenye suala la ajira.
Mbunge huyo amesema kuna haja ya Serikali kuangalia mifumo hiyo kwa kutumia vyombo vya ulinzi na usalama kwani halifichiki.
“Mheshimiwa Spika, kuna raia wa kigeni ambao wanakopesha hadi bukubuku kama wanavyofanya Waha, nendeni mkaangalie,” amesema Hanje.
Kauli za wabunge hawa zinaakisi matukio ya hivi karibuni wakati wa ajira za ualimu, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambapo maelfu ya watu walijitokeza kuziomba.
Sakata la ajira katika kada ya ualimu lilizua mjadala kiasi cha kusababisha kupishana katika kinachoitwa Chama cha Walimu wasio na ajira na Serikali.
Kwa ajira za Zimamoto watu wengi walilalamikia suala la vipimo vya urefu na uvungu wa miguu, huku TRA walilalamikia uchache wa nafasi kwa kundi kubwa la waombaji.
Ajira milioni nane
Akiwasilisha hotuba yake jana Jumatano kwenye eneo la utekelezaji wa ahadi za Serikali, Majaliwa alisema kuanzia Novemba 2020 hadi Februari 2025, ajira milioni 8.08 zimezalishwa kwenye sekta ya umma na binafsi.
Kuzalishwa kwa ajira hizo, alisema kunatokana na Serikali kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuzalisha fursa kupitia uwekezaji na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.
Miongoni mwa miradi hiyo, ametaja ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki, reli ya kisasa, Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato.
Pia, alisema Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kukua na kupanua wigo wa uzalishaji wa ajira nchini.
Majaliwa ameomba kuidhinishiwa Sh595.29 bilioni, kati ya hizo Sh183.82 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh411.47 bilioni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Fedha hizo ni ongezeko la Sh244.3 bilioni ukilinganisha na Sh350.99 bilioni alizoziomba mwaka 2024/2025
Kadhalika, ameomba kuidhinishiwa Sh186.79 bilioni kwa ajili ya mfuko wa Bunge, kati ya hizo, Sh174.96 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh793.33 milioni za maendeleo, sawa na ongezeko la Sh4.98 bilioni ukilinganisha na Sh181.81 bilioni alizoziomba mwaka 2024/2025.