Wabunge waibuka sakata la kukosekana kwa uzio katika shule

Dodoma. Kilio cha ujenzi wa uzio kwa shule msingi na sekondari leo limechukua nafasi kubwa baada ya wabunge wengi kusimama wakihoji lini shule zitajengewa uzio.

Maswali ya wabunge yaliibuliwa leo Jumanne Aprili 21, 2025 kufuatia swali namba 107 lililoulizwa na Mbunge wa Temeke, Doroth Kilave ambaye ameuliza kuna mpango gani wa kutenga fedha kujenga uzio katika Shule za Msingi na Sekondari – Temeke.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Tamisemi, Zainabu Katimba amesema Serikali inatambua umuhimu wa uzio kwa ajili ya ulinzi na usalama wa wanafunzi hususani maeneo ya mijini.

Naibu Waziri amesema katika mwaka 2024/25, Serikali ilitumia Sh190.7 milioni kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika shule za msingi Wailes na Likwati na Shule za Sekondari Miburani na Nzasa zilizopo Manispaa ya Temeke. 

“Mheshimiwa Spika, mwaka 2025/26, Serikali imepanga kutumia Sh200 milioni kwa ajili ya ujenzi uzio katika shule za msingi Kibasila, Mji mpya na Kibondemaji na Sh150 milioni katika shule mpya za sekondari za Chang’ombe, Makangarawe na Mwembe Bamia,” amesema Kapinga.

Amesema Serikali itaendelea kutenga fedha za ujenzi wa uzio katika shule za msingi na sekondari kupitia mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kadiri ya upatikanaji wa fedha. 

Wabunge wengine waliouliza kuhusu ujenzi wa uzio kwenye shule za majimboni mwao ni Anne Kilango Malecela (Same Mashariki), Sebastian Kapufi (Mpanda Mjini), Omary Kigua (Kilindi), Asharose Matembe na Neema Lugangira wote wa viti maalumu.

Kwa upande wake, Kilango amesema jimboni kwake kuna shule watoto wanashindwa kwenda masomoni kwa kuogopa Tembo kwani eneo hilo ni mapito ya wanyama hao wakubwa.

Katika majibu ya jumla kwenye maswali hayo, Naibu Waziri amesema Serikali inaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa uzio kwenye shule zote.

Naibu Waziri pia amewaagiza Wakurugenzi kutenga fedha kwa mapato ya ndani ili wajenga uzio kwenye shule zote walau kwa awamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *