Wabunge wacharuka fedha kilimo kutopelekwa kwa wakati

Wabunge wacharuka fedha kilimo kutopelekwa kwa wakati

Dodoma. Wabunge wameijia juu Serikali kwa kushindwa kuipelekea fedha za kutosha Wizara ya Kilimo, ikilinganishwa na bajeti iliyopitishwa katika mwaka wa fedha 2024/2025.

Wamesema hali hiyo imechangia kwa kiwango kikubwa kukwamisha baadhi ya shughuli za maendeleo za sekta hiyo, huku baadhi wakitaka kuanzishwa kampeni ya kuondoa jembe la mkono.

Wabunge hao wameyasema hayo leo Mei 22, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2025/26.

Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa Sh1.2 trilioni kwa mwaka 2025/26 huku Sh702.27 bilioni zikienda katika miradi ya maendeleo, ambapo Bunge liliidhinisha kiasi hicho cha fedha.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya ameshangazwa na wizara ambayo inalisha Taifa na kutengeneza ajira kwa Watanzania wengi kutopelekewa fedha zote ilizoidhinishiwa kwenye bajeti yake.

Amesema wizara hiyo imepokea asilimia 53 tu ya bajeti iliyopitishwa na Bunge, akisisitiza kuwa ingekuwa bora kama kiwango hicho kingefikia angalau asilimia 70 au 80.

“Ninawaomba wabunge wenzangu tuihimize  Wizara ya Fedha ipeleke fedha ili malengo mazuri yaliyowekwa na wizara hii yatimie,” amesema.

Bulaya ameongeza kuwa hatua hiyo itawasaidia Watanzania, wakiwamo wa Bunda mkoani Mara, kunufaika na shughuli za kilimo.

“Lazima tuhakikishe Wizara ya Fedha inaelekeza fedha katika maeneo nyeti ili Watanzania wanufaike na uhakika wa kilimo,” amesema.

Mbunge wa Muhambwe (CCM), Dk Florence Samizi ameshauri kutengwa fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya Wizara ya Kilimo katika mwaka wa fedha 2025/26.

“Serikali isipoweka fedha hizi, hata ile asilimia ya bajeti tunayoipanga haitaenda kwa wakati wala ukamilifu na malengo mazuri ya Waziri Bashe na Rais Samia Suluhu Hassan hayatofikiwa,” amesema.

Hoja ya kuchelewa kwa fedha imeibuliwa pia na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, ambayo imeeleza kutoridhishwa kwake na upatikanaji wa fedha na kuitaka Serikali kupeleka fedha kwa wakati.

Kilimo cha jembe la mkono

Mbunge wa Momba (CCM), Condester Sichalwe amesema baada ya kuanzisha programu ya Jenga kesho iliyo bora (BBT), sasa ni wakati wa kampeni ya kutokomeza matumizi ya jembe la mkono na kuhamia kilimo cha kidijitali.

“Pamoja na takwimu na jitihada ulizosoma za miaka minne, bado asilimia 60 ya Watanzania wanalima kwa kutumia jembe la mkono. Watakapolima kisasa, watatumia akili zaidi, nguvu kidogo, eneo dogo, lakini watazalisha kwa wingi,” amesema.

Ameongeza kuwa anatarajia, Bunge la 13 litakaporejea na wakati wa kusoma bajeti utakapowadia, Serikali itakuwa na takwimu zinazobainisha idadi ya wakulima walioondokana na jembe la mkono.

Mbegu za asili

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Neema Lugangira, amesema sheria ya sasa ya mbegu inawapa haki zaidi wafanyabiashara wakubwa, hivyo kuna haja ya kuifanyia marekebisho ili itambue pia umiliki wa mbegu za asili zinazotumiwa na wakulima wadogo.

“Pia sera ya mbegu ifanyiwe marekebisho ili iweze kutambua mbegu za asili, jinsi zitakavyosimamiwa na kulindwa, na kuhakikisha hazitafifishwa kutokana na mikataba ya kimataifa inayozipa upendeleo mbegu za kisasa kutoka nje ya nchi,” amesema Lugangira.

Amesisitiza umuhimu wa kuanzisha benki ya mbegu za asili ili kulinda haki na ustawi wa wakulima.

“Mbegu hizi zina mchango mkubwa katika lishe, kwani tafiti zimeshaonesha kuwa zina virutubisho vingi kama madini, chumvi na vitamini mbalimbali,” ameongeza.

Naye Mbunge wa Mchinga (CCM), Salma Kikwete amesema Tanzania kwa sasa ina uwezo wa kuzalisha mbegu kwa asilimia 80, lakini ni muhimu kuendeleza mbegu za asili ili kuliondolea Taifa utegemezi wa kununua mbegu kutoka nje.

“Mbegu za asili ni muhimu kwa Taifa lolote. Wakoloni walipokuja walitugawa na kutunyima vitu vyetu vya msingi, ikiwa ni pamoja na kutudhoofisha kwenye suala la mbegu. Tunahitaji kuwa na mbegu zetu ili kuondokana na aina mpya ya utumwa wa kikoloni,” amesema Salma.

Skimu za umwagiliaji

Mbunge wa kuteuliwa (CCM), Dk Leonard Chamuriho amesema miradi ya umwagiliaji iliyotekelezwa imeifanya sekta ya kilimo isihusishe tu chakula bali pia biashara, huku ikitoa ajira kwa vijana na wanawake.

Amepongeza bajeti ya wizara kwa kuitaja kuwa ni ya matumaini, na kusifu mpango wa BBT kwa kuleta mapinduzi makubwa katika sekta hiyo.

“Hakuna mashaka, wateja wa mazao yetu wapo ndani na nje ya nchi,” amesema Chamuriho.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Mbarali (CCM), Bahati Ndingo amesema jimbo lake limepokea miradi mitano ya umwagiliaji yenye thamani ya Sh80 bilioni ambapo Sh60 bilioni zaidi zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa saba.

“Miradi hii imeleta ukombozi kwa wakulima. Migogoro yote iliyokuwepo katika sekta ya kilimo sasa inaelekea kufikia mwisho,” amesema Ndingo.

Bajeti iliyowasilishwa ni ya wananchi kwa kuwa miradi ya skimu za umwagiliaji inalenga kuleta mageuzi katika maisha yao, amesema Mbunge wa Nzega Vijijini (CCM), Hamisi Kigwangalla.

Amesema kama miradi mikubwa itasimamiwa na kutekelezwa kama ilivyopangwa,  itakumbukwa na Watanzania kwa muda mrefu huku akimtaka Waziri wa Kilimo kuendeleza diplomasia ya chakula.

Akijibu hoja za wabunge kuhusu wizara hiyo kutopelekewa fedha kwa wakati, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema hadi Aprili mwaka huu walikuwa wamepelekewa Sh600 bilioni lakini aliwahakikishia wabunge  kuwa itakapofika Juni 30, 2025 watakuwa wamepata sehemu kubwa ya fedha kutoka Hazina.

“Tumekuwa na  majadiliano na Waziri wa  Fedha tunatarajia kuendelea kupata fedha ndani ya Mei, Juni, 2025 na naamini  hadi tutakapomaliza mwaka huu wa fedha tutakuwa tumepata sehemu kubwa ya fedha,”amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *