Wabunge, CAG waibua udhaifu ujenzi wa masoko

Dodoma. Suala la ujenzi wa masoko bila kuwashirikisha wafanyabiashara limeibuka bungeni, wabunge wakitaka wananchi washirikishwe kuanzia hatua za awali.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Masoko imeibua suala hilo leo Jumatano Mei 14, 2025 ilipowasilisha taarifa yake bungeni iliyosomwa na Mariam Ditopile.

Mariam, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo amesema ujenzi wa masoko umekuwa na changamoto kubwa kwani mengi yanajengwa maeneo siyo rafiki hivyo kuachwa.

“Ushirikishaji wananchi katika ujenzi wa masoko lazima uanzie ngazi ya awali, watu waulizwe yajengwe wapi ili Serikali isipate hasara ya kujenga majengo yakakosa watu,” amesema.

Kauli ya wabunge hao imekuwa ikitolewa mara kadhaa na wafanyabiashara hususan ndogo ndogo (machinga) wanaporejea maeneo yasiyo rasmi mitaani, wakilalamika wanakopelekwa ama mazingira si rafiki kwa biashara au miundombinu haijakamilika.

Mbali ya hao, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti kuhusu ukaguzi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2023/24 amezungumzia suala hilo. CAG alisema uwekezaji wa fedha za umma katika miundombinu ya masoko unapaswa kupangwa, kuendelezwa na kusimamiwa ipasavyo ili kuhakikisha matumizi bora, kuongeza tija ya kiuchumi na kuboresha utoaji wa huduma.

Amesema alipopitia uwekezaji katika masoko ya Mamlaka za Serikali za Mitaa alibaini ukosefu wa mipango madhubuti na ushirikishwaji duni wa wadau katika uwekezaji, uliosababisha matumizi hafifu kwa yaliyokamilika na upotevu wa mapato.

Mwongozo wa kitaifa wa kuandaa na kufadhili uwekezaji wa miundombinu inayozalisha mapato uliotolewa na Ofisi ya Rais- Tamisemi Julai 2021, unaeleza kuwa mamlaka za serikali za mitaa huandaa mapendekezo ya miradi bila mipango madhubuti, mara nyingi zikisahau kufanya upembuzi yakinifu, kutambua wadau muhimu, kubaini hatari na mbinu za kudhibiti.

“Hali hii husababisha changamoto wakati wa utekelezaji. Uwekezaji wa mamlaka za serikali za mitaa katika masoko unakutana na ufanisi mdogo kutokana na mipango duni, jambo linalosababisha masoko kutotumika ipasavyo. Usimamizi na uangalizi mzuri ni muhimu katika kuongeza mapato na kuzuia hasara,” alisema CAG katika ripoti hiyo. Alisema alipitia uwekezaji wa masoko katika halmashauri za Manispaa ya Kinondoni, Wilaya ya Hai na Wilaya ya Urambo na kubaini kutotumika ipasavyo kwa masoko yaliyokamilika, hivyo kusababisha kupoteza mapato na utoaji duni wa huduma.

“Masoko yaliyokamilika kwa kiasi kikubwa hayajapangishwa. Baadhi ya wafanyabiashara bado wanaendelea kufanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi, huku majengo ya masoko yaliyojengwa yakibaki wazi. Hali inayoonyesha tofauti kati ya uamuzi wa uwekezaji na mahitaji halisi ya biashara,” amesema.

Amesema alibaini baadhi ya masoko yametelekezwa kutokana na kuchagua maeneo yasiyofaa na ushindani kutoka kwa masoko mengine ya jirani, huku migogoro kati ya wawekezaji na mamlaka za serikali za mitaa ikichelewesha uendeshaji wa miundombinu iliyokamilika.

Pia ukosefu wa mifumo madhubuti ya usimamizi wa fedha na mipangilio ya usimamizi wa kiutendaji inaibua walakini kuhusu uwazi, uwajibikaji na uwekezaji endelevu na wa muda mrefu katika masoko.

“Iwapo changamoto hizi hazitatatuliwa zinaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa ukusanyaji wa mapato na kukua kiuchumi katika mamlaka za serikali za mitaa husika,” amesema.

Uamuzi wenye ushawishi wa kisiasa na tathmini dhaifu ya mahitaji amesema umesababisha miundombinu isiyolingana na uhitaji halisi, huku usimamizi dhaifu na ushiriki mdogo wa mamlaka za serikali za mitaa vikichangia kuendelea kwa hali hiyo.

“Matokeo yake ni upotevu wa mapato, upungufu wa fedha kwa ajili ya huduma na kutopata manufaa ya kiuchumi

yaliyokusudiwa. Iwapo hali hii haitashughulikiwa ipasavyo, kuendelea kutotumika kwa masoko hayo kutachochea uharibifu wa miundombinu, hivyo kushindwa kutimia kwa malengo ya kupata thamani ya fedha,” amesema.

Amependekeza Serikali kupitia mamlaka husika ikiwamo Ofisi ya Rais- Tamisemi na Wizara ya Fedha iwezeshe na kufuatilia mamlaka za serikali za mitaa ili kuhakikisha zinafanya tafiti za kina na kupanga maeneo ya kimkakati kwa ajili ya masoko, kuwezesha matumizi bora ya ardhi na ufanisi wa uwekezaji.

“Naishauri Serikali kuimarisha ushirikishwaji wa wadau ili kutatua migogoro ya umiliki na kuboresha mifumo ya usimamizi wa masoko, zikilenga matumizi sahihi ya masoko yaliyojengwa na kuboresha upangaji na usimamizi ili kuepuka kutotumika ipasavyo kwa masoko hayo,” amesema.

Kuhusu miundombinu

CAG amezungumzia kuhusu miundombinu isiyojitosheleza na usimamizi usioridhisha wa masoko, akisema unasababisha kutokuwapo kwa ufanisi kiuchumi.

“Masoko ya umma ni muhimu kwa uchumi wa ndani, lakini ufanisi wake unategemea usimamizi mzuri na miundombinu inayojitosheleza,” amesema.

Katika ukaguzi wa hali za masoko amesema ulibaini upungufu katika miundombinu na changamoto za usimamizi katika mamlaka sita za serikali za mitaa, zikiwa ni ukosefu wa majisafi na vyoo vinavyotumika hali iliyosababisha mazingira kuwa machafu.

“Nilibaini masoko kadhaa yamekuwa yakifanya kazi kwa muda mrefu bila vyoo, hali inayowalazimu wafanyabiashara na wateja kutumia njia mbadala zisizo salama kiafya,” amesema.

Ukosefu wa mifumo ya kutupa taka, mifereji duni ya maji na njia zisizopitika wakati wa mvua amesema umefanya masoko kuwa na mazingira yasiyo rafiki kwa biashara.

“Upungufu huu wa miundombinu na usimamizi duni umeathiri ufanisi wa masoko, kusababisha upotevu wa fursa za kiuchumi na mapato ya mamlaka za serikali za mitaa,” amesema.

Halmashauri husika zimetajwa kuwa Manispaa za Kinondoni, Kigamboni, Ubungo na Iringa, Jiji la Tanga na Wilaya ya Bukombe.

CAG amependekeza Ofisi ya Rais-Tamisemi ifanye tathmini ya kina ya miundombinu na usimamizi wa masoko ili kushughulikia changamoto hizo, kipaumbele kiwe ukarabati wa miundombinu iliyochakaa na kuweka huduma muhimu kama majisafi na vyoo bora.

Ameshauri Tamisemi kuweka mifumo madhubuti ya usimamizi wa taka, kuimarisha ulinzi na kuweka utaratibu wa ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kudumisha viwango vya usafi na kuboresha mvuto wa masoko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *