
Milan, Italia. Timu nane za kwanza kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya zilijulikana jana, huku Arsenal ikishinda mabao 2-1 dhidi ya Girona na Liverpool ikipoteza mchezo wake wa kwanza wa michuano hiyo msimu huu baada ya kulala kwa mabao 3-2 dhidi ya PSV.
Timu ya Manchester City ambayo ilikuwa ipo kwenye wakati mgumu, ilifanikiwa kushinda mchezo wake wa jana na kufuzu kwenye mtoano baada ya kuichapa Club Brugge mabao 3-1 na kumaliza kwenye nafasi ya 22.
Timu 8 zimefuzu moja kwa moja huku nyingine zikicheza mechi za mtoano kuhakikisha zinapata timu nyingine nane ambazo zitafikisha 16 ambazo zinatakiwa kwenye hatua inayofuata.
Timu nane ambazo zimefuzu moja kwa moja baada ya michezo ya jana ni Liverpool, Barcelona, Arsenal, Inter Milan, Atletico Madrid, Bayern Leverkusen, Lille na Aston Villa.
Wakati hizo zikiwa zimefuzu, timu 16 ambazo zitacheza mtoano ni Atalanta, Borussia Dortmund, Real Madrid, Bayern München, Milan, PSV , Paris Saint-Germain, Benfica, Monaco, Brest, Feyenoord, Juventus, Celtic, Manchester City, Sporting CP na Club Brugge.
Droo ya mtoano inatarajiwa kufanyika kesho ambapo timu zote zitapangwa zitavaana na nani kwenye hatua ya 16 bora, zile ambazo bado hazijafuzu zitapangwa kwenye mtoano endapo zitafuzu, hivyo hakutakuwa na droo nyingine ya hatua ya 16 bora zaidi ya hii ya kesho.
Timu ambazo zimeondolewa moja kwa moja kwenye michuano hiyo msimu huu ni zile ambazo zilishika kuanzia nafasi ya 25 mpaka 36 kwenye msimamo ambazo ni Young Boys, Bratslava, Salzburg, Girona, Leipzig, Sparta Praha, Sturm, Grevena, Bologna, Shakhtar, Stuttgart na Dinamo.