Waangalizi wa EU wanasema matokeo ya uchaguzi wa Msumbiji yalibadilishwa bila sababu

Waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya wamebaini “kubadilishwa bila sababu” kwa baadhi ya matokeo katika uchaguzi mkuu wa Msumbiji, huku kukiwa na shutuma za mgombea mkuu wa upinzani kwamba serikali ilimuua wakili wake.

Taarifa hiyo ya waangalizii wa uchaguzi wa EU imetolewa leo Jumanne siku moja baada ya raia wa Msumbiji kufanya maandamano wakipinga kinachosemekana kuwa ni udanganyifu katika uchaguzi wa rais na bunge wa Oktoba 9.

“Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi ya Umoja wa Ulaya [EU EOM] … imebaini dosari wakati wa kuhesabiwa kura na mabadiliko yasiyo na msingi ya matokeo ya uchaguzi katika vituo vya kupigia kura na ngazi ya wilaya,” imesema taarifa ya waangalizi wa EU.

Timu hiyo imezitaka mamlaka za uchaguzi katika nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika kuhesabu kura “kwa njia ya uwazi na ya kuaminika, na kuhakikisha ufuatiliaji wa matokeo ya vituo vya kupigia kura”.

Ghasia zilizoibuka baada ya uchaguzi nchini Msumbiji ziliendelea kuikumba nchi hiyo jana Jumatatu huku miito ya kurejeshwa utulivu ikitolewa.

Machafuko, Maputo

Vyombo vya usalama vya Msumbiji jana vililazimika kutumia mabomu kutoa machozi katika mji mkuu Maputo kuwatawanya waandamanaji.  Maandamano hayo sasa yamechukua sura ya kususia shughuli za serikali baada ya wito wa mgomo mkuu uliotolewa na kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane kulaani udanganyifu wakati wa uchaguzi wa rais.

Mondlane pia ameituhumu serikali kuwa imehusika na mauaji ya wakili Elvino Dias pamoja na mgombea wa ubunge kupitia chama cha Podemos Paulo Guambe nchini Msumbiji.

Wawili hao waliuawa baada ya gari lao kuzingirwa na magari mengine katika mji mkuu wa Maputo siku ya Jumamosi, wiki moja tu baada ya Mondlane kushiriki katika uchaguzi mkuu wa tarehe 9 ya mwezi Oktoba.

Kumekuwa na hofu ya kutokea machafuko ya kisiasa nchini humo hasa baada ya matokeo ya awali kuonesha kuwa mgombea wa chama tawala, Frelimo, atashinda kwa kura nyingi.