Waandamanaji mashariki mwa DRC walaani hatua ya Rwanda kufanya mazungumzo na waasi wa M23

Nyimbo na nara za wakazi wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi aya Congo zimedhihirisha wazi hasira yao dhidi ya hatua ya Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23. Mamia ya waandamanaji huko Butembo, mashariki mwa DRC, waliingia mitaani Jumanne ili kuonyesha uungaji mkono wao kwa wanajeshi wa Kongo na zaidi ya yote, kupinga mazungumzo yoyote na waasi wa M23.

Hasira hiyo imezuka wakati DRC na Rwanda zikiendelea na mazungumzo mjini Luanda kujaribu kutatua mzozo katika eneo hilo.

Waandamanaji hao pia, wamelaani mauaji yanayotekelezwa na kundi la kigaidi la ADF huko Kivu Kaskazini, mauaji ambayo yamekuwa yakiendelea tangu mwezi huu wa Oktoba. Kwa mujibu wa mashirika ya kiraia  tayari kumekuwa na vifo vingi zaidi ya 17,000.

Rose Kahavu, mmoja wa waandamanahi amesema: “Tunauawa kwa umati Beni, katika eneo la Lubero, tunasema imetosha tena, wape FARDC suhula zote zinazohitajika ili waweze kupigana na waasi wa M23 na ADF.”

Oparesheni hizi zinaendelea katika eneo hilo linalohusisha majeshi ya Kongo na Uganda, lakini juhudi hizi bado hazijamaliza ghasia katika eneo hilo. Siku ya Jumapili Oktoba 3, wakati wa mkutano na maafisa wa Uganda, Rais Félix Tshisekedi wa Kongo alitoa maagizo ya wazi ya kuimarisha ushirikiano wa kijeshi kati ya DRC na Uganda ili kumaliza ukosefu wa usalama katika eneo hilo.