
New York. Wananchi zaidi ya 300 wameandamana katika duka la kampuni ya Tesla mjini New York, Marekani, kupinga uongozi wa Elon Musk, imeripoti ABCNews.
Maandamano hayo yaliyofanyika katika maeneo mbalimbali ya Marekani Jumamosi, Machi mosi, 2025, yanalenga kupinga hatua ya Rais Donald Trump kumpa mfanyabiashara huyo jukumu la kusimamia Idara ya Ufanisi wa Serikali (DOGE).
Wengi wa waandamanaji walielezea hasira zao dhidi ya Musk, ambaye ana ushawishi mkubwa serikalini licha ya kutochaguliwa na wananchi. Wapo wanaohofia kuwa hatua zake ni za kujinufaisha kifedha kupitia kampuni zake nyingine kama SpaceX na jukwaa la X.
“Tunaweza kumwondoa Elon,” alisema Nathan Phillips, mtaalamu wa mazingira mwenye umri wa miaka 58 kutoka Newton, Massachusetts, aliyeshiriki katika maandamano ya Boston. “Tunaweza kuleta hasara za kiuchumi kwa Tesla, kwa kujitokeza katika maonyesho yao kote na kuhimiza watu wasinunue magari ya Tesla, wauze hisa zao, na kuachana na magari yao ya Tesla,” aliongeza.
Maandamano hayo ni sehemu ya wimbi la upinzani unaokua Amerika Kaskazini na Ulaya dhidi ya jukumu la Musk katika siasa za Washington.
Makundi yanayompinga Trump na Musk yamekuwa yakipanga maandamano ya kuipinga Tesla, na lengo ni kuzuia ushawishi wa DOGE na kuwapa moyo Wana-Demokrati walioshindwa na Trump Novemba mwaka jana.
Katika jiji la New York, polisi walisema watu tisa walikamatwa wakati wa maandamano hayo, ingawa hawakutoa maelezo zaidi kuhusu mashtaka waliyokabiliwa nayo.
Huku maandamano yakishika kasi, baadhi ya wamiliki wa magari ya Tesla wameripoti magari yao kuharibiwa, ikiwa ni pamoja na kupakwa rangi za swastika, hali inayohusishwa na ongezeko la chuki dhidi ya Wayahudi kulingana na makundi ya watazamaji wa haki za kibinadamu.
Huko Colorado, mwanamke alishtakiwa kwa uharibifu wa duka la Tesla, ambapo aliripotiwa kurusha molotov cocktails kwenye magari na kupaka maneno “Magari ya Nazi” kwenye jengo.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Harrison Fields, alisema kuwa maandamano hayo hayatawakwamisha Rais Trump na Elon Musk kutimiza ahadi yao ya kuanzisha DOGE na kuboresha ufanisi wa serikali ya shirikisho kwa manufaa ya wafanyakazi wanaolipa kodi.
“Hatuwezi kuruhusu serikali hii inayoongozwa na Trump na Musk iendelee kuporomoka, tuko hapa kuizuia,” alisema Carina Campovasso, mfanyakazi mstaafu wa serikali, akiwa kwenye maandamano ya Boston yaliyokuwa na hali ya sherehe, huku bendi ya shaba ikipiga muziki na waandamanaji wakibeba mabango yenye maneno ya kumpinga Musk.
Mpaka sasa, Tesla haijazungumza chochote kuhusu maandamano hayo, lakini bei ya hisa za Tesla imeshuka kwa karibu theluthi moja tangu Trump aingie madarakani, ingawa inasalia juu ikilinganishwa na mwaka uliopita. Thamani ya utajiri wa Musk kwa sasa inakadiriwa kuwa dola bilioni 359 kulingana na Forbes, huku ikionekana kuendelea kupungua kutoka bilioni 364 wiki iliyopita.
Maandamano zaidi yanatarajiwa kufanyika katika maeneo mbalimbali ya Marekani na Ulaya katika wiki zijazo, kulingana na tovuti ya Tesla Takedown.