
Kati ya vyuo vikuu 19 vilivyoshiriki katika mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira, vitano vimeibuka katika nafasi ya juu vikiongozwa na Chuo cha Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM- AIST) kilichopo halmashauri ya Jiji la Arusha.
Taarifa iliyotolewa kwa umma leo Jumatano, Aprili 9, 2025 na Wizara ya Afya imeonyesha NM-AIST iliibuka kuwa mshindi wa kwanza kwa kupata asilimia 93.3 ya alama zote.
Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) kilishika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 89.6 ya alama zote. Nafasi ya tatu ilishikwa na Catholic University of Health and Allied Science (CUHAS) iliyopata asilimia 84.5 ya alama zote.
Nafasi ya nne ilishikwa na Sauti kilichopo jijini Mwanza kwa asilimia 71.5 na nafasi ya tano ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kilichopo jijini Dar es Salaam kilichopata asilimia 70.5.
Vigezo ambavyo ni muhimu katika usafi ilikuwa maeneo yanayozunguka, uwepo usimamizi wa mpango wa usafi wa mazingira, uwepo wa vyoo bora, vifaa vya kunawa mikono na usafi kwa ujumla.