Vyombo vya habari vyatakiwa kufichua rushwa uchaguzi mkuu

Dar es Salaam. Vyombo vya habari nchini vimetakiwa kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa hususani kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Crispin Chalamila wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari katika warsha iliyoandaliwa na taasisi hiyo Aprili 29, 2025.

Chalamila amesema vyombo vya habari ni wadau muhimu katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, wa haki na usiohusisha vitendo vya rushwa.

Amesema kupitia uandishi wa habari za kichunguzi waandishi wa habari wanauwezo wa kuchunguza na kubaini viashiria vya rushwa katika mchakato wa uchaguzi na kuviripoti mamlaka husika.

“Vyombo vya habari vina jukumu kubwa katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kupinga masuala ya rushwa, hasa tunapoelekea katika kipindi cha uchaguzi,” amesema Chalamila.

Amesisitiza kuwa ni muhimu elimu hiyo ifikie kila mpigakura, hivyo bila ushirikiano haliwezi kufanikiwa bila kuwahusisha vyombo vya habari.

Ameeleza kuwa vyombo vya habari vina nafasi ya kuelimisha jamii kuhusu athari za kutoa na kupokea rushwa, pamoja na umuhimu wa kuchagua viongozi kwa misingi ya sera zao, siyo wale wanaotanguliza rushwa.

Chalamila amesema vitendo vya rushwa vinaharibu misingi ya demokrasia na utawala bora kwa kutoa upendeleo kwa wagombea wanaotoa rushwa na kuwanyima nafasi wale wanaostahili.

 “Rushwa hudhalilisha utu na thamani ya mtu. Kuzuia hali hii, kuna hatua nne muhimu ambazo ni kuhakikisha uteuzi wa wagombea unazingatia usawa, uwazi, uwajibikaji na uzalendo,” amesema.

Amesema ni muhimu kudhibiti matumizi mabaya ya rasilimali za umma, fedha za kampeni, na kuhakikisha vyama vyote vya siasa na wagombea wanapata fursa sawa.

Amesisitiza mazingira ya upigaji kura yanapaswa kuwa salama na ya haki, bila vitisho au upendeleo na malalamiko kushughulikiwa kwa uwazi na haki.

Chalamila amebainisha kuwa Serikali tayari imeanza kuchukua hatua kadhaa ili kuhakikisha uchaguzi wa 2025 unakuwa huru na wa haki na amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na jitihada zake za kupambana na rushwa.

“Namshukuru Rais Samia kwa namna anavyopambana na masuala ya rushwa ili kuimarisha mapambano dhidi ya janga hili,” amesema.

Akizungumza katika warsha hiyo, Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma Takukuru, Joseph Mwaiselo  amewataka wahiriri wa vyombo vya habari kuwa kiungo katika kufikisha elimu ya rushwa ili wananchi wachukie rushwa katika maeneo yao na kutoa taarifa.

Amesema kupitia vyombo vya habari inawezekana kutokomeza rushwa kwa kushirikisha makundi yote ili wawe na uelewa juu ya athari ya rushwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *