Shinyanga. Vyama vya ushirika mkoani Shinyanga vimetakiwa kujikita katika mifumo ya uwekezaji wa kidigitali na kujiendesha kibiashara badala ya kubaki masikini wakati vina rasilimali za kutosha ambazo zikitumika vizuri zitachangia kukuza uchumi.
Hayo yameelezwa jana Machi 28, 2025 na Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga, Kakozi Ibrahim wakati akifungua mkutano mkuu wa 30 wa Chama cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga (Shirecu) ambapo amesema inasikitisha kuona vyama vya ushirika bado ni duni.
Amesema vyama vya ushirika vina jukumu la kuwaondoa watu kwenye umasikini lakini matokeo yake badala ya kutekeleza jukumu hilo wanaanza kulalamika wakati wanarasilimali nyingi na kuwataka viongozi wake kujitathimini.
“Huu ni wakati wa vyama ushirika kubadilika tunataka kuona vyama vya ushirika vikijiendesha kibiashara, na siyo tena kutegemea huduma za msingi. Vyama vya ushirika lazima viwe na nguvu na viwe na uwezo wa kufanya biashara ili kusaidia wanachama wao,” amesema Ibrahim.
Ibrahim amesema vyama vya ushirika lazima viongeze nguvu katika kuzalisha mazao na kuwekeza katika miradi ya kiuchumi ili kuwa na michango inayokubalika, huku akiwataka kuacha kulalamika, badala yake watumie rasilimali walizonazo kuboresha hali zao za kiuchumi.
Kaimu Meneja Mkuu wa Chama cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga, Asnath Changamike amesema chama hicho kinakabiliwa na changamoto kubwa ya madeni ambapo deni wanalodaiwa ni Sh12.8 bilioni, hali inayosababisha ukuaji wa ushirika huo kusuasua na kushindwa kuwahudumia vizuri wakulima.
Amesema fedha ambazo zimekuwa zikipatikana kutoka kwenye vyanzo vingine vya ushirika zimekuwa zikiishia kulipa madeni, hivyo kushindwa kuwekeza kwenye miradi ya kiuchumi ili kusaidia kuimarisha zaidi hali ya kifedha na ustawi wa wake.
Amesema licha ya ushirika huo kumiliki mali zenye thamani ya zaidi ya Sh45 bilioni lakini bado hazijaleta tija kutokana na kushindwa kutumika ipasavyo na kusababisha mapato ya ushirika kubaki chini ikilinganishwa na rasilimali zilizopo, jambo linalohitaji nguvu ya pamoja.

Katibu tawala wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Paulo Faty akizungumza wakati wa mkutano mkuu wa saba wa chama kikuu cha ushirika Mbogwe na Bukombe (MBCU) cha mkoani Geita leo March 29, 2025. Picha na Amina Mbwambo
Mwanachama wa ushirika, Sekotule Maganga kutoka Amcos ya Kijiji cha Ngwangosha, amesema mfumo wa kidigitali unawasaidia kujua bei ya mazao pamoja na kupata taarifa mbalimbali za chama na mwenedo wa biashara kwa urahisi.
Kwa upande wake, Daniel Emmanuel kutoka Chama cha Msingi Kijiji cha Mangu, amesema anaamini kutokana na mikakati waliyoweka, changamoto za ushirika zitakwisha yakiwemo madeni na matumizi ya mfumo wa kidigitali.