
Volkano ya Mlima Nyamulagira, ulioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ilianza kuripuka tena tangu Jumamosi na hadi hivi sasa mripuko huo unaendelea.
Hayo yamethibitishwa na duru za habari na Kituo cha Uchunguzi wa Volkano cha Goma (OVG). Charles Balagizi, mkurugenzi wa masuala ya kisayansi wa kituo hicho cha OVG alisema jana Jumatatu kwamba: “Mripuko huo ulianza Jumamosi kwa kufurika lava kutoka kwenye kreta yake na hivi sasa lava inamiminika kwenye pande za kaskazini, magharibi na kusini magharibi.”
Picha za karibuni kabisa za satelaiti zinaonesha alama za kumiminika lava kwenye mlima huo katika pande zake tatu na inaelekea kwenye maeneo ya jirani na mlima huo.
Volkano ya Mlima Nyamuragira ni moja ya volkano hai zaidi barani Afrika. Iko katikati ya Hifadhi ya Taifa ya Virunga, ambayo kwa kiasi kikubwa inadhibitiwa na waasi wa M23 na hivyo kuifanya kazi ya mamlaka husika kuwa ngumu sana.
Katika upande mwingine, kwa miezi kadhaa sasa, wafanyakazi wa kituo cha OVG wako kwenye mgomo wakidai malimbikizo ya mishahara yao kutoka kwa serikali ya DRC.
Goma kuna volkano mbili hai, Nyamulagira na Nyiragongo. Mlima wa volkano wa Nyiragongo ulitipuka mwezi Mei 2021 na kuua watu wasiopungua 32. Kwa mujibu wa OVG, Nyamulagira iliripuka mara ya mwisho tarehe 14 Machi, 2023.