
Tanzania, Kenya na Uganda ndiyo nchi ambazo zinatarajiwa kuandaa mashindano makubwa ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), baadaye mwaka huu na Kombe la Mataifa Afrika mwaka 2027.
Wakati Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatangaza wazo la kuomba uenyeji wa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), wengi walionyesha wasiwasi kama hilo litafanikiwa.
Kulikuwa na sababu ya msingi ambayo ilifanya wadau wa soka kuwa na wasiwasi kuwa maombi hayo ya pamoja ya nchi za Tanzania, Kenya na Uganda zingekubaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kupewa uenyeji wa mashindano hayo.
Hofu kubwa ilikuwa ni uwezekano wa nchi hizo tatu kutimiza vigezo vya msingi ambavyo vimekuwa vikizingatiwa na kupewa kipaumbele katika kuipa nchi uenyeji wa mashindano hayo makubwa na yenye thamani zaidi kwa mchezo wa soka barani Afrika.
Kigezo cha usalama kisingekuwa sababu ya hofu hiyo kwa vile Kenya, Uganda na Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwa na amani na kuna uhuru mkubwa wa mizunguko ya watu pindi wanapokuwa ndani ya ardhi ya nchi hizo.
Uhakika wa huduma bora za usafirishaji na malazi ni jambo lingine ambalo CAF imekuwa ikilizingatia katika kutoa haki ya uenyeji wa fainali za AFCON kwa nchi husika.
Kigezo hiki nacho hakikuonekana kama kinaweza kukwamisha uandaaji wa Afcon 2027 kwa kuwa nchi zote hizi zimekuwa na mendeleo makubwa sana kwenye idara hiyo.
Wasiwasi mkubwa ilikuwa ni kwenye miundombinu hasa viwanja vya mazoezi na vya mechi ambapo kiuhalisia hadi muda wa kutuma maombi ya kuandaa, tulikuwa tuko nyuma sana.
Hata hivyo, mara baada ya kupewa tiketi ya kuandaa mashindano hayo, tumeona hatua za haraka kwa nchi zetu tatu kuboresha viwanja vya michezo na kuanza ujenzi wa vingine ili kuhakikisha mwaka 2027, unapofika viwe na namba inayotosha ya viwanja.
Tanzania ndio inaonekana kuwa na msukumo mkubwa katika suala la maandalizi ya viwanja kuanzia vile vya mazoezi na vya mechi. Tumeona maboresho makubwa yanayoendelea katika Viwanja vya Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na New Amaan Complex, Zanzibar.
Pia serikali imeweka nguvu kwenye ujenzi wa viwanja vingine vipya mkoani Arusha na Dodoma.
Mkataba wa ujenzi wa Uwanja wa Arusha ulisainiwa mwaka jana ambao utagharimu kiasi cha Shilingi 286 bilioni na ule wa Uwanja wa Dodoma ulisainiwa mwezi uliopita ambao utailazimisha serikali kulipa kitita cha Sh350 bilioni, hivi ni fedha nyingi sana ambazo serikali imewekeza hapa.
Kuwa na viwanja hivi ni jambo jema, lakini kuvitunza ni jambo lingine ambalo mikoa hiyo inatakiwa kuhakikisha kila mara vinakuwa kwenye mazingira mazuri.
Majiji hayo mawili yanatakiwa kuhakikisha viwanja hivyo vinatunzwa vyema ili viweze kutumika kwa muda mrefu badala ya matumizi yake kuishia katika fainali za AFCON tu kama ambavyo imekuwa ikionekana kwenye mataifa mengine.
Hivyo ni vyema Dodoma na Arusha kuandaa mipango mikakati ya kuhakikisha timu za mikoa hiyo zinakuwa na ushiriki endelevu kwenye ligi kuu baada ya AFCON 2027 kumalizika ili kuhakikisha vinatunzwa vyema na kuendelea kutumika vizazi na vizazi kwa kuwa mara nyingi tumekuwa na changamoto ya matunzo kama timu hazichezi Ligi Kuu.