Viwanja vikaguliwe kabla ya kufungiwa

Hivi karibuni kumekuwa na taarifa mbalimbali ambazo zimetoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) za kuvifungia baadhi ya viwanja vya Ligi Kuu Bara kutoka na kutokidhi mahitaji muhimu yayotakiwa kwenye kanuni.

Hili ni jambo zuri kwa kuwa inaonekana kuwa TFF inataka kuona ligi yetu inakuwa kwenye kiwango bora ambacho kinatakiwa na inataka kuhakikisha soka letu linakuwa kwa kasi kubwa.

Kwa sasa Ligi Kuu Bara inashika nafasi ya nne kwa ubora na kama mambo yataendelea kuwa mazuri basi tunauwezo wa kupanda hata hadi nafasi ya tatu au ya kwanza kwa miaka kadhaa ijayo.

Taarifa ilitoka ya kufungiwa uwanja wa Al Hassan Mwinyi uliopo Tabora ambao unatumiwa na timu ya Tabora United baadaye ikatoka ya kufungiwa Uwanja wa CCM Kirumba uliopo mkoani Mwanza, ikieleza kuwa havikidhi vigezo vinavyotakiwa na shirikisho hilo.

Hii ilionyesha kuwa TFF kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi wanataka kuhakikisha kuwa ligi hiyo inachezwa sehemu ambayo ina viwango vya kutosha.

Hata hivyo, viongozi wa timu hizo walikanusha kwa kusema kuwa viwanja vyao vinakidhi vigezo na wengine wakienda mbali kueleza hata kiwango cha fedha ambacho kilitumika kwa ajili ya marekebisho, jambo ambalo lilizua sitofahamu.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda ,ambaye ni mlezi wa timu ya Pamba ambayo inatumia Uwanja wa CCM Kirumba aliitisha kikao na baadhi ya viongozi wa mkoa huyo na wasimamizi wa uwanja na kugundulika kuwa hakuna ugeni ambao ulienda kuukagua uwanja huo kabla ya kufungiwa hali ambayo inazua maswali mengi.

Katika maelezo yake aliwaomba TFF na Bodi ya Ligi kwenda Mwanza ili kujiridhisha na kama kuna sehemu itakuwa na kasoro basi wawaeleze ili warekebishe haraka.

Hata hivyo, siku chache baadaye viwanja vyote vilifunguliwa na sasa vinaruhusiwa kutumika baada ya shirikisho hilo kusema kuwa limejiridhisha kuwa vipo sawa kwa ajili ya matumizi.

Tunafikiri pamoja na mambo mengine mengi, TFF kabla ya kuufungia uwanja inatakiwa kujiridhisha kuwa uwanja husika una matatizo na hauna vigezo vya kutumika kwa ajili ya ligi badala ya kusikia aidha kutoka kwa watu au kuona kwenye vyombo vya habari.

Kitendo cha kutangaza kuufungia uwanja na baada ya muda mfupi kuufungulia kinaleta maswali mengi kuhusu kamati inayosimamia viwanja hivi, lakini pia ni usumbufu kwa timu na mashabiki wanaotumia viwanja hivyo kwa kuwa wakati mwingine wanalazimika kutumia gharama kubwa kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kwa ajili ya mechi zao.

Tunaamini kuwa TFF ina viongozi karibu nchi nzima ambao wanaweza kutoa taarifa ambazo hazina maswali mengi na ikishindikana basi kamati husika inatakiwa kuhakikisha inafika sehemu husika.

Ni kweli kuna baadhi ya viwanja vinaonekana kwenye kamera kuwa vina kasoro, lakini ni jambo jema kama kamati husika itafika eneo hilo ili kuwa na uhakika ambao hauwezi kuzua mashaka yoyote kwa maendeleo ya soka letu.

Pamoja na kufika, ni vizuri pia kamati hiyo ikafanya ukaguzi ikiwa pamoja na viongozi wa eneo husika ili kuwaelekeza yale ambayo yanatakiwa kufanyika kwa kuwa kuna mengine yanaweza kufanyiwa kazi kwa haraka bila hata uwanja haujafungiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *