
Dodoma. Ujenzi wa viwanja vya michezo, mazoezi, maeneo ya kupumzikia na changamani ya michezo utachota mabilioni ya fedha katika makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka 2025/26.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi ameyasema hayo leo Mei 7,2025 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2025/26.
Wizara hiyo imeliomba Bunge kuwaidhinishia Sh519.66 bilioni huku miradi ya maendeleo ikitengewa Sh458.19 bilioni.
Akiwasilisha makadirio hayo Profesa Kabudi amesema mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Arusha katika mwaka 2025/26 umetengewa Sh193.09 bilioni.
Amesema uwanja huo mara baada ya kukamilika utakuwa na uwezo wa kuchukua watu 32,000 ambapo ujenzi wake unajumuisha miundombinu ya eneo la kukimbilia riadha.
Pia amesema ujenzi utahusisha viwanja vya mpira wa mikono, pete na netiboli na kuwa mradi huu ni sehemu ya maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027 kama uwanja wa mashindano.
Ameutaja uwanja mwingine ni mradi wa ujenzi wa eneo changamani la michezo Dodoma, katika mwaka wa fedha 2025/26 umetengewa Sh140 bilioni.
Amesema mradi huo utajengwa katika eneo la Nzuguni jijini Dodoma na mara baada ya kukamilika utakuwa na uwezo wa kuchukua watu 32,500.
Profesa Kabudi amesema uwanja utajumuisha viwanja vya mpira wa mikono, pete, na netiboli.
Kuhusu ujenzi wa vituo vya mazoezi na Kupumzikia wananchi, , Profesa Kabudi amesema katika mwaka 2025/26 umetengewa Sh8 bilioni.
“Shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi kwa Dar es Salaam na Dodoma inayojumuisha miundombinu ya majengo ya utawala,”amesema.
Vingine vitakavyojengwa ni viwanja vya mpira wa miguu, netiboli, pete, wavu, tenisi, vyumba vya kubadilishia nguo na eneo la mapumziko (recreation).
Aidha, amesema shughuli nyingine ni kuanza ujenzi wa awamu ya pili kwa Dar es Salaam na Dodoma unaohusisha jiko, bwawa la kuogelea lenye hadhi ya Olimpiki, uzio na eneo la mapumziko.
Pia amesema mradi wa ujenzi wa sports and Arts Arena katika mwaka 2025/26 umetengewa Sh450 milioni.
“Shughuli zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na kupata mshauri elekezi na kufanya upembuzi yakinifu wa mradi utakaohusisha michoro, gharama za ujenzi, utafiti wa athari za mazingira na andiko la biashara (business plan),”amesema.
Kuhusu ujenzi wa ujenzi wa eneo Changamani la Michezo jijini Dar es Salaam, Profesa Kabudi amesema katika mwaka 2025/26 umetengewa Sh29 bilioni.
“Shughuli zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na kuendelea na ukarabati mkubwa wa miundombinu ya Uwanja wa Uhuru ikiwamo kubadilisha viti chakavu na kuweka vipya eneo la watu mashuhuri (VIP),”amesema.
Ametaja shughuli nyingine ni kuweka viti vipya eneo la watazamaji wa kawaida (u-shape), kubadilisha paa, kurekebisha mifumo ya maji, umeme, viyoyozi, vyoo na eneo la kuchezea (pitch).
Aidha, Profesa Kabudi amesema shughuli zingine zitakazotekelezwa ni kuendelea na ukarabati kinga wa Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwamo utunzaji wa uwanja, miundombinu ya maji, umeme, mifumo ya zimamoto, kamera na kiyoyozi.
Bila kutaja kiasi cha fedha kilichotengwa, waziri huyo amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wamiliki wa viwanja itakamilisha taratibu na kuanza ukarabati mkubwa wa viwanja vitano vya CCM kwa mujibu wa makubaliano ya pande mbili.
“Msingi wa ukarabati huu ni kuongeza miundombinu ya michezo nchini, kuimarisha vituo vya mazoezi, ubora wa ligi na hatimaye timu zetu za Taifa,”amesema.
Kwa upande wa ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya michezo katika Shule maalumu za michezo, Profesa Kabudi amesema katika bajeti ya mwaka 2025/26 umepangiwa Sh11.5 bilioni.
“Shughuli zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na kuanza kwa ukarabati wa miundombinu ya shule maalumu saba za michezo ambapo ni pamoja na ununuzi wa vifaa vya michezo katika shule hizo,”amesema.
Amezitaja shule hizo ni pamoja na Dk Damas Ndumbaro Sec School (Songea-Ruvuma), Kicheba 135 Secondary School (Tanga), Ikwiriri Secondary School (Pwani), Babati Seconary School (Manyara) na Mtwara Ufundi Secondary School (Mtwara).
Nyingine ni New-Kiomboi Secondary School (Singida), Kanono Se (Karagwe Kagera).
Aidha amesema mradi wa Akademia ya Michezo katika Chuo cha Michezo Malya katika mwaka 2025/26 umetengewa Sh15 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo viwanja vya michezo mbalimbali.
Amesema pia wataanza ujenzi wa bwawa la kuogelea lenye hadhi ya olimpiki katika chuo hicho.
Aidha, Profesa Kabudi amesewa ujenzi wa ukumbi wa wazi wa sanaa katika mwaka 2025/26 umepangiwa Sh1 bilioni.