Viwanda vipya vinane vya asali kujengwa nchini

Viwanda vipya vinane vya asali kujengwa nchini

Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imejipanga kujenga viwanda vipya vinane vya kuchakata na kuongeza thamani kwenye mazao ya nyuki, ikiwemo asali na nta kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha sekta ya ufugaji nyuki kwa kuongeza thamani ya mazao yake, kuinua kipato cha wafugaji wa nyuki, na kuchochea ajira kupitia viwanda vidogo na vya kati.

“Uwepo wa viwanda hivi utahakikisha asali yetu inachakatwa kwa ubora wa hali ya juu na kufikia viwango vya kimataifa. Hili litatuwezesha kuongeza mauzo ya nje na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazotegemewa katika usambazaji wa asali duniani,” amesema Majaliwa.

Aidha, Majaliwa amesema kuwa Tanzania inaongoza kwa uzalishaji wa asali miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

“Kwa bara la Afrika, Tanzania inashika nafasi ya pili kwa uzalishaji wa asali, huku duniani tukiwa katika nafasi ya 14. Takwimu hizi zinaonesha wazi kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zinazotumia fursa ya rasilimali ya nyuki kwa manufaa ya kiuchumi,” amesema Majaliwa.

Amesema sekta hiyo imekuwa na mchango kwa Taifa na imeajiri watu zaidi ya milioni mbili na imeingia kwenye masoko mbalimbali duniani ikiwamo Uingereza na China.

Aidha, Majaliwa ameuagiza Mfuko wa Misitu Tanzania kuhakikisha unatenga fedha za kuwezesha vikundi vya wafugaji asali na wajieleze walipo, namna ya kupata kilichopo katika mfuko na masharti yaangaliwe.

Pia, ameuagiza Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), kuanzisha mashamba makubwa ya ufugaji nyuki kibiashara kwa kuruhusu wananchi kufunga mizinga katika misitu ili kuongeza kiwango upatikanaji wa asali na uhifadhi nyuki.

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana amesema pamoja na mafanikio mbalimbali ambayo kama nchi imeendelea kupata kupitia ufugaji nyuki, bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kiwango kidogo cha uzalishaji wa asali ikilinganishwa na uwezo uliopo.

Pia, ametaja changamoto nyingine kiwango kidogo cha asali kinachouzwa katika masoko ya nje ya nchi, kuendelea kwa matumizi ya mizinga ya asili ambayo huchangia katika uharibifu wa misitu na uvamizi wa maeneo ya hifadhi, ambayo ndiyo makazi ya asili ya nyuki na matumizi ya viuatilifu vinavyoathiri afya ya nyuki.

 “Kutokana na changamoto hizi, wizara kwa kushirikiana na wadau tumekuja na Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Ufugaji Nyuki ya Tanzania Iliyobora,” amesema.

Amesema mpango huo unalenga kuongeza kiwango cha uzalishaji wa asali kutoka tani 34,861 za sasa hadi kufikia tani 75,000 ifikapo Juni, 2035 na kuongeza mauzo ya mazao ya nyuki katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Kadhalika, amesema kupitia mpango huo takriban ajira mpya 43,055 zinatarajiwa kuzalishwa hasa kwa vijana na wanawake.

Waziri mkuu mstaafu,  Mizengo Pinda amewataka vijana kutumia fursa ya uwepo wa nyuki kujishughulisha na ufugaji wake na kusaidia ni kwa nini mazao yake yanaimarisha nchi kiuchumi

“Katika sekta ambazo nafikiri ni rahisi zaidi ni ufugaji wa nyuki, jaribuni kujifunza juu ya mdudu huyo na msaidie kueleza ni kwa nini tunampa nafasi kubwa namna hii. Mazao yanatokana na nyuki kiuchumi nayo yanatuimarisha sana,” amesema Pinda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *