
Dodoma. Serikali imeanzisha vituo vya umahiri 13 kati ya vituo 13 sawa na asilimia 100 ya lengo la miaka mitano.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga leo Jumatano Februari 12, 2025, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Shally Raymond.
Mbunge huyo amehoji vituo vingapi vya umahiri vya sayansi na teknolojia na akili mnemba katika taasisi za elimu ya juu vimeanzishwa.
Akijibu swali hilo, Kipanga amesema Serikali imeanzisha jumla vituo vya umahiri 13 kati ya vituo 13 sawa na asilimia 100 ya lengo la miaka mitano katika taasisi za elimu ya juu.
Amesema lengo la kuanzishwa kwa vituo hivyo ni kuimarisha uwezo katika utoaji wa Elimu ya Juu na utafiti katika maeneo ya afya na biolojia ya molekuli, Tehama, kilimo na mifugo, maji na nishati jadidifu.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuanzisha vituo vipya vya umahiri kulingana na mahitaji hususan katika kuimarisha mchango wa utafiti na ubunifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Septemba 9, 2024 Mkurugenzi wa Elimu Ufundi kutoka Wizara ya Sayansi na teknolojia Fredrick Salukeke alisema miongoni mwa vituo vya umahiri vimejengwa kupitia Mradi wa Kujenga Ujuzi kwa Maendeleo na Uingiliano wa Kikanda katika Afrika Mashariki (EASTRIP), uliofadhiliwa na Benki ya Dunia na kuanza kutekelezwa tangu mwaka 2019 na kugharimu zaidi ya Sh172 bilioni.
Alisema mradi huo hapa nchini umewezesha kujengwa kwa vituo vya umahiri vinne ambavyo ni kituo cha umahiri cha Mafunzo ya Tehama (RAFIC), katika Taasisi ya Teknolojia Kampasi ya Dar es Salaam, (DIT), Operesheni za Usafishaji (CoEATO) katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Vingine ni Kituo cha Mafunzo na Utafiti wa Nishati Jadidifu (Kikeletwa) katika Chuo cha Ufundi Arusha na Uchakataji Ngozi (CELPAT) kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Saalam Kampasi ya Mwanza.