
Dar es Salaam. Wakristo na Waislam duniani wapo katika kipindi cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na Kwaresma.
Wako katika kipindi cha toba ambacho baadhi ya maeneo yanashuhudiwa kuwa na jua kali jambo ambalo hufanya miili kuwa dhaifu. Pia baadhi ya watu hutokwa mpaka vipele kutokana na joto kuwapo kwa jua na joto kali.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Februari 12, 2025 ilitoa taarifa ya uwepo wa joto kali katika baadhi ya maeneo nchini, hususan yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kipindi hiki cha joto kali kimesababishwa na kusogea kwa jua la utosi sambamba na upungufu wa mvua unaojitokeza katika maeneo hayo
Licha ya uwepo wa hali hii ikiwemo nchini Tanzania haiwazuii watu kutimiza imani zao kupitia funga kama dini zao zinavyotaka ambapo hujizuia kula kwa kati ya saa 12 hadi 14 kwa Waislam.
Hali hii ya kukosekana kwa chakula au unywaji wa maji, wakati wa mchana hususan kwa wanaofunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, husababisha mwili kupoteza maji kwa kiwango kikubwa kwa siku, ingawa njia mbadala inaweza kutumika kupunguza tatizo hilo.
Mtaalamu wa lishe kutoka Hospitali ya Rufaa ya Tumbi, Mkoa wa Pwani, Fatma Mwasora anasema upungufu mkubwa wa maji mwilini hudhoofisha utendaji kazi kimwili na kiakili.
Anasema tafiti zinaonyesha upotevu wa maji unapokuwa mkubwa unaweza kuathiri utendaji kimwili, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa uzito wa mwili.
Kwa watu wanaoishi kwenye ukanda wa mazingira ya hali ya joto sana, upoteaji wa maji mwilini unaweza kuwa ni mkubwa zaidi.
Tafiti zinaonyesha upoteaji huo huweza kufikia takriban asilimia 1 ya uzito wa mwili hii ni kwa wale wanaofunga kila siku bila chakula au maji.
“Upotevu huu hauna madhara makubwa katika utendaji mwili bali kunapokuwa na hali ya joto kali sana, mwili huhitaji maji zaidi, kutokana na maji mengi mwilini kupotea kwa njia ya jasho,” anasema Fatma.
Ili kupunguza hali hiyo anasema ni muhimu kunywa maji ya kutosha angalau glasi nane au lita 1.5 kila siku kama ilivyopendekezwa katika miongozo, ili mwili ufanye kazi zake kwa ufanisi.
Hiyo ni kwa sababu mwili hutumia maji katika seli, viungo na tishu mwilini kukata kiu, kudhibiti hali ya joto la mwili na kuwa katika hali ya unyevunyevu.
Anasema macho, pua au mdomo unapokauka ina maana mwili unapoteza maji mengi kwa njia ya kupumua, kutoka jasho na wakati wa uyeyushaji wa chakula hivyo ni muhimu kunywa maji mengi ya kutosha na kula vyakula vyenye majimaji.
Tafiti zinaonesha maji husaidia kuweka au kuhifadhi viwango vya unyevu katika damu, mifupa na ubongo. Pia, maji yana faida katika uti wa mgongo.
Vitu vya kuzingatia ukifunga
Mtaalamu huyu wa lishe anasema katika kipindi hiki cha funga na joto kali, unywaji maji ya kutosha huusaidia mwili kutoa uchafu kupitia jasho, haja ndogo na kubwa kwani ni kipindi ambapo figo na ini hufanya kazi ya ziada kutoa uchafu mwilini.
Tafiti zinaonyesha maji husaidia kupunguza hali ya tumbo kujaa au kuvimbiwa kwa kulainisha choo kikubwa hasa wale wanakuwa katika mfungo.
Usagaji huo wa chakula hutegemea kuwepo kwa vichocheo ambavyo husaidia kuvunjavunja chakula na kuyeyushwa mwilini. Hivyo maji na ulaji wa vyakula vyenye nyuzinyuzi husaidia katika uyeyushwaji na husaidia kulainisha choo.
Ulaji uwaje
Anasema kipindi hiki cha mfungo ni vizuri kuzingatia ulaji wa mlo kamili unaotokana na vyakula mchanganyiko kutoka katika makundi yote matano ya vyakula.
“Ni vyema jamii ielewe kuwa kuna umuhimu wa kula vyakula vya asili ya nyama na jamii ya mikunde katika kipindi hiki cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kwani kundi hili husaidia huupatia mwili protini ambayo husaidia kujenga mwili na kuimarisha kinga ya mwili,” anasema.
Ulaji wa matunda na mbogamboga pia ni jambo ambalo linapaswa kuzingatiwa zaidi, kwani makundi haya husaidia kuupatia mwili madini na vitamini ambayo husaidia kuimarisha kinga ya mwili.
“Ni vizuri kula vyakula aina ya asusa (snacks) na matunda kwa wingi wakati wa mlo wa daku. Ni vizuri kunywa maji kwa wingi baada ya kufungua angalau lita moja na nusu kila siku.”
Pia mtu anayefunga anashauriwa kunywa supu, maziwa freshi au mtindi, juisi ambayo haijachanganywa na sukari.
Pia watu wanashuriwa kula matunda na mbogamboga kama vile tikiti maji, nyanya, tango na zabibu zinazojulikana kwa kiwango kikubwa cha maji ambayo husaidia kupunguza kiu.
“Epuka matumizi makubwa ya chumvi. Chumvi nyingi na vyakula vyenye viungo vingi kwenye futari, huongeza hitaji la maji mwilini hivyo ulaji wake unaweza kuongeza kiu na kuleta madhara kwa baadhi ya wagonjwa wa moyo na shinikizo la juu la damu wanapokuwa wamefunga,” anasema.
Pia watu wanashauriwa kuepuka kutumia sukari kwa wingi kwani tafiti zinaonyesha ulaji na matumizi makubwa ya sukari katika mapishi husababisha kuongezeka kwa uzito na kusababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile shinikizo la juu la damu, kisukari, magonjwa ya moyo na baadhi ya saratani.
“Inashuriwa kula matunda angalau aina mbili ili kuongeza maji mwilini na kukata kiu. Mfano ulaji wa matango yana maji mengi. Pia mtu anatakiwa kupunguza matumizi ya vinywaji vyenye Kafeini na nikotini kwani huongeza upotezaji wa maji mwilini na pia husababisha kiu,” anasema.
Vitu vya kuepuka
Vinywaji vya kafeini pia vinashauriwa kutoliwa pamoja na futari au daku na badala yake vitumike kabla au baada ya saa moja, kwani huzuia ufyonzwaji wa madini ya chuma.
“Epuka kuvuta sigara kwani husababisha kinywa kikavu na kiu endelevu, epuka kupigwa na jua au shughuli za kimwili wakati wa mchana kutokana na hali ya joto la juu na kupigwa na jua moja kwa moja, kwani kufanya hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kupata upungufu wa maji mwilini na kuongezeka kwa kiu,” anasema.
Kwa wale wafanya mazoezi, inashauriwa kwa kipindi hiki cha mfungo kufanya mazoezi baada tu ya futari.
“Mazoezi bora ni kutembea, kazi za nyumbani na ibada ya tarawehe kuwa zoezi zuri la kuushughulisha mwili.”
Ikiwa mtu atahitaji kufanya mazoezi atatakiwa kufanya mepesi na iwe kati ya saa mbili hadi tatu baada ya futari.
Mtaalamu huyo wa lishe pia anashauri wanaofunga kuepuka kazi nzito wakati wa jua kali au muda wa mchana na hasa katika hali ya hewa ya joto.
“Pia punguza kazi nzito au shughuli ngumu za kimwili wakati wa jua kali na joto, kwani zinaweza kusababisha ukapata kizunguzungu, kichefuchefu, kupumua kwa shida au maumivu ya kifua,” anasema.
Mtaalamu wa lishe, Dk Daudi Gambo anasema kuwa katika kipindi hiki cha joto kali ni muhimu kwa mtu anayefunga kuhakikisha anakunywa maji ya kutosha katika kipindi cha usiku kabla ya kuanza kwa siku nyingine ya mfungo.
Dk Gambo anasema hiyo itasaidia kurejesha maji ambayo yalipotea mwilini wakati wa mchana kupitia njia mbalimbali ikiwemo kutoka jasho.
Anasema pamoja na kunywa maji ya kutosha ni muhimu pia kutumia vinywaji vya asili kama maji ya matunda akitolea mfano wa madafu, juisi za matunda ambazo husaidia kurejesha madini ya mwili.
“Ni muhimu kuepuka kunywa maji mengi kabla ya kula chochote, ni vyema unapoanza kufuturu kuanza na uji ama chai ya moto”anasema.
Dk Gambo anasema katika kipindi hiki cha joto kwa anayefunga ni muhimu kuepuka vyakula vyenye mafuta mengi, chumvi au sukari nyingi.
“Ulaji wa vyakula hivyo huweza kusababisha mtu kupata kiu ya mara kwa mara hivyo kwa mtu anayefunga haswa kipindi hiki cha joto kali ni vyema kuviepuka”anasema.
Anaongeza kuwa mtu kufungua kwa kula vyakula ya moto, vyepesi ambavyo vitasagika tumboni kwa urahisi na vyenye glukosi kwa kuwa amekaa muda mrefu bila ya kula chakula.
“Pia wakati anakuwa amefunga utumbo unapokuwa unatafuta chakula na kukikosa husinyaa, hivyo ni vyema wakati wa kufungua kuanza na aina ya chakula au kinywaji cha moto na chenye glukosi ambayo itasaidia kusisimua enzyme na utumbo kuuweka tayari kwa ajili ya mmeng’enyo wa chakula.”
“Mfano wa baadhi ya vyakula hivyo ni tende, uji wa moto, supu, magimbi, maboga, juisi ya matunda pamoja na mihogo. Zingatia unapofungua kutokaa sehemu itakayokufanya utoke jasho jingi.
Anasema mbali ya wakati wa kula, aliyefunga anapaswa kuepuka kukaa mahali penye joto kali yatakayosababisha kutoka jasho jingi hasa nyakati za mchana.
“Ni muhimu kuhakikisha unakuwa katika mazingira ambayo unapata hewa ya kutosha ili kuepuka kupoteza maji mengi kwa njia ya jasho.
Anashauri kwa wale waliopo makazini kuhakikisha wanafanya kazi zao asubuhi wakati ambao mwili bado una nguvu ya kutosha.
Faida za funga kiafya
Daktari wa magonjwa ya binadamu, Rahel Mwinuka kutoka Hospitali ya Anglikana anasema kuwa faida kubwa inayozibeba nyingine juu ya tendo la kufunga kwa binadamu ni kuongezeka kwa kinga dhidi ya maradhi.
Dk Mwinuka anasema kinga hizo huongezeka kutokana na muhusika kuacha baadhi ya tabia ambazo alikuwa akifanya awali zikiwamo hatarishi kwa afya yake.
“Katika kipindi cha mfungo watu wengi huacha tabia za unywaji pombe, uvutaji sigara hivyo hufanya afya kuimarika.”
Anasema pia aina ya ulaji katika kipindi cha mfungo, watu kwa kupanga au kutopanga hula vyakula vya mchanganyiko vyenye virutubisho muhimu mwilini wanapofuturu au kula daku.
“Wengine kabla ya kufunga walikuwa hawazingatii ulaji wa lishe lakini kwa kipindi hicho wengi wao hujitahidi kula vyakula vya lishe ambavyo husababisha kinga zao kupanda,”alisema.
Anasema kuongezeka kinga humueusha muhusika na magonjwa ambukizi kama kikohozi, mafua na magonjwa mengine yanayoambukizwa kwa njia ya hewa.
Anashauri kwa wale waliopo makazini ni vyema kuhakikisha wanafanya kazi zao asubuhi wakati ambao mwili bado una nguvu ya kutosha.
Faida za funga kiafya
Pamoj na hayo kufunga nako kuna faida ambapo Daktari wa magonjwa ya binadamu, Rahel Mwinuka kutoka Hospitali ya Anglikana anasema kuwa faida kubwa inayozibeba nyingine juu ya tendo la kufunga kwa binaadamu ni kuongezeka kwa kinga dhidi ya maradhi.
Dk Mwinuka anasema kinga hizo huweza kuongezeka kutokana na muhusika kuacha baadhi ya tabia ambazo alikuwa akifanya awali zikiwa hatarishi kwa afya yake.
“Katika kipindi cha mfungo watu wengi huacha tabia za unywaji pombe, uvutaji sigara hivyo hufanya afya yake kuimarika.”
Anasema pia katika kipindi hiki baadhi watu hujikuta aidha kwa kutarajia au kutotarajia hujikuta wakila vyakula vya mchanganyiko vyenye virutubisho muhimu mwilini wanapofuturu au kula daku.
“Wengine kabla ya kufunga walikuwa hawazingatii ulaji wa lishe lakini kwa kipindi hicho wengi wao hujitahidi kula vyakula vya lishe ambavyo hupelekea kinga zao kupanda,”alisema.
Aliongeza kuwa kuongerezeka kwa kinga mwilini husaidia kumuepusha mtu na magonjwa ambukizi kama vikohozi na mafua na magonjwa mengine yanayoambukizwa kwa njia ya hewa.
“Faida nyingine za mfungo ni kuhifadhi uzito sahihi wa mwili pamoja na kudhibiti ongezeko la sukari,”anasema.