
Mambo yanaendelea kuwa mambo katika Ligi Kuu Bara, kwani vita zinazidi kuongezeka katika kila eneo kuanzia ile ya ubingwa, kuwania kufuzu mashindano ya kimataifa msimu ujao na ile ya kushuka daraja, lakini imechomoza pia ile ya kuwania kiatu cha ufungaji bora.
Clement Mzize kwa sasa ni kinara wa mabao katika Ligi Kuu Bara akifunga 13, jambo ambalo linaifanya vita ya kuwania ufungaji bora msimu huu kuwa na mvutano mkubwa kutokana na ukaribu uliopo kwa wanaoshindana huku zikibaki mechi chache za kuamua.
Mzize hajaachana sana na wanaomfuatia – Prince Dube anayecheza naye ndani ya Yanga na Jean Charles Ahoua wa Simba ambao kila mmoja ana mabao 12, huku Jonathan Sowa (11) na Elvis Rupia (10) wanaoicheza Singida Black Stars wakifuatia kwa kasi.
Kutokana na Ahoua kuwa na rekodi nzuri ya ufungaji ndani ya Simba huku akiwa mchezaji wa kikosi cha kwanza, inaweza kumfanya kuongeza idadi ya mabao katika mechi nne za viporo na kumrudisha kileleni kama ilivyokuwa awali kabla ya kuwepo kwa viporo hivyo.
Ahoua mwenye mabao 12 na asisti saba katika mechi 20, ana wastani wa kufunga bao 1.6, huku Mzize akiwa na wastani wa kufunga 1.9 kufuatia kucheza mechi 25 na kupachika mabao 25. Dube naye mechi 25 alizocheza na kufunga mabao 12 akiwa na wastani wa kufunga ni 2.1.
Kwa upande wa Sowah aliyeingia dirisha dogo la usajili msimu huu, amefunga mabao 11 katika mechi 11 akiwa na wastani wa kufunga bao kila mechi jambo ambalo linamfanya kuwa mshambuliaji hatari zaidi hadi sasa.
KAZI IPO HAPA
Mpaka sasa Yanga imecheza mechi 26 ikibakiwa na nne, imeshinda 23, sare moja na kupoteza mbili ikiwa imefunga mabao 68 na kuruhusu 10 ikiwa inashika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 70.
Inafuatiwa kwa karibu na Simba iliyocheza mechi 22 ikikusanya pointi 57, ikiwa bado mechi nane huku ikifunga mabao 52 na kuruhusu manane.
Wakati ligi ikiendelea, Simba ikicheza mechi zake nne za viporo na kufanikiwa kushinda zote itaachwa pointi moja na Yanga, hivyo kufanya ushindani kubwa mkubwa zaidi kuelekea kuwania ubingwa.
Singida Black Stars ni ya nne kwenye msimamo, imebakiwa na mechi tatu ambazo Sowah na Rupia kama wakichanga vizuri karata zao wanaweza kukaa juu kwa ufungaji.
Yanga imesalia na mechi nne mkononi, huku Simba ikibakiwa nazo nane, hivyo Dube au Mzize wanatakiwa kufunga mabao mengi zaidi katika kila mechi watakazocheza ili kubeba tuzo hiyo.
Rekodi zinaonesha ndani ya misimu kumi ya Ligi Kuu Bara kuanzia 2015-16, Tuzo ya Ufungaji Bora imechukuliwa na wachezaji kumi tofauti kutoka timu nne pekee huku Yanga ikibeba mara nne, Simba tano, Geita Gold moja sawa na Ruvu Shooting.
HAMDI HUYU HAPA
Kutokana na vita hiyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi, amewaachia maagizo Dube na Mzize kuhakikisha Tuzo ya Ufungaji Bora wanaichukua.
Maagizo hayo hayakuishia hapo kwani kocha huyo mwenye uraia wa Algeria na Ufaransa amewahakikishia washambuliaji hao kuwa atawarahisishia kazi kwa kuwaandaa viungo kutengeneza nafasi nyingi za wao kufunga. Tuzo ya Ufungaji Bora inashikiliwa na Stephane Aziz Ki wa Yanga aliyemaliza msimu uliopita na mabao 21.
Akizungumza na Mwanaspoti, Hamdi alisema, amewaambia washambuliaji wake hao kama sio Dube basi Mzize lazima wahakikishe wanachukua Tuzo ya Mfungaji Bora.
Alisema licha ya mechi kusalia chache huku ushindani ukiwa mkubwa, lakini anaiona nafasi hiyo kwa washambuliaji hao.
“Nimewaambia washambuliaji wangu kama sio Dube, basi Mzize lazima wahakikishe wanachukua Tuzo ya Mfungaji Bora na ili waweze kulifanikisha hilo wanatakiwa kuendelea kutumia nafasi.
“Hata wachezaji wenzao sasa wanawarahisishia kazi uwanjani kwa kuwatengenezea nafasi za kufunga zaidi, lakini pia mfumo wa timu namna inavyocheza haitakuwa na kisingizio kwao kutokuwa juu kwa ufungaji,” alisema Hamdi.