
Benchi la ufundi la Tabora United, limekiri kuwa vita yake na Singida Black Stars kuwania nafasi moja mojawapo kati ya nne za juu katika Ligi Kuu Bara inawatia presha ambayo inawalazimisha kuhakikisha wanashinda mechi zao.
Tabora Utd inakamata nafasi ya tano ikiwa imekusanya pointi 37 katika michezo 22, huku Singida Black Stars ikiwa kwenye nafasi ya nne na alama zake 41 ambapo Yanga inaongoza ikiwa na pointi 58 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 54.
Nyuki hao wa Tabora kesho Ijumaa Machi 7, 2025 watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuwaalika JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu raundi ya 23. Timu hiyo inatumia uwanja huo baada ya Alli Hassan Mwinyi, Tabora kufungiwa na Bodi ya Ligi kwa kutokidhi vigezo.
Akizungumzia maandalizi ya timu yake katika mkutano na waandishi wa habari jijini Mwanza leo Machi 6, 2025, kocha msaidizi wa Tabora United, Khalfani Mbonde amesema wanahitaji alama tatu ili kufikisha pointi 40 na kuisogelea Singida Black Stars ambayo inawapa presha kwa sasa.
“Ni kweli presha iko juu kutokana na vita yetu na Singida Black Stars kwasababu nasi tunapambana kuhakikisha tunawapita jambo ambalo linatuumiza lakini mechi zetu hatuogopi na hatuna wasiwasi tunachotaka ni ushindi tu,” amesema Mbonde.
Mbonde amesema licha ya kutumia uwanja wa ugenini, hawana wasiwasi kwani wamejipanga vyema na wachezaji wako kamili kwa mchezo wa kesho huku wakichagizwa na rekodi nzuri ya mzunguko wa pili ambao wamepoteza mchezo mmoja pekee dhidi ya Simba.
“JKT Tanzania hawatusumbui wala hatuwaogopi na hatuna wasiwasi kwa mchezo wa kesho, mashabiki waje kuangalia burudani nzuri kwa sababu sehemu yoyote tukienda ni kama nyumbani,” amesema Mbonde.
Mshambuliaji wa timu hiyo, Moses Msukanywele amesema wachezaji wameshakubaliana na wanapenda kupata alama tatu katika michezo yao yote, hivyo wako tayari kisaikolojia na kimbinu kwa mchezo wa kesho ili kuwapa furaha mashabiki wao.
“Maandalizi yamefanywa vizuri na makocha na sisi wachezaji tumefuata maelekezo wanayotaka makocha kwenye mchezo huu, tunaamini kila mchezaji ana morali ya kuisaidia timu kushinda kesho,” amesema Msukanywele.
Ofisa Habari wa Tabora United, Christina Mwagala amesema tangu mwanzo wa msimu walikuwa na malengo mawili ya kutwaa ubingwa ama kumaliza ndani ya nafasi nne za juu, hivyo, wanapanga kuhakikisha lengo hilo la pili linafanikiwa baada ya lile la ubingwa kugonga mwamba.
“Lengo la kwanza limekuwa gumu lakini hili la pili linawezekana, katika hizi nafasi tatu tunaamini kwamba tunaweza kuzifikia, hivyo, lazima tufanye vizuri katika mechi zilizopo mbele yetu,” amesema Mwagala na kuongeza;
“Tumeshafikia hatua ambayo tukienda mahali popote hatujihisi kama tuko ugenini kokote tunacheza na ndiyo maana tumepata ushindi katika mechi nyingi za ugenini.”