Vita ya Lugalo ilivyozaa jina kambi ya jeshi

Neno Lugalo kwa wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Iringa, siyo geni.Kwa Iringa jina hilo linawarudisha hadi miaka ya 1891 wakati Chifu Mkwawa wa Wahehe alipokuwa akikabiliana na jeshi la Mjerumani.

Kwa Dar es Salaam, Lugalo ni jina la kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania mahala ilipo pia hospitali maarufu ya Lugalo inayomilikiwa na jeshi hilo.

Upo uhusiano mkubwa wa mfanano wa Lugalo ya Iringa na ile ya Dar es Salaam.

Ni hivi kambi ya Lugalo ilipewa jina hilo na Mwalimu Julius Nyerere baada ya Uhuru, ikiwa sehemu ya kuenzi na kukumbuka namna Chifu Mkwawa alivyoligaragaza jeshi la mkoloni Mjerumani katika sehemu iitwayo Lugalo. Eneo hilo kwa sasa lipo wilayani Kilolo.

Julai mwaka 1891, kiongozi wa Kikosi cha maofisa wajerumani 13 wakiongozwa na Von Zelewski pamoja na askari 320, baadhi wakiwa Waafrika kutoka Sudan pamoja na wapagazi 113 walitaka kuwashughukia Wahehe.

Kikosi hicho kilikuwa na bunduki za kisasa na mizinga midogo, hivyo Zelewski akawadharau Wahehe kwa sababu wao walikuwa na silaha duni kama mikuki na pinde.

Kutokana na hali hiyo, Zelewski hakuona haja ya kutuma wapelelezi wa awali kujua uwezo wa Mkwawa na jeshi lake.

Historia inaeleza kuwa akiwa njiani na kikosi chake alikutana na Wahehe watatu waliomkaribia, naye akaagiza wauawe bila mazungumzo.

Wahehe hao walikuwa wajumbe wa Mkwawa aliyetaka kufanya majadiliano na Wajerumani.

Zelewski aliongoza kikosi chake mpaka aneo la Lugalo, hiyo ilikuwa ni Agosti 17, 1891.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu na Iringa na mtafiti wa historia, Jimson Sanga anasimulia kuwa wakiwa karibu na eneo la Lugalo, walikutana na nyasi ndefu hivyo wakalazimika kupita hapo.

Mkwawa alikuwa anamsubiri akiwa na askari wake 3,000 na walinyamaza mpaka Wajerumani waliposogea na kuanza kuwashambulia.

Inasadikiwa kuwa Wajerumani walikosa muda wa kuandaa silaha zao, hivyo sehemu kubwa ya askari waliuawa akiwamo Von Zelewski.

Kutokana ushindi huo Wahehe walipata bunduki 300 za kisasa walizokusanya, mizinga miwili na bomu moja.

Mzee maarufu mkoani Iringa, Gerald Malangalila anasema vita hiyo ilimpatia sifa kubwa Mkwawa ambaye alipigana akiwa na silaha duni.

Mtembeza wageni katika makumbusho ya Boma Iringa mjini, Abobakar Said anasema mpaka sasa mzinga mmoja, umehifadhiwa kwenye makumbusho hiyo.

“Mzinga ni sehemu ya makumbusho, unatunza historia ya vita ya Lugalo,” anasema.