Vita ya kuisaka Ligi Kuu Bara inaendelea

BAADA ya jana kupigwa mchezo mmoja kati ya Transit Camp dhidi ya Mbeya City, raundi ya 24, Ligi ya Championship inaendelea tena leo kwa michezo minne kwenye viwanja tofauti, huku ikihitimishwa kesho Jumapili kwa mechi nyingine tatu.

Kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara, Polisi Tanzania iliyotoka sare ya bao 1-1 na Bigman FC, itaikaribisha Mbeya Kwanza, yenye kumbukumbu mbaya ya kucharazwa ugenini mchezo wake wa mwisho kwa mabao 3-0, mbele ya Geita Gold.

Kiluvya United iliyochapwa pia mabao 4-0, dhidi ya Mbeya City, itakuwa kwenye Uwanja wa Mabatini Pwani kucheza na Songea United yenye ari kubwa baada ya mechi ya mwisho kubaki na pointi tatu nyumbani, baada ya kuichapa Transit Camp mabao 3-0.

‘Chama la Wana’ Stand United iliyoichapa Mtibwa Sugar nyumbani bao 1-0, itasalia tena kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga kucheza dhidi ya African Sports, iliyotoka kuchapwa ugenini bao 1-0 na ‘Wanajeshi wa Mpakani’ Biashara United.

Mchezo wa mwisho utapigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha na Mbuni FC iliyolazimishwa suluhu dhidi ya Cosmopolitan ugenini, itajiuliza mbele ya Green Warriors yenye kumbukumbu ya kuchapwa mechi ya mwisho 1-0 na TMA FC.

Kivumbi cha ligi hiyo kitaendelea tena kesho Jumapili kwa michezo mitatu kupigwa na TMA iliyoichapa Green Warriors bao 1-0, itakuwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kucheza na Cosmopolitan iliyotoka suluhu na Mbuni FC.

Vinara wa ligi, Mtibwa Sugar baada ya kuchapwa mechi iliyopita bao 1-0 na Stand United, itakuwa Uwanja wa Manungu Complex mjini Morogoro kuikaribisha Biashara United inayoburuza mkiani na pointi zake saba baada ya michezo 23.

Mchezo wa mwisho wa raundi ya 24, utapigwa Uwanja wa Ilulu Lindi na Bigman FC iliyotoka sare ya kufungana bao 1-1, dhidi Polisi Tanzania, itaikaribisha Geita Gold, yenye kumbukumbu ya kuichapa Mbeya Kwanza mechi ya mwisho mabao 3-0.

Kocha wa Songea United, Meja Mstaafu Abdul Mingange alisema licha ya nafasi ya nane waliopo ila bado wana matumaini ya kusogea juu zaidi kutokana na kutopishana pointi nyingi na wapinzani wao, huku akikomaliza sana safu ya ushambuliaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *