Vita ya injini kurindima Dar

BARABARA za vumbi ndani ya viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe Dar es Salaam zimeandaliwa  kuelekea raundi ta tatu ya mbio fupi za magari, keshokutwa Jumapili.

Ni mashindano ya tatu ya mbio fupi za magari Dar es Salaam na safari hii yanatakuwa na bango la Toyota  Dar Sprint, kwa mujibu wa Chama cha Mbio za Magari Tanzania (AAT).

Bingwa mtetezi wa mashindano hayo ni Manveer Birdi ambaye alishinda pia raundi mbili za awali katika viwanja hivyo.

Birdi anarudi Tanganyika Packers siku saba baada ya kushinda mbio za magari za Mkwawa ambazo ni raundi ya kwanza ya ubingwa wa magari kitaifa mwaka huu akiwa pia ni bingwa mtetezi baada ya kuibuka mshindi 2024.

Kwa mujibu wa AAT, zaidi ya washiriki 50 wanategemewa kushiriki katika mashindano hayo.

Mashindano haya yanahusisha magari maalumu ya mashindano, magari ya kawaida pamoja na pikipiki za magurudumu manne.

“Wengi wa washiriki wanatoka jijini Dar es Salaam, lakini tunategemea wachache kutoka mikoa ya jirani,” ilisema taarifa ya AAT.

Mbio fupi za Toyota Dar Sprint zinafanyika Tanganyika Packers takriban miezi mitatu baada ya kufanyika kwa mbio za magari za Usiku wa Mbalamwezi ambazo mshindi alikuwa Manveer Birdi akifuatiwa na Randeep Singh.

AAT imeeleza kwamba  walioshiriki raundi mbili za awali watakuwepo tena safari hii na wengi wao wakipania kuuangusha ufalme wa Birdi.

Wapinzani wengine ni Harinder Deere, Irfan Aladin, Zubair Piredina, Salim Haji, Ethan Taylor, Kelvin Taylor na David Bicco.

“Tunawakaribisha wapenzi na mashabiki wa mbio za magari kufika kwa wingi katika viwanja vya Tanganyika Packers ili kujua nani ni bingwa wa raundi hii,” alisema mwenyekiti wa kamisheni ya mbio za magari nchini, Satinder Birdi ambao ni waandaaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *