Vita ya Hamdi, Fadlu hapatoshi

KILA mtu anazungumza tukio moja tu kuhusu mechi kubwa Afrika Mashariki na Kati linalohusisha mechi ya Yanga na Simba.

Huo utakuwa mchezo wa mwisho baina ya timu hizo kwenye ligi msimu huu ambapo mzunguko wa kwanza Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Hata hivyo, kwenye mechi hiyo kocha wa Simba, Fadlu Davids ataingia kwenye mechi ya tatu dhidi ya Yanga akitangulia kukutana nayo kwenye nusu fainali ya Ngao ya jamii akipoteza kwa 1-0 kisha kukubali kipigo kama hicho kwenye ligi.

Yanga itaingia ikiwa na kocha mpya ambaye atalionja joto la mechi hiyo kubwa nchini kwa mara ya kwanza, Miloud Hamdi lakini jambo zuri kwake ni kwamba ana kikosi kinachojua presha ya mchezo kama huo.

DABI 08

MFUMO MMOJA

Makocha wote wawili Fadlu na Miloud wanatumia mfumo mmoja lakini kuna namna wanatofautiana katika utekelezaji wake sambamba na ubora wa wachezaji waliopo kwenye timu hizo mbili.

Fadlu anatumia mfumo wa 4-2-3-1 ambao pia ndio mfumo anaoutumia Miloud uliokuwa unatumiwa na watangulizi wake kuanzia Nasreddine Nabi, Miguel Gamondi na baadaye Sead Ramovic lakini ukweli ni kwamba huu ndio mfumo unaotumiwa na klabu nyingi duniani kwa sasa unaorahisisha mambo ukitengeneza usawa mzuri wa kikosi kuzuia, kutengeneza mashambulizi na hata kumalizia.

DABI 07

YANGA KIUNGO

Nguvu kubwa ya Yanga ambayo itambeba Miloud ni namna safu yake ya kiungo ilivyo na nguvu ya kutengeneza mashambulizi.

Wenyeji wa mchezo huo wana safu bora ya kiungo inayojua kuzuia na hata kutengeneza mashambulizi mtego mkubwa kwa Simba unatakiwa kuwa hapa, kama wanataka kutoka salama basi wahakikishe wanawadhibiti viungo wa watani wao.

Uwepo wa wachezaji kama Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Stephanie Aziz KI, Clatous Chama, Mudathir Yahya, Khalid Aucho na Duke Abuya hii inampa nafasi kubwa Miloud kufanya maamuzi ya nani awatumie kuunda safu yake imara ya kiungo itakayompa ushindi.

DABI 06

SIMBA MABEKI, KIUNGO

Ukiitazama Simba ina tofauti kidogo na Yanga, wao nguvu yao kubwa ya kujenga mashambulizi inatokana na mabeki wake wa pembeni hususan beki wake wa kulia Shomari Kapombe  na nahodha wake Mohammed Hussein ‘Tashabalala.

Mabeki hawa wawili wamekuwa na kasi ya kupandisha mashambulizi ingawa kwenye mechi hii haitakuwa rahisi sana kwao kufanya mambo kama mechi zingine kwa kuwa wanajua kwamba maeneo yao yatakuwa yanakabiliwa na viungo hatari ambao kama watapata nafasi ni rahisi kuwamaliza.

DABI 04

MPANZU, KIBU, AHOUA

Kuna viungo watatu wa Simba watakuwa na nguvu kubwa ya kutengeneza ushindi lakini wawili kati ya hao ni wazi watakuwa silaha muhimu kwa Fadlu kuanza kujenga mashambulizi yao ambao ni Kibu Denis na Ellie Mpanzu anayecheza dabi ya kwanza.

Mpanzu na Kibu watakuwa muda mwingi wanatokea pembeni na katikati kwa matukio machache lakini nguvu yao ya kukimbia na mpira na kuwapunguza mabeki, Yanga inatakiwa kuwa nao makini kwani endapo walinzi watafanya papara wanaweza kujikuta wanasababisha madhara makubwa kwenye lango.

Juu ya viungo hao yupo Jean Charles Ahoua ambaye anajua kupiga pasi za maangamizi akiwa anacheza dabi ya tatu lakini shida yake kubwa ni kwamba amekuwa anakosa uchangamfu kwenye mechi kubwa kama hizi.

DABI 02

UKUTA SIMBA PRESHA, YANGA NAKO MH!

Kabla ya mchezo huu Simba imekuwa ikionyesha ina safu bora ya ulinzi ikiwa imeruhusu mabao nane pekee lakini presha kubwa kwao ni kama afya za beki wake wa kati Che Malone Fondoh na kipa chaguo la kwanza Moussa Camara afya zao ziko sawa kabla ya mchezo baada ya kukosa uliopita.

Wawili hao ni nguzo muhimu kwenye ukuta wa Simba kutokana na viwango ambapo endapo wataukosa mchezo huo inaweza kuwa changamoto kwa timu yao kwenye utulivu wa ukuta.

Hali ya wasiwasi ipo pia kwenye ukuta wa Yanga ambao umeruhusu mabao tisa ambapo umekuwa ukifanya makosa na yakijirudia hali inaweza kuwa tofauti.

DABI 01

MILOUD FRESH, FADLU PRESHA

Kule mbele utulivu wa washambuliaji anaweza kuwa nao Miloud ambaye mastaa wake wawili Clement Mzize na Prince Dube wote wamefunga jumla ya mabao 20 ambapo kila mmoja akifunga nusu ya mabao hayo.

Safu hiyo ndio bora zaidi lakini habari njema kowa ni kwamba washambuliaji hao wenye kasi wamehusika na mabao 30 ya timu hiyo msimu huu kutokana na Dube kuwa na asisti saba wakati Mzize ana asisti tatu.

Simba iko tofauti kidogo ambapo washambuliaji wake wawili, Leonel Ateba na Steve Mukwala wamefunga jumla ya mabao 16 ambapo kila mmoja akifunga nusu ya mabao.

Washambuliaji hao wamehusika kwenye jumla ya mabao 21 kutokana na kuwa na asisti tano ambapo Ateba anazo tatu huku Mukwala mbili.

Mmoja kati ya washambuliaji hao ndiye ataanza kwenye mchezo huo, lakini ikumbukwe juu ya washambuliaji hao wawili mtu hatari ni Ahoua ambaye ndiye kinara wa ufungaji kwa Wekundu hao akihusika kwenye jumla ya mabao 16 yakiwemo mabao 10 aliyoyafunga akiongoza ufungaji sambamba na Dube na Mziz,e lakini pia kiungo huyo akiwa na asisti sita.

DABI 03

YANGA KASI ZAIDI

Ni kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake Miloud timu yake nayo ina kasi inapoanza nusu ya wapinzani wake, ikiwahi kwenda kumalizia mashambulizi yake ambayo viungo wake na hata washambuliaji wake wamekuwa mwiba kwa wapinzani kwa nidhamu hiyo.

Simba mambo yako tofauti kidogo kasi yao sio kubwa sana inategemea na Kibu na Mpanzu zaidi lakini pia hata inaposhambuliwa bado hawana kasi kubwa kwenye kuwahi kuwadhibiti hatua ambayo Fadlu lazima aifanyie kazi.