Vita vya Urusi na Ukraine: ICRC yachunguza hatima ya watu 50,000 waliotoweka

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu imesema siku ya Alhamisi, Februari 13, kwamba inajaribu kutafuta waliko karibu watu 50,000, wengi wao wakiwa wanajeshi, ambao wametoweka wakati wa mzozo kati ya Urusi na Ukraine tangu mwaka 2022.

Imechapishwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

“Tangu Februari 2024, idadi ya kesi za wazi za watu waliotoweka waliotafutwa na familia zao imeongezeka zaidi ya mara mbili, na kufikia karibu 50,000 leo na idadi hii kwa bahati mbaya inaendelea kuongezeka,” Dusan Vujasanin, ambaye anaongoza jitihada za ICRC, amewaambia waandishi wa habari, akibainisha kuwa zaidi ya 90% ya watu hao ni askari.

Mkutano wa “haraka”

Kremlin inasema inataka mkutano wa “haraka” kati ya Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Marekani Donald Trump, baada ya mazungumzo ya simu kati ya viongozi hao wawili, ambao walikubali kuanza mazungumzo ya kumaliza mzozo nchini Ukraine.

“Kwa hakika ni muhimu kwa mkutano huu kufanyika kwa haraka, wakuu wa nchi wana mengi ya kusema wao kwa wao,” msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa habari.

Kremlin pia inasema inataka mazungumzo juu ya Ukraine na juu ya usalama barani Ulaya na wasiwasi wa Moscow, ambayo mnamo mwaka 2021 iliitaka NATO kujiondoa kutoka bara la Ulaya. “Kwa hakika, masuala yote yanayohusiana na usalama katika bara la Ulaya, hasa yale yanayohusu nchi yetu, Shirikisho la Urusi, lazima yajadiliwe kwa pamoja, na tunadhania kwamba itakuwa hivyo,” Dmitry Peskov amebainisha