

- Author, Quentin Sommerville
- Nafasi, BBC
Kisanduku cheusi kipo kwenye dashibodi ya gari la jeshi, skrini yake ndogo inawaka ikitoa maonyo ikiwa ndege zisizo na rubani za Urusi ziko juu yetu. Tunaendesha gari kwa kasi kwenye barabara ya mashambani wakati wa giza karibu na mstari wa mbele nje ya Kharkiv.
Juu ya paa la gari kuna antena tatu zenye umbo la uyoga ambazo zinafuatilia ndege zisizo na rubani. Gari hilo hutoa ulinzi kwa kutatiza baadhi ya ndege zisizo na rubani za Urusi (lakini sio zote) zinazoshika doria angani juu ya uwanja huu wa vita,
“Imegundua ndege droni ya Zala Lancet za Urusi,” anasema Luteni Yevhenii, 53, kutoka kiti cha mbele cha abiria. Ni mojawapo ya ndege zisizo na rubani zenye nguvu za masafa marefu za Urusi.
“Ndio maana tunaendesha gari kwa kasi?” Ninauliza, nikifahamu kwamba mfumo wetu wa ulinzi juu ya gari haufanyi kazi kwa ndege za aina ya Lancet.
“Sisi sio kipaumbele chao, lakini ni bora kutopunguza kasi kwa sababu ni hatari sana,” anasema Yevhenii, kutoka Brigedi ya Khartia ya Jeshi la Kitaifa la Ukraine.
Vifaa vya kutatiza droni huzuia takribani 75% ya frikwensi ambazo droni hutumia kuwasiliana na waendeshaji wao, lakini baadhi ya droni kama Lancet ni vigumu kutatiza frikwensi hizo kwa sababu zinajiendesha zenyewe punde shabaha inapowekwa alama.
Kwa sababu ya uwezo wa Lancet, hutumika kulenga shabaha kubwa zaidi, kama vile magari ya kivita au wanajeshi wa ardhini walio mstari wa mbele.
Teknolojia hii haikuwepo hapa Ukraine mwaka mmoja uliopita. Lakini sasa ipo huku Ukraine ikijitahidi kuzuia Urusi kusonga mbele.
Vita vya angani

Jeshi la Ukraine linatumia droni zake kujibu mapigo. Askari mmoja wa Ukraine ananiambia kila siku wanaua takribani askari 100 wa Urusi.
Kamanda wa brigedi ya droni mwenye umri wa miaka 37, anaetumia jina la Aeneas, anasema, “ni njia mpya katika vita vya kisasa. Mwaka 2022 vilikuwa ni vita vya ardhini na leo nusu ya vita ni droni, vita kati ya ndege zisizo na rubani za Urusi na zetu.”
Ukraine inakabiliwa na uhaba wa makombora, na washirika wake wamekuwa wazito kuyazalisha na kuyapeleka. Lakini baadhi ya nchi washirika wa Ukraine wamehidi kuipatia nchi hiyo ndege zisizo na rubani milioni moja mwaka huu.
Urusi imefanya ubunifu wake kwenye uwanja wa vita pia, kwa kutumia teknolojia ya zamani, na kijiji cha Lyptsi, maili sita tu (10km) kutoka mpaka wa Urusi, kimelipa gharama.
Kijiji hicho kiliharibiwa na mabomu ya enzi za Soviet. Baadhi ni makubwa na hufika kilo 3,000 na yanapoachiwa kutoka kwenye droni, hushambulia wanajeshi wa mstari wa mbele wa Ukraine na huleta athari mbaya kwa miji.
Mwanamke mmoja aitwaye Svitlana, aliyekimbia Lyptsi kwa sababu ya mashambulizi haya, alituambia: “Kila kitu kilikuwa kikilipuka vipande vipande. Kila kitu kilikuwa kinawaka. Inatisha. Huwezi hata kutoka nje ya handaki.”
Vikosi vya droni

Aeneas anatupeleka katika vikosi vya droni, karibu na mstari wa mbele huko Lyptsi. Kila gari tulokutana nalo limefungwa vifaa vya kutatiza ndege zisizo na rubani; lakini ulinzi huo huisha unapotoka kwenye gari.
Ni hatari ukiwa eneo la wazi, kwa hivyo tunamfuata Aineas akikimbia kwenye vifusi ili kujificha. Wakati huo huo kifaa cha kutambua ndege zisizo na rubani cha BBC kinaita kwenye sikio.
Tukipumua kwa nguvu, tunafika kwenye kituo cha chini ya ardhi cha kitengo cha ndege zisizo na rubani chini ya jengo lililoharibika, tunatambulishwa kwa marubani wawili, Yakut na Petro.
Kuna ndege zisizo na rubani kwenye kila kipembe, hadi karibu na karai na mlo wao wa jioni. Nyingi ni za matumizi ya mara moja tu, hulipuka kwenye shabaha zao.
Droni wanayoipenda ni First Person View (FPV), ambayo hubeba shehena ya kati ya kilo 1 na 2 ya vilipuzi. Ni droni zilizoboreshwa ambazo zina kamera inayoleta picha kwa rubani.
“Tunaziita ndege za sherehe nchini Ukraine. Zilitumiwa kurekodi sherehe za harusi na karamu kabla ya vita,” anasema Aeneas.
Mimi natazama kwenye skrini kando ya Yakut ambaye anapeperusha ndege isiyo na rubani yeye mwenyewe kuelekea kwenye shabaha, kwenye uwanja wazi na misitu.
“Anajua kila dimbwi, kila mti katika eneo hilo,” anasema Petro.
Droni hiyo ya FPV inakaribia jengo ambalo mwanajeshi wa Urusi anaaminika kujificha. Inaingia kupitia dirisha lililo wazi na kulipuka, skrini ya rubani inaganda huku picha ikipotea.
Wakati huo huo, timu nyingine ya droni inalenga gari la kivita la Urusi aina ya Tigr na kulishambulia moja kwa moja, tukio hilo linanaswa na droni nyingine inayotazama kutoka juu.
Wanaume hawa hukaa kwenye maeneo haya, wakiendesha droni mchana na usiku, hadi siku tano kwa wiki na kisha hutoka kidogo kunyoosha miguu na kutumia muda nje.
Hofu yao kubwa ni mabomu makubwa. Moja lilitua karibu yao mapema wiki hiyo, na jengo zima likatetemeka.
Kipi kitatokea ikiwa kuna shambulio la moja kwa moja kwenu? namuuliza Petro. “Tunakufa,” anajibu.
Aeneas ananionyesha video ya mwanzoni mwa wiki. Askari wa Urusi ananaswa na ndege isiyo na rubani ya kitengo hicho. Askari anaiona na kukimbia ili kujificha, akijificha kwenye bomba la kupitishia maji kando ya barabara.
Umbali wa maili tatu. Polepole droni inashuka chini, ikiangalia upande mmoja wa bomba hilo, kisha inazunguka upande mwingine, ambapo askari amejificha.
Inalipuka na askari huyo analipuliwa anafariki kando ya barabara. “Aligawanywa sehemu mbili,” anaeleza Aineas.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla