Vita Shirikisho yaanza upyaa

SIMBA na Coastal Union zinafunga hesabu za Ligi Kuu kwa raundi ya 22 kabla ya mambo kuhamia katika Kombe la Shirikisho na hatua ya 32 itaanza kupigwa kesho Jumapili ikihusisha michezo tisa itakayojumuisha timu za Ligi Kuu, Ligi ya Championship, First League na RCL.

Mechi hizo ni za kusaka timu 16 zitakazochuana hatua ya 16 Bora kusaka nafasi nane za kutinga robo fainali ili kuanza kusaka ubingwa wa michuano hiyo ambao kwa sasa unashikiliwa na Yanga kwa misimu mitatu mfululizo.

Kwa mujibu wa ratiba ya hatua hiyo ya 32 Bora, kesho kuna mechi kati ya mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu wa mwaka 1967, Cosmopilitan itakayokuwa wenyeji wa KMC, huku Tanzania Prisons itaumana na Bigman na Kagera Sugar itaikaribisha Namungo kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.

Mechi nyingine za kesho ni kati ya Kiluvya United dhidi ya Pamba Jiji, Mashujaa itakayoialika Geita Gold, ilihali wana fainali wa msimu uliopita, Azam FC itakuwa wenyeji wa Mbveya City, ilihali Singida Black Stars itaikaribisha Leo Tena iliyoiduwaza Dodoma Jiji na kuing’oa hatua ya 64 Bora na mechi ya mwisho itazikutanisha Fountain Gate na Stand United ‘Chama la Wana’ mjini Karatu, Manyara.

Ratiba inaonyesha kuwa Jumatatu itakuwa ni zamu ya timu 12 tofauti kuumana, ambapo Mbeya Kwanza itakuwa nyumbani kuikaribisha Mambali Ushirikiano, Polisi Tanzania na Songea United zitaonyeshana kazi mjini Moshi, huku vinara wa Ligi ya Championship na mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu 1999 na 2000 Mtibwa Sugar itakwaruzana na  Towns Stars.

Mechi nyingine za Jumatatu itazikutanisha Girrafe Academy  dhidi ya Green Warriors, maafande wa JKT Tanzania watakaoumana na vibonde wa Ligi ya Championship  Biashara United wakati Tabora United itaonyesha kazi na maafande wa  Transit Camp.

Vigogo wa soka nchini Simba na Yanga zenyewe zitacheza mechi zao za raundi hiyo ya 32 Bora wiki ijayo mara baada ya Dabi ya Kariakoo  itakayopigwa Machi 8 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Simba ndio itakayokuwa ya kwanza kuvaana na TMA Stars ya Arusha Machi 11 na siku inayofuata, itakuwa zamu ya Yanga kukabiliana na Wagosi wa Kaya, Coastal Union wakikumbushia fainali za mwaka 2022 iliyopigwa jijini Arusha na timu hizo kufunga mabao 3-3 katika dakika 120 kabla ya penalti 4-1 kuipa Yanga ubingwa ikiinyanga’anya Simba na tangu hapo haijauachia ubingwa huo.