VITA ya ufungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake (TWPL) inazidi kupamba moto kati ya mastaa wawili, Stumai Abdallah ((JKT Queens) na Jentrix Shikangwa (Simba Queens) huku mbio zao zikikolezwa na takwimu bora kati yao.
Wachezaji hao wameendelea kukabana koo kwenye ufungaji wa mabao kila mmoja akikitaka kiatu cha kufumania nyavu kwenye ligi hiyo msimu huu wa mwaka 2024/2025.
Stumai Abdallah wa JKT Queens ndiye kinara wa mabao mpaka sasa katika raundi ya 12 ya ligi hiyo akiwa ametupia kambani mabao 18, huku Jentrix Shikangwa akifukuzia kwa karibu na mabao yake 17.
Stumai ambaye ni mzawa amefikia mabao hayo 18 baada ya mchezo wa mwisho dhidi ya Mlandizi Queens kufunga mabao saba katika ushindi wa mabao 12-0 akiweka rekodi mpya ya mchezaji aliyefunga mabao hayo kwenye mchezo mmoja wa michuano hiyo.
Mbali na nyota hao kuwa na vita yao lakini timu zao pia zinachuana vikali kuwania ubingwa wa ligi msimu huu ambapo Simba Queens inaongoza ikiwa na alama 34 katika mechi 12, huku JKT Queens ikifuatia na alama 29 baada ya michezo 11.
STUMAI ABDALLAH
Mbio hizi ni muhimu zaidi kwa Mtanzania huyu ambaye anatafuta rekodi kwa mara ya kuwa kuwa kinara wa mabao Ligi Kuu ya Wanawake ambayo misimu iliyopita amekuwa akinyang’anywa tonge mdomoni.
Ni timu mbili tu za Simba Queens na Yanga Princess ambazo mshambuliaji huyu mzawa hajazifunga mabao msimu huu, huku timu nyingine nane akiziadhibu vikali.

Katika mabao 18 aliyoyafunga mpaka sasa likiwemo moja la penalti, mabao 13 ameyafunga kwenye mechi tatu tu, mechi hizo ni dhidi ya Mlandizi Queens (7), Alliance Girls (3) na Malndizi Queens (3).
Mlandizi Queens ni timu ambayo imefungwa mabao mengi zaidi na Stumai Abdallah mpaka sasa akiifunga jumla ya mabao 10. Kati ya hayo, matatu aliyafunga kwenye ushindi wa mabao 7-0 na saba akifunga mchezo wa marudiano katika ushindi wa 12-0.
Mshambuliaji huyo ana hattrick tatu alizozifunga dhidi ya Mlandizi Queens (3), Alliance Girls (3) na Mlandizi Queens (7). Mabao saba aliyoyafunga kwenye mchezo dhidi ya Mlandizi alitupia dakika ya tatu, 5, 14, 18, 25, 36 na 88.
JENTRIX SHIKANGWA
Nyota huyu raia wa Kenya anatafuta kiatu cha pili cha ufungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake nchini kwani amewahi kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo msimu wa mwaka 2022/2023 akitupia mabao 17.
Baada ya hapo alitimkia Beijing Jingtan ya China ambako alidumu miezi sita na Januari 11, 2024 alirejea tena Simba Queens na kuendeleza moto wake.
Mabao yake 17 ameyafunga katika mechi nane tu kati ya 12 za timu yake msimu huu huku akizionea zaidi Fountain Gate na Ceassia Queens ambazo amezifunga nje ndani.
Shikangwa amefunga hat trick tatu dhidi ya Gets Program akitupia mabao matatu, Mlandizi Queens akitupia manne na Fountain Gate akifunga matatu. Pia amefunga mabao mawili mawili dhidi ya Alliance Girls na Ceassia Queens.

Ni timu tatu pekee mpaka sasa ambazo hazijafungwa na Jentrix Shikangwa. Timu hizo ni Yanga Princess, JKT Queens na Mashujaa Queens.
MISIMU ILIYOPITA
Ni wachezaji wawili tu wa kigeni wameshachukua kiatu cha ufungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara ambao ni Jentrix Shikangwa (Kenya) msimu wa 2022/2023 na Asha Djafari (Burundi) msimu wa mwaka 2021/2022.
2019/20 – Fatuma Mustapha (JKT Queens) – mabao 33
2020/21 – Aisha Masaka (Yanga Princess) – mabao 35
2021/22 – Asha Djafari (Simba Queens) – mabao 26
2022/23 – Jentrix Shikangwa (Simba Queens) – mabao 17
2023/24 – Aisha Mnunka (Simba Queens) – mabao 20
WASIKIE WADAU
Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Soka la Wanawake Mkoa wa Arusha, Manka Mbise alisema ushindani kwenye ligi hiyo unazidi kuwa mkubwa kila siku ukichagizwa na wadau wengi kuona umuhimu wa mashindano hayo na kuyapa thamani kubwa.
“Ukitazama hawa wafungaji wanaokimbizana yaani Stumai na Jentrix ni kama wana ligi yao peke yao ukilinganisha na wanaofuata jambo ambalo pia naona ni la kuwafanya wenzao wapate wivu na kutia nia ya kuweza angalau kuwafikia au kuwapita kabisa ikiwezekana ila kwa sasa tuwape maua yao wanastahili,” alisema Manka.
Kocha wa zamani wa Marsh Queens ya Mwanza, Godfrey Chapa anasema ushindani walionao washambuliaji hao umekuwa ukishuhudiwa mara kwa mara katika ligi hiyo huku akiwapongeza wachezaji wazawa kwa kuendelea kupambana na kutoa ushindani kwa wazawa.
“Hii siyo mara ya kwanza tumewahi kuona misimu ya nyuma ushindani wa Aisha Masaka na Oppah Clement, Clara Luvanga na Asha Djafari au Aisha Mnunka na wengine, jambo hili linaendelea kuongeza ladha kwenye ligi yetu na kuifanya iwe ya kuvutia,” anasema Chapa.